BAADA ya kuanza na sare, Kocha Mkuu wa Mbeya City Salum Mayanga amesema namna bora na ya uhakika kwa timu hiyo kubaki salama Ligi Kuu ni muunganiko wa wadau, mashabiki na timu nzima, huku akiipigia hesabu ‘Dabi’ ya Mbeya.
Mayanga alitua kikosini humo hivi karibuni kuchukua nafasi ya Mecky Maxime aliyeachana na timu hiyo kufuatia matokeo yasiyoridhisha, ambapo jana aliiongoza dhidi ya Mashujaa na kuambulia pointi moja katika suluhu ya bila kufungana.
Hata hivyo, timu hiyo imekuwa na matokeo yasiyoridhisha katika Uwanja wa Sokoine kwani katika michezo yote waliyocheza uwanjani hapo ya Ligi Kuu hawajapata ushindi ukiachana na ile ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Bandari FC.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mayanga amesema mwanzo huo si mbaya sana ikizingatiwa na muda aliokabidhiwa majukumu, akieleza kuwa ameridhishwa na ubora wa timu japokuwa alihitaji ushindi.
Amesema kwa sasa namna bora ya kuinusuru timu hiyo ni muunganiko, mshikamano na umoja kwa wadau, mashabiki, viongozi na timu kwa ujumla kuhakikisha michezo iliyobaki wanapata matokeo mazuri.
“Ili tuwe salama lazima tushinde mechi nyingi zinazokuja, tunayo kazi kubwa ya kufanya ili tuweze kuwa salama, mwanzo huu si mbaya kwakuwa ni mapema sana tangu nianze kazi” amesema Mayanga.
Kwa upande wake, nahodha wa timu hiyo, Eliud Ambokile amesema sare dhidi ya Mashujaa si matokeo mazuri sana kwao ikizingatiwa wapo nyumbani, akiahidi mchezo ujao kufanya vizuri na kujiweka nafasi nzuri.
“Bado hatujapata ushindi hapa lakini si matokeo mabaya sana kwetu tunapokuwa nyumbani, tutaendelea kupambana kuhakikisha tunainusuru timu kutoshuka daraja” amesema straika huyo.
Kwa sasa timu hiyo iliyopo nafasi ya 14 kwa pointi 18 inatarajia kushuka tena uwanjani kuwakabili ndugu zao Tanzania Prisons, mchezo ukipigwa Mei 4 katika Uwanja wa Sokoine jijini humo, huku ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa 2-1 mechi ya awali.