
Dodoma. Wadau wa maendeleo nchini wameitaka Serikali kuwachukulia hatua watu wote waliotajwa katika ripoti za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zilizowasilishwa hivi karibuni kwa Rais Samia Suluhu Hassan ili iwe fundisho kwa wengine.
Kauli hiyo imekuja ikiwa zimepita wiki kadhaa tangu CAG alipokabidhi ripoti hiyo ambayo imeonyesha kuwa na ubadhirifu wa mali za Umma.
Ofisa Utafiti na Uchambuzi wa Sera kutoka Taasisi ya Wajibu, Mcheleli Machumbana, ametoa kauli hiyo Aprili 30,2026 Jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasilisha uchambuzi wa ripoti za CAG kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Machumbana anasema baada ya kuwasilishwa ripoti hizo, sasa ni nyaraka za umma ambazo zinaruhusiwa kusomwa na Mtanzania yeyote na kutoa maoni na mapendekezo kwa ajili ya kuboresha maeneo yaliyotajwa kuwa na upungufu.
Amesema katika uchambuzi huo, wamebaini maeneo kadhaa yenye upungufu, ikiwemo usimamizi wa bajeti, viashiria vya rushwa pamoja na matumizi yasiyo na tija.
“Mfano wa karibu ni kwamba, mwaka huu CAG amesema katika mwaka wa fedha 2024/25 kulikuwa na matumizi yasiyo na tija ya Sh171 bilioni, tofauti na zaidi ya Sh300 bilioni zilizoripotiwa katika mwaka wa fedha uliopita, hivi tunawezaje kuwaacha wahusika,” amesema Machumbana.
Kwa mujibu wa mchambuzi huyo, ripoti hizo zimeonesha changamoto katika mashirika ya umma, ikiwemo hasara inayoongezeka katika Shirika la Ndege la Air Tanzania ambayo hasara yake imeongezeka hadi kufikia zaidi ya Sh700 bilioni, kiwango alichosema ni kikubwa kulinganisha na miaka yote tangu shirika hilo lianze kufanya kazi.
“Tumeona pia kwenye ujenzi wa uwanja wa michezo wa Arusha, ambapo CAG amebainisha kuwa makadirio ya mradi yalikuwa Sh181 bilioni, lakini matumizi yanaonesha zitafikia zaidi ya Sh300 bilioni hali inayoashiria ongezeko la asilimia 81, bado wanataka kulindana,” amehoji.
Anapendekeza kuwa, Serikali na vyombo vingine washirikiane kuhakikisha wanatekeleza mapendekezo yote yaliyowasilishwa na CAG ili kuimarisha usimamizi wa fedha za umma.
Hata hivyo, amewahimiza wananchi kusoma ripoti mbalimbali za CAG, ikiwemo ripoti ya Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, miradi ya maendeleo pamoja na mashirika ya umma, ili waweze kutoa maoni na michango yao katika kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Amani Africa Organization, Anna Frank amesema kuwa asilimia kubwa ya mikopo inayotolewa haifiki kwa walengwa wenye uhitaji halisi, badala yake hunufaisha wachache na vingi ni vikundi hewa.
Anna anasema ni wakati sasa kwa Serikali kuhakikisha mikopo inayotolewa inawafikia walengwa husika, kwani kwa kiasi kikubwa imekuwa vigumu kwa mtu kupata mkopo bila kuwa na ukaribu au kufahamiana na wahusika jambo ambalo si sahihi.
Ameyataja masharti yaliyowekwa kwa watu wenye ulemavu kupata mikopo kwamba yamekuwa kikwazo kwa wahitaji wengi, akitolea mfano sharti la mlemavu kutakiwa kuwa kwenye kundi la walemavu wasiopungua watano ili aweze kupata mkopo.
Hata hivyo kwa sasa Serikali imeweka utaratibu kuwa mtu mwenye ulemavu anaweza kupata mkopo akiwa peke yake ilimradi akizi vigezo.