
Mgonjwa mmoja amethibitika kuwa na ugonjwa huo kupitia uchunguzi uliofanywa katika maabara iliyoko ndani ya meli hiyo, pamoja na wagonjwa wengine watano wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa huo. Kati ya watu sita walioathirika, watatu wamefariki dunia, na mmoja yuko katika uangalizi maalum nchini Afrika Kusini.
WHO imesema uchunguzi wa kina unaendelea, ukiwemo vipimo zaidi vya maabara na uchunguzi wa kitabibu wa mlipuko. Huduma za matibabu na msaada zinatolewa kwa abiria na wafanyakazi wa meli, huku uchunguzi wa kinasaba wa virusi ukiendelea.
Hantavirus ni nini?
Hantavirus ni kundi la virusi vinavyoenezwa hasa na panya. Huambukiza binadamu kupitia kugusana na kinyesi, mkojo au mate ya wanyama walioambukizwa. Njia za kawaida za maambukizi ni kuvuta hewa yenye chembechembe zilizo na virusi kutoka kinyesi kilichokauka au kugusa mdomo na pua baada ya kushika vitu vilivyochafuliwa.
WHO inaeleza kuwa Hantavirus inaweza kuenea kutoka mtu hadi mtu, ingawa ni nadra, na inaweza kusababisha ugonjwa mkali wa mfumo wa upumuaji, hivyo wagonjwa wanahitaji uangalizi na matibabu ya karibu.
Kwa dalili za kitabibu, virusi hivi husababisha aina mbili kuu za magonjwa hatari: barani Asia na Ulaya, husababisha homa ya damu yenye madhara kwa figo; huku katika bara la Amerika, husababisha ugonjwa wa mapafu wa Hantavirus unaoambatana na matatizo makubwa ya kupumua na mshtuko wa shinikizo la damu, wenye kiwango cha juu cha vifo.
Hatua za dharura na tathmini ya hatari
WHO inasaidia nchi wanachama na kampuni ya meli kupanga uhamishaji wa wagonjwa wawili wenye dalili, huku ikiendesha tathmini ya kina ya hatari kwa afya ya umma na kutoa msaada kwa abiria waliobaki. Shirika hilo limepongeza ushirikiano wa haraka wa wadau wote.
Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus kupitia ukurasa wake wa mtandao wa X amesisitiza kuwa hatua za haraka na zenye uratibu ni muhimu kudhibiti hatari na kulinda afya ya umma.
Aidha, WHO imearifu mashirika ya kitaifa ya mawasiliano ya nchi wanachama kwa mujibu wa Kanuni za Afya za Kimataifa na itatoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu mlipuko wa ugonjwa huo.
Matibabu na kinga
Kuzuia Hantavirus kunategemea kudhibiti na kuangamiza panya. Kwa sasa hakuna dawa maalum inayopatikana kwa wingi, hivyo matibabu yanategemea zaidi huduma saidizi.
Katika maisha ya kila siku, kudumisha usafi wa mazingira ya kuishi na kazi, kuziba mianya inayoweza kuingiza panya, na kuvaa barakoa na glavu wakati wa kusafisha maeneo yenye uwezekano wa kuchafuliwa na panya ni hatua muhimu za kupunguza hatari ya maambukizi.