Arusha. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam imemhukumu Ramadhan Muhunzi, kifungo cha miaka 12 jela, baada ya kumkuta na hatia ya kosa la kujaribu kumuua mfugaji, Kaburu Lacha (78).

Tukio hilo lilitokea eneo la Makurunge wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, Novemba 29, 2024, mshtakiwa alivamia na kuchoma nyumba zake na kumkata kwa panga sehemu mbalimbali za mwili wake na kusababisha madhara makubwa.

Hukumu hiyo imetolewa Aprili 30, 2026 na Jaji Arnold Kirekiano, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya jinai namba 13314/2025.

Hukumu hiyo ilitolewa na Jaji Kirekiano Aprili 30, 2026 kufuatia usikilizwaji wa ushahidi kutoka kwa mashahidi saba wa upande wa mashtaka pamoja na utetezi wa mshtakiwa mwenyewe, ambaye aliamua kujitetea bila uwakilishi wa wakili licha ya kupewa fursa hiyo.

Jaji amesema baada ya kuchambua ushahidi wote uliowasilishwa mahakama imeridhika bila kuacha shaka yoyote kuwa mshtakiwa ndiye aliyefanya kitendo hicho.

Amesema utambuzi wa mshtakiwa ulifanywa na mashahidi waliomfahamu kabla ya tukio hilo lililotokea mchana hivyo kuridhika upande wa mashtaka umethibitisha kosa la kujaribu kuua na Mahakama kumhukumu kifungo cha miaka 12 jela.

Ilivyokuwa

Ramadhan alipatikana na hatia ya kosa la kujaribu kuua, kinyume na Kifungu cha 211(a) cha Kanuni ya Adhabu.

Katika kuthibitisha kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi saba ambao ni Dk Makubu Gushi, H6667 Koplo Abdallah, Inspekta Dastan Wilbard, Kaburu, Maria Kaburu (binti wa mwathirika wa tukio hilo), Julius Benjamin na F4300 Sajenti Edson.

Walidai baada ya kumshambulia, mshtakiwa aliendelea kuharibu mali kwa kuwachinja ng’ombe wa mwathiriwa.

Kaburu alidai siku ya tukio, mshtakiwa alifika nyumbani kwake akiwa na panga alimkata nalo kichwani, kidole kimoja cha mkono wa kushoto na kumjeruhi sehemu zingine mbalimbali ikiwamo begani, tumboni na shingoni.

Alidai kutokana na majeraha hayo alianguka chini na kupoteza damu nyingi huku akimshuhudia mshtakiwa kiendelea kuwakata ng’ombe wake kwa panga hilo na baadaye alipelekwa hospitali.

Shahidi wa tano na sita walidai kushuhudia tukio hilo na kuwa walimuona mshtakiwa akimkata Kaburu kwa panga huku shahidi wa nne akieleza walimpeleka Hospitali ya Bagamoyo na baadaye akahamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Shahidi wa tatu aliieleza Mahakama akiwa na maofisa wenzake wa Jeshi la Polisi, walipofika eneo la tukio walimpokonya mshtakiwa panga hilo na kuumizwa na mshtakiwa.

Shahidi wa kwanza aliyempokea mwathiriwa katika Hospitali ya Bagamoyo alieleza mahakamani kuwa majeraha aliyokuwa nayo yalikuwa makubwa na ya kina, yakionesha matumizi ya silaha yenye ncha kali.

Amedai kutokana na hali mbaya ya mwathiriwa, alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi ili kuokoa maisha yake.

Kumbukumbu za Mahakama zinaonesha kuwa mshtakiwa alikataa msaada wa kisheria wa bure (huduma ya wakili) na kujiwakilisha mwenyewe huku akikanusha tuhuma zilizomkabili.

Katika utetezi wake, amesema kutokana na maelezo ya tukio, inawezekana alihusika, lakini hakutoa maelezo ya kina wala kuhoji ushahidi wa mashahidi waliotoa ushuhuda dhidi yake na hahitaji maswali.

Alipohojiwa na wakili wa Jamhuri kuhusu kukamatwa kwa panga na kukamatwa kwake, mshtakiwa alikataa kujibu.

Uamuzi Jaji

Jaji amesema Mahakama ilizingatia misingi ya kisheria katika kufikia uamuzi wake, ikiwamo wajibu wa upande wa mashtaka kuthibitisha kosa bila kuacha shaka yoyote.

Jaji alieleza kuwa, ushahidi uliotolewa ulikuwa thabiti, unaoendana na unaothibitisha bila shaka kuwa mshtakiwa ndiye aliyefanya shambulio hilo.

Aidha, Mahakama ilichambua kwa kina suala la nia ya kuua, ikizingatia aina ya silaha iliyotumika, maeneo ya mwili yaliyolengwa, idadi ya majeraha pamoja na ukubwa wake.

Amesema Mahakama imebaini kuwa mashambulizi yalilenga sehemu nyeti za mwili ambazo zinaweza kusababisha kifo, hivyo kuthibitisha kuwepo kwa nia ya kuua.

Mahakama pia ilizingatia kuwa kifo hakikutokea kutokana na msaada wa haraka uliotolewa na ndugu wa mwathiriwa pamoja na huduma za kitabibu,hivyo kitendo hicho kilibaki katika hatua ya jaribio la kuua.

Katika hatua ya kutoa adhabu, upande wa mashtaka uliiomba Mahakama itoe adhabu kali kutokana na ukatili wa tukio hilo, matumizi ya silaha hatari na kutokuwepo kwa dalili zozote za majuto kutoka kwa mshtakiwa.

 Pia, ulieleza kuwa mwathiriwa alikuwa mzee na dhaifu, hivyo alihitaji ulinzi zaidi kutoka kwa jamii.

Kwa upande wake, mshtakiwa aliomba kupunguziwa adhabu akidai kuwa ana wazazi wazee wanaomtegemea.

Katika uamuzi wake, Jaji Kirekiano alibainisha kuwa pamoja na kuzingatia hali binafsi za mshtakiwa, jamii inahitaji kulindwa dhidi ya watu wenye tabia za vurugu, akisisitiza kuwa adhabu hiyo inalenga kutoa funzo kwa wengine na kuhakikisha haki inatendeka kwa mwathiriwa.

Baada ya kuchambua ushahidi wa pande zote mbili, Mahakama ilimhukumu mshtakiwa kutumikia kifungo cha miaka 12 jela.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *