
Matokeo mazuri katika michezo mitano mfululizo yameonekana kumpa jeuri Kocha Mkuu wa TRA United, Ettiene Ndayiragije, akitamba kuwa hesabu si za nafasi nne tu bali hata ubingwa, ili kuitambulisha rasmi timu hiyo kimataifa.
TRA United, ambayo ilijulikana kama Tabora United na Kitayosce FC ya mkoani Tabora, haijapoteza mechi kati ya tano ilizocheza mfululizo msimu huu na kuwa nafasi ya tano kwa pointi 30.
Katika michezo hiyo, imeshinda minne dhidi ya Singida Black Stars, Pamba Jiji na Tanzania Prisons (Zote Ligi Kuu Bara) na Namungo (Kombe la Shirikisho la CRDB), huku ikitoa sare moja mbele ya Simba (Ligi Kuu Bara), na Mei 4 itakuwa kibaruani dhidi ya Mashujaa.
Hadi sasa bingwa mtetezi Yanga ndiye kinara wa Ligi Kuu akiwa na pointi 47, ambapo kesho Jumapili atakuwa na shughuli pevu dhidi ya watani wao Simba waliopo nafasi ya pili kwa pointi 42.
Akizungumza jijini Mbeya, Ndayiragije raia wa Burundi, amesema matokeo mazuri ni kutokana na kujituma kwa wachezaji wake, wakipewa nguvu na mazingira bora yaliyowekwa na uongozi ndani na nje ya uwanja.
Amesema wakati kwa sasa wakiufikiria mchezo ujao dhidi ya Mashujaa, hesabu zao zinawaza mbali ikiwamo nafasi nne za juu na ubingwa, ili kuitambulisha zaidi TRA United kwa wadau ndani na nje ya nchi.
“Kujituma kumezaa matokeo mazuri, niwashukuru wachezaji na uongozi ambao unatupa sapoti kubwa. Tunaiwaza sana nafasi ya nne, lakini hata ubingwa ili kuitambulisha TRA United kimataifa,” amesema kocha huyo.
Ndayiragije, ambaye alitua Tanzania kwa mara ya kwanza 2017 katika kikosi cha Mbao FC ya Mwanza akitokea Vital’O, aliifikisha fainali ya Kombe la Shirikisho (kwa sasa CRDB). Alizifundisha pia Geita Gold, KMC, Azam FC na timu ya taifa ya Stars kwa mafanikio.
Hata hivyo, kabla ya kutua kwa ‘Wakusanya Kodi’ hao, alikuwa akiinoa Police FC ya nchini Kenya, aliyoipa taji la Ligi Kuu msimu uliopita, na sasa anasaka rekodi nyingine, huku vita ya ‘Top Four’ Ligi Kuu Bara ikiwa na upinzani mkali kuanzia Yanga, Simba, Azam, JKT Tanzania, Pamba Jiji na Singida Black Stars ambazo zimepishana pointi chache.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Christina Mwagala, amesema pointi 17 walizoachwa na Yanga si nyingi sana, hivyo mkakati wao ni kuendeleza ushindi kila mchezo, akitamba kuwa msimu huu wana jambo lao Ligi Kuu.
“Tunatarajia kurejea tena Mbeya kumalizia mechi yetu ya mwisho dhidi ya Mbeya City. Tutaomba sherehe zetu za ubingwa tufanyie hapa. Uwezo na nia tunayo, kimsingi tunahitaji kuendeleza ushindi,” amesema Christina.