
Dar es Salaam. Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) kupitia Mpango wa Ubunifu wa Funguo limeendelea kubadilisha mazingira ya ujasiriamali nchini Tanzania, baada ya kuwekeza mabilioni ya shilingi katika biashara bunifu zinazoanzishwa na vijana wa vyuo vikuu.
Katika hafla ya Tuzo za #YouthIgnite Awamu ya Tatu na Uzinduzi wa Wito wa Tano wa Ufadhili wa Kichocheo wa Funguo, iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Funguo imetunuku biashara 20 zilizoanzishwa na wanafunzi.
Hatua hiyo imesababisha jumla ya biashara zilizoungwa mkono kufikia 60 kupitia awamu tatu, na kuonesha ukuaji wa mchango wa vyuo vikuu katika uundaji wa ajira na maendeleo ya uchumi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja wa Mradi wa Funguo, Joseph Manirakiza amesema tangu kuanzishwa kwake, Funguo imewekeza Sh7.5 bilioni katika biashara changa bunifu 88 pamoja na kusaidia zaidi ya nusu ya biashara hizo kupata Sh18 bilioni za mitaji ya ziada.
“Kwa pamoja, biashara hizi zimechangia kuzalisha na kudumisha zaidi ya ajira 10,000 nchini Tanzania,”amesema.
Hata hivyo, Manirakiza ametangaza kuongezeka kwa msaada kwa vituo saba vipya vya ubunifu vinavyotegemea vyuo vikuu, hivyo kufikisha jumla ya vituo vinavyoungwa mkono kote nchini kufikia 17.
“Vituo hivi vina mchango muhimu katika kulea wajasiriamali wachanga kupitia mafunzo, ushauri elekezi, ujasiriamali shirikishi, na upatikanaji wa rasilimali za awali,” amesema.
Hafla hiyo pia ilishuhudia uzinduzi rasmi wa Wito wa Tano wa Ufadhili wa Kichocheo wa Funguo, unaolenga biashara bunifu na changa zinazofanya kazi kwenye mnyororo wa thamani wa kilimo, ubunifu wa kidijitali na madini muhimu sekta zilizopewa kipaumbele katika maendeleo ya Taifa.
Mpango wa Funguo unatekelezwa na UNDP Tanzania kwa ushirikiano na Anza Entrepreneurs, kwa msaada wa Umoja wa Ulaya, Serikali ya Finland na UK FCDO.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP Tanzania John Rutere amesema, “kwa kuwekeza katika wanafunzi wa vyuo vikuu nchini, Funguo inasaidia kufanya vyuo kuwa vichocheo vya ujasiriamali na kuongeza ajira.
“Hii inadhihirisha kinachowezekana pale ambapo kuna uwezeshaji kifedha, ushirikiano na ubunifu vinaunganishwa pamoja.”
Mwakilishi wa Umoja wa Ulaya (EU), Lamine Diallo amesema umoja huo unajivunia kuiwezesha programu ya Funguo kwa vijana, kubadili mawazo yao ya kibunifu kuwa biashara.
“Kufadhili ubunifu unaoongozwa na wanafunzi na sekta nyeti kama kilimo, ubunifu wa kidijitali na madini muhimu, kunahitajika ili ukuaji wa uchumi uwe endelevu,”amesema Diallo.
Mwakilishi wa UK FCDO, Euan Davidson amesema kupitia programu ya Funguo wanashuhudia ni namna gani uwezeshaji wa kifedha unaweza kuchochea uwekezaji binafsi, kukuza ajira na kusaidia biashara ambao zinaashiria dalili njema.
“Uzinduzi wa Wito wa Tano wa Ufadhili ni hatua muhimu katika kuwezesha ukuaji wa ubunifu Tanzania.”