Arusha. Jeshi la Polisi nchini linawashikilia watu watatu wanaodaiwa kujihusisha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii, ikiwemo kufanya utapeli, kutukana na kudhalilisha wengine, wakiwemo viongozi mbalimbali katika jamii, pamoja na wajumbe wa Tume ya Kuchunguza Matukio Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Mei 2, 2026 na Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi, David Misime, watuhumiwa hao walikamatwa katika mikoa ya Arusha, Iringa na Mbeya baada ya kubainika kujihusisha na vitendo vinavyokiuka sheria za makosa ya mtandaoni.

Hatua hiyo ya kukamatwa kwa watuhumiwa inakuja siku chache baada ya mmoja wa wajumbe wa tume hiyo, Jaji Mkuu mstaafu, Profesa Ibrahim Juma, kueleza kuwa wamepokea zaidi ya ujumbe 300 wa matusi baada ya kuwasilisha ripoti yao kwa Rais Samia Suluhu Hassan Aprili 23, 2026.

Profesa Juma aliyasema hayo jijini Dar es Salaam, Jumanne, Aprili 28, 2026, alipozungumza na wahariri na waandishi wa habari.

“Katiba inasema wazi kwamba kila mtu ana haki ya kuwa na maoni. Sasa kuna vikundi ambavyo vinataka maoni yao ndiyo yasikike, na hii unaiona dhahiri kwenye mitandao ya kijamii. Mtu akijitokeza akitoa maoni yake, anashambuliwa kama nyuki.

“Nadhani hiyo siyo afya. Tunataka tuwe na soko la mawazo. Mtu ambaye hukubaliani na mawazo yake unamsikiliza, nawe unatoa maoni yako. Sisi wengine, baada ya taarifa kutoka, tumepokea simu za matusi zaidi ya 300 kwa sababu kuna mtu hataki maoni yetu yaliyopatikana kwa njia ya metodolojia ambayo tumeonyesha yasijulikane kwa Watanzania.”

Ameongeza, “Nadhani ni jambo la hatari sana. Unaposema wewe ni muumini wa demokrasia na haki za binadamu, kuwa tayari kusikiliza maoni na mawazo ambayo hupendi kuyasikiliza,” alisema.

Hata hivyo, taarifa ya Jeshi la Polisi imesema msako unaendelea kuwabaini na kuwakamata watu wengine wanaodaiwa kushiriki kusambaza ujumbe wa matusi, uchochezi, chuki na upotoshaji kupitia mitandao ya kijamii.

“Tunaendelea kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano wanaotupa katika kuwafichua wahalifu hawa. Ushirikiano huo umetusaidia kudhibiti matukio mengi na hali ya usalama inaendelea kuwa shwari,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Hata hivyo, hatua hiyo imeibua mjadala miongoni mwa wadau wa sheria na haki za binadamu, wakitaka vyombo vya dola pia kuelekeza nguvu katika kushughulikia masuala makubwa ya kitaifa, hususan madai ya vurugu zilizotokea wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Akizungumza na Mwananchi, Wakili Peter Madeleka amesema pamoja na umuhimu wa kudhibiti matusi mitandaoni, bado kuna haja ya vyombo vya dola kushughulikia kikamilifu matukio ya vurugu yaliyosababisha vifo na uharibifu wa mali wakati wa uchaguzi.

Amesema katika kipindi ambacho taifa linaendelea kuomboleza waliopoteza maisha katika matukio hayo, ni muhimu kwa vyombo vya dola kufanya kazi kwa weledi na kuepuka hatua zinazoweza kuonekana kama za kuwaonea wengine.

“Matusi ni kosa la jinai na hayapaswi kuvumiliwa, lakini kwa sasa taifa linahitaji majibu kuhusu waliopanga na kutekeleza vurugu za uchaguzi wa 2025. Hilo ni jambo kubwa zaidi linalohitaji uwajibikaji,” amesema Madeleka.

Ameongeza kuwa kila mtu ana haki ya kulindwa heshima yake, lakini pia vyombo vya dola vinapaswa kuweka kipaumbele katika masuala yenye athari kubwa kwa usalama na mshikamano wa taifa.

Kwa upande wake, Wakili Fulgence Massawe kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), amesema hali ya sasa ya kijamii na kisiasa nchini inahitaji uvumilivu mkubwa wa maoni tofauti.

Amesema siyo kila kauli kali inaweza kuchukuliwa kama tusi bila kuangalia muktadha wake na kusisitiza umuhimu wa kujenga utamaduni wa kujibu hoja kwa hoja badala ya kutumia lugha ya matusi.

“Ili kujua kama ni tusi lazima uangalie ujumbe wenyewe unasemaje. Katika jamii yenye mitazamo tofauti ya kisiasa na kiitikadi, si rahisi kumridhisha kila mtu. Kinachotakiwa ni kutumia lugha ya staha na kujenga hoja,” amesema Massawe.

Ameongeza kuwa katika mazingira ya taifa lililogawanyika kimtazamo, ni muhimu kujenga utamaduni wa kusikilizana na kuheshimiana, hata pale ambapo mtu hakubaliani na mawazo ya mwingine.

“Nchi inahitaji kujenga daraja la maelewano. Kama tunataka kuvuka salama, lazima tujifunze kutumia lugha ya staha na kuheshimu maoni ya wengine,” ameongeza.

Aidha, ameshauri kuwa uwezo wa vyombo vya dola katika kutumia intelijensia kuwabaini wahalifu wa mtandaoni unaweza pia kuelekezwa katika kubaini wahusika wa matukio makubwa zaidi ya uhalifu, ikiwemo vurugu za uchaguzi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *