
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayehusika na Masuala ya Sheria na Kimataifa ameweka wazi msimamo rasmi wa Iran kuhusu juhudi zinazoendelea kufanywa kwa ajili ya kufikiwa mapatano na Marekani.
Kazem Gharibabadi ameeleza haya alipokutana na mabalozi kadhaa wa nchi za kigeni mjini Tehran. Amesema kuwa Iran iko tayari kikamilifu kwa ajili ya kuabiliana na kitendo chochote kipya cha uchokozi, ingawa pia inaamini katika diplomasia ya kutatua masuala yaliyopo.
“Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewasilisha mpango wake kwa Pakistan kama mpatanishi kwa lengo la kukomesha kabisa vita vya kulazimishwa dhidi ya Iran, na sasa mpira uko upande wa Marekani kuchagua kati ya suluhisho la kidiplomasia au kuendeleza njia ya makabiliano,” amesema Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Anayehusika na Masuala ya Sheria na Kimataifa.
Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameongeza kuwa hata hivyo Tehran haina imani na Marekani kwa sababu ya rekodi ya Washington katika duru zilizopita za mazungumzo.
Kazem Gharibabadi ametoa kauli hii mjini Tehran baada ya mkutano wa pande tatu na mabalozi wa China na Russia nchini Iran.
Iran na Marekani zilifanya duru ya kwanza ya mazungumzo tarehe 11 Aprili katika mji wa Islamabad, Pakistan siku chache baada ya Pakistan kufanikisha kufikiwa usitishaji vita ulioepelekea kusitishwa vita vya siku 40 vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.