OFISA Habari wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Karim Boimanda, amesema kuwachagua waamuzi kutoka Morocco kuchezesha Dabi ya Kariakoo kati ya Simba dhidi ya Yanga, si pendekezo la klabu, bali ni muongozo wa kanuni za ligi hiyo.

Kauli ya Boimanda imekuja baada ya TPLB kuwatangaza waamuzi wa mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara itakayochezwa kesho Jumapili Mei 3, 2026 saa 12 jioni kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Dar es Salaam.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Boimanda amesema: “Waamuzi hawakuja kwa pendekezo la klabu, bali kanuni inaruhusu, kamati inapoona kuna umuhimu wa kutoa waamuzi kutoka ndani itafanya hivyo, kama itateuwa kutoka nje  pia inaruhusiwa,”

Waamuzi waliochaguliwa kuchezesha mechi hiyo ni Hamza El Fareq (mwamuzi wa kati), Lahsen Agaou (mwamuzi msaidizi namba moja), Hamza Massiri (mwamuzi msaidizi namba mbili) na Mustapha Kechaf (mwamuzi wa nne wa mezani) ambao wote ni raia wa Morocco.

Kanuni ya 39 ya Ligi Kuu toleo la 2025 inayozungumzia waamuzi, imefafanua jambo hilo.

Kanuni hiyo ya 39 kifungu cha 7.1, inasema: “Kamati ya Waamuzi ya TFF inaweza kupanga mwamuzi/waamuzi kutoka nje ya Tanzania kwenye Michezo ya Ligi Kuu.”

Hii itakuwa mara ya pili kwa Dabi ya Kariakoo ndani ya Ligi Kuu Bara kuamuliwa na waamuzi kutoka nje, ambapo msimu uliopita mchezo wa mwisho baina ya timu hizo uliochezwa Juni 25, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, uliamuliwa na waamuzi kutoka Misri na Yanga kushinda 2-0.

Mwamuzi wa kati alikuwa Amin Mohamed Amin Omar, huku Mahmoud Ahmed Abo El Regal akiwa mwamuzi msaidizi namba moja na Samir Gamal Saad Mohamed ni mwamuzi msaidizi namba mbili, Ahmed Mahrous alikuwa mwamuzi wa nne wa mezani, hawa wote kutoka Misri, huku mtathimini waamuzi akiwa Alli Mohamed wa Somalia.

Akizungumzia kuhusu utaratibu wa kuingia uwanjani, Boimanda amesema: “Mageti yatafunguliwa kuanzia saa 7 mchana, mashabiki wale wenye tiketi ndio wataruhusiwa kuingia, vinywaji havitaruhusiwa kesho.”

Simba na Yanga zinakutana katika duru la pili la Ligi Kuu Bara baada ya ile ya kwanza Machi Mosi 2026 kumalizika bila ya kufungana, mechi ikichezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Mbali na hilo, timu hizo zinakutana ndani ya siku nne kwani zimetoka kucheza fainali ya Kombe la Muungano iliyochezwa Aprili 29, 2026 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar ambapo Simba ilishinda bao 1-0. Mwamuzi wa kati wa mechi hiyo akiwa Dickens Mimisa Nyagrowa raia wa Kenya, huku wasaidizi wake ni Ally Mbwana na Yusuf Shombe wote wakiwa kutoka Zanzibar, huku Isihaka Mwalile akiwa mwamuzi wa nne mezani kutoka Tanzania Bara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *