
KOCHA Malale Hamsini, ameweka wazi kuachana na Klabu ya KVZ inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar baada ya kufikia makubaliano ya pande mbili kuhusu masuala ya kusitisha kimkataba.
Malale ambaye aliwahi kuinoa Mbeya City kabla ya kutimka KVZ msimu huu, alisema uamuzi huo haujatokana na mgogoro wowote, bali ni hatua ya kawaida ya kitaaluma inayompa nafasi ya kuangalia mwelekeo mpya wa maisha yake ya soka huku akijikita pia kwenye mambo binafsi kwa sasa.
“Nimeachana na KVZ kwa makubaliano maalum ya kimkataba. hakukuwa na tatizo, ni maamuzi ya pamoja kwa manufaa ya pande zote,” alisema kocha huyo.
Aliongeza kuwa, kwa sasa hana haraka ya kusaini klabu mpya, akisisitiza kuwa anasubiri ofa sahihi itakayolingana na malengo yake ya baadaye ndani ya soka.
“Kwa sasa nataka kupumzika kidogo na kuendelea na mambo yangu binafsi huku nikisubiri ofa nzuri itakayokuja,” aliongeza.
Malale alisema mechi ya mwisho aliyocheza ilikuwa dhidi ya Azam FC katika mashindano ya Kombe la Muungano, mchezo uliokuwa na ushindani mkubwa ambapo Azam ilishinda 2-0.
“Mchezo wangu wa mwisho ulikuwa dhidi ya Azam kwenye Kombe la Muungano. Ilikuwa mechi nzuri na yenye ushindani mkubwa,” alisema.