Dodoma. Licha ya mambo mawili kuonekana yatakula muda wa vikao vya Bunge, lakini kuna dalili itakuwa wiki iliyochangamka na mpishano wa mijadala kutoka na wizara zilizopangwa kuwasilisha bajeti zao.

Miongoni mwa mambo yatakayofanyika ndani ya Bunge wiki hii ni uchaguzi wa wabunge watatu kwa ajili ya kuziba nafasi za Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kwa ajili ya kuziba nafasi zilizo wazi.

Jambo jingine nje ya mjadala wa bajeti ni hotuba ya Rais wa Kenya, William Ruto ambaye atalihutubia kesho Jumanne, Mei 5, 2026.

Mawaziri ambao wiki hii watakuwa na jukumu la kuwasilisha bajeti zao na kujibu hoja mbalimbali ambazo zitaibuliwa ni Paul Makonda (Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo), Jumaa Aweso (Maji) na Profesa Adolf Mkenda wa Elimu, Sayansi na Teknolojia atahitimisha wiki.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda. Picha na Maktaba

Bajeti ya Makonda itakuwa ya siku moja huku Aweso na Profesa Mkenda wao ni siku mbili. Mwananchi limezungumza na wadau mbalimbali juu ya matamanio yao wanayowiwa kuyasikia kutoka kwenye bajeti hizo.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ameizungumzia sekta ya habari akisema hakutakuwa na kitu kipya ikiwa Waziri Makonda hatakuja na suluhisho la kilio cha wamiliki wa vyombo vya habari ambacho kimedumu kwa zaidi ya miaka 10 sasa.

“Mimi naamini anaweza kukonga nyoyo za watu ikiwa atafanya jambo moja kubwa nalo ni kutoa kauli ya anafufuaje uchumi wa vyombo vya habari na kwenye hilo hakuna jinsi ila ni kutoa kauli ya kuachia wizara na taasisi ili ziendelee kutangaza na vyombo vya habari na kulipa kwa wakati,” amesema Balile.

Mwenyekiti huyo amesema wamiliki wanapitia magumu isipokuwa mwenye kuyamaliza ni Waziri Makonda kama atakuja na mageuzi.

Mbali na hilo, suala la upatikanaji wa habari kwa mujibu wa sheria ya vyombo vya habari ya 2026 bado linatajwa kuwa na mkwamo kwani taasisi nyingi zimegeuza kivuli cha kutokutoa habari na kutengeneza mlolongo mrefu.

Kwa Makonda pia anategemewa kukazia kwenye uandishi wa weledi ikiwamo uthibitisho wa waandishi waliosajiliwa kwa Bodi ya Ithibati (JAB) kwani sheria hiyo inaonekana kulegea kwa baadhi ya vyombo vya habari na badala yake husimama pale wanapobaini kuna kosa limefanyika.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso. Picha na Maktaba

Bajeti ya Aweso

Changamoto ya maji, miradi kutokamilika kwa wakati na ubambikiwaji wa ankara ni miongoni mwa mambo ambayo Waziri Aweso anatarajia kukutana nayo kutoka kwa wawakilishi wa wananchi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Waziri Aweso aliitisha semina ya wabunge wote akiwaeleza namna miradi ya uchimbaji visima inavyokwenda kutekelezwa.

Uamuzi huo unatafsiriwa kama njia ya kuwazima midomo wakati wa kuchangia hotuba hiyo kwani kila mmoja atakaonekana kama mtu anayeifahamu wizara.

Mmoja wa wabunge wa siku nyingi kutoka mikoa ya kati, amesema mpango huo ni sawa na kufuli na kufungia midomo akieleza waziri amefanya hivyo baada ya kuona hoja zilizokuwa zikijitokeza hasa kwenye mitambo ya kuchimbia visima ambayo inatajwa kuwa utaratibu wake hauko wazi.

Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Msafiri Frank yeye amesema: “Tatizo la maji ni kubwa, maeneo mengi ya Dar es Salaam yana changamoto, sijajua waziri atakuja na nini kutueleza na si ajabu na maeneo mengine mikoani hali bado lakini maneno ni mengi.”

Waziri wa Elimu, Profesa Adolf Mkenda. Picha na Maktaba

Profesa Mkenda

Ingawa lilijadiliwa wakati wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, suala la michango shuleni linaweza kujirudia tena wakati Profesa Mkenda atakapowasilisha bajeti yake ya mwaka 2026/27.

Ujenzi wa Vyuo vya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta), lugha ya kufundishia, uhaba wa walimu kwa baadhi ya masomo hususan ya sayansi, teknoloajia inavyochagiza mabadiliko ya mitalaa vyuoni na mikakati ya Serikali kuhakikisha wahitimu wanaendana na soko la ajira ni miongoni mwa mambo yanayomsubiri.

Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Dodoma, Samwel Mkotya amesema katika wizara hiyo anategemea kauli ya zuio la michango isiyo ya kiholela ambayo imekuwa ni kero kubwa kwa wazazi wa watoto wa shule za msingi na sekondari.

Mkotya amesema ujenzi wa miundombinu kwa sasa hakuna shaka na mazingira ya kazi kwa walimu yanaridhisha hivyo kwa namna yoyote itakavyokuja, hana shaka na bajeti isipokuwa eneo la michango.

“Mimi sipingi kuhusu michango lakini enzi tulizofundisha sisi na wakati huu siyo, kama Serikali imefanikiwa kujenga miundombinu ya namna hii basi suala la michango nalo liwekewe utaratibu, kuna michango ya chakula, taaluma au kitu ambacho wazazi wamekubaliana haina shida, lakini isiwe kila kukicha ni michango mingine inawaumiza wanyonge, waziri alisemee hili,” amesema Mkotya.

Mwalimu huyo mstaafu amesema akiona mkakati wa maboresho na kuongeza majengo kwa ajili ya kupokea wanafunzi wengi 2028, nalo litakuwa jambo la heri ambalo analisubiri kwa hamu kubwa ili isijekuwa ni zimamoto kwa bajeti ya 2027/28.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *