
Katika ujumbe huo uliosambazwa na ofisi yake, kwa njia ya video Türk ameelezea taswira ya kutisha ya hali hiyo, akisema “ingekuwa dunia ya kutojali, ambapo vurugu zinakutana na ukimya,” na ukweli unakuwa “kuuzwa kama bidhaa,” hali ambayo ingewafanya watu washindwe kutofautisha kati ya ukweli na uongo.
Dunia isiyo na ukweli
Türk ameonya kuwa bila vyombo vya habari huru, jamii ziko katika hatari ya kuingia katika hali ya kutojali na kuchanganyikiwa, ambapo ukweli unafifia na uelewa wa umma unadhibitiwa kwa urahisi.
“Dunia ambayo watu hawawezi kutofautisha kati ya ukweli na uongo,” anasema, akisisitiza hatari ya kudhoofika kwa uandishi wa habari huru.
Ameongeza kuwa “vyombo vya habari huru ni hewa ya uhai ya jamii huru na wazi,” akieleza mchango wa vyombo vya habari katika kuhabarisha mijadala ya umma, kujenga imani, na kuimarisha mshikamano wa kijamii, ustahimilivu na usalama.
Heshima kwa wanahabari walioko mstari wa mbele
Akitoa heshima kwa wanahabari duniani kote, Türk anawasifu waandishi na wapiga picha wanaohatarisha maisha yao kuandika kuhusu ukatili, kufichua rushwa, na kuwawajibisha wenye mamlaka.
“Kwa kufichua ukweli na kutoa nafasi kwa mitazamo mbalimbali, wanakuza utawala ulio wazi, shirikishi na wa kidemokrasia,” alisema, akiongeza kuwa kazi yao inaendeleza uwajibikaji na kuzuia ukiukwaji wa haki.
Taaluma iliyo katika hatari
Licha ya umuhimu wake, Türk ameonya kuwa uandishi wa habari umekuwa taaluma hatarishi zaidi.
Wanahabari “wanalipuliwa wakiwa kwenye magari yao, kutekwa kutoka ofisini, kufungwa jela, na kufukuzwa kazi,” anasema.
“Mwaka huu pekee, takribani wanahabari 14 wameuawa,” aliongeza, akibainisha kuwa hali ya kutokuwajibishwa inaendelea, ambapo ni kesi chache tu zinazopata haki kamili.
Maeneo ya vita: hatari kubwa zaidi
Kuripoti kutoka maeneo ya vita ndiko kunakobeba hatari kubwa zaidi kwa wanahabari.
Türk anavitaja vita vya Israel huko Gaza kuwa “mtego wa kifo kwa vyombo vya habari,” akibainisha kuwa karibu wanahabari 300 wameuawa tangu Oktoba 2023. Anaongeza kuwa hadi sasa mwaka 2026, Lebanon ndiyo nchi hatari zaidi kwa wanahabari.
Wanahabari wa ndani, ambao mara nyingi ndio mashahidi pekee wa vita, wanaendelea kufanya kazi katika hali ngumu. Türk amekumbuka kukutana na wanahabari nchini Sudan waliokumbana na vurugu, ukatili na hata njaa huku wakiendelea kuripoti.
Hatari nje ya maeneo ya vita
Vitisho dhidi ya wanahabari havipo tu katika maeneo ya vita. Kamishna huyo wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa anasisitiza kuwa “hakuna nchi iliyo salama kabisa kwa wale wanaosema ukweli kwa walio madarakani.”
Anataja hatari zinazowakabili wanahabari wanaochunguza rushwa, uharibifu wa mazingira na uhalifu uliopangwa, pamoja na ongezeko la ukandamizaji wa kimataifa na ufuatiliaji, ikiwemo mashambulizi dhidi ya wanahabari wa Iran walioko nje ya nchi yao.
Sheria na vitisho vya kisheria
Türk ameelezea wasiwasi wake kuhusu matumizi mabaya ya sheria kunyamazisha vyombo vya habari.
Sheria kuhusu kashfa, upotoshaji wa taarifa, uhalifu wa mtandao na ugaidi zinatumika “kulinda wenye nguvu dhidi ya uchunguzi,” anasema. Kesi za kisheria zinazolenga kuwatisha badala ya kutoa haki zimegeuza mahakama kuwa chombo cha vitisho.
Kwa mujibu wa Kamishna huyo, takriban wanahabari 330 na wafanyakazi wa vyombo vya habari wamefungwa duniani kote, pamoja na wanahabari wa kiraia na wanablogu wapatao 500.
Unyanyasaji mtandaoni pia unaongezeka kwa kasi. Wanawake wanahabari wanaathirika zaidi, ambapo robo tatu yao wamekumbana na matusi, kampeni za kuwachafua na hata unyanyasaji wa kijinsia.
Türk anaonya kuwa hali hii inaweza kusababisha “jamii ya upotoshaji,” ambapo vyombo vya habari hulazimika kuficha ukweli ili viweze kufanya kazi kwa usalama.
Shinikizo la kiuchumi na kufungwa kwa vyombo vya habari
Changamoto za kifedha pia zinaongeza tatizo. Türk anasema kupunguzwa kwa ufadhili na mkusanyiko wa umiliki wa vyombo vya habari kunasababisha vyombo vidogo kufungwa katika karibu theluthi moja ya nchi duniani, na hivyo kuwanyima watu sauti. Wakati mwingine, wafanyakazi hufukuzwa kazi kimkakati ili kukandamiza taarifa muhimu.
Wito wa kulinda ukweli
Licha ya changamoto hizi, wanahabari wanaendelea kufanya kazi katika mazingira magumu.
“Wanaamini kuwa ukweli una nguvu kuliko risasi, na unastahili kupiganiwa,” anasema Türk.
Ametoa wito kwa serikali kukomesha mateso dhidi ya wanahabari, kufuta sheria kandamizi, na kuhakikisha uwajibikaji kwa mashambulizi yote. Pia anazitaka kulinda wanahabari dhidi ya ufuatiliaji na kuhakikisha mazingira huru ya vyombo vya habari.
Makampuni ya teknolojia yanapaswa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya unyanyasaji mtandaoni na upotoshaji wa taarifa.
Uhuru uko hatarini
Akihitimisha ujumbe wake, Türk ameonya kuhusu madhara makubwa ya kudhoofika kwa uhuru wa vyombo vya habari.
“Mashambulizi dhidi ya vyombo vya habari yanapokuwa ya kawaida, uhuru huanza kudorora, na pamoja nao misingi ya amani, usalama na maendeleo endelevu,” anasema.
Anahitimisha akihimiza hatua za pamoja kuhakikisha kuwa “wale wanaosimama kwa ajili ya ukweli hawasimami peke yao.”