Dar es Salaam. Wakati Kamati Kuu ya Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) ikitarajiwa kukutana kesho Jumanne, Mei 5, 2026 kumteua mgombea Ubunge wa Isimani, mkoani Iringa, wagombea watatu wamejitokeza kuitaka nafasi hiyo.

Kikao hicho kinatarajiwa kufanyika katika ofisi za Makao Makuu ya chama hicho zilizopo  Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Aprili 20, 2026 Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), ilitangaza uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo hilo utakaokwenda sambamba na uchaguzi wa udiwani katika kata 12 za Tanzania Bara utakaofanyika Juni 1, 2026.

Uchaguzi wa Isiman unafanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Lukuvi kufariki dunia Machi 25, 2026 kwa ugonjwa wa mshtuko wa moyo.

Mbali ya kuwa mbunge, pia Lukuvi hadi anakutwa na umauti, alikuwa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu).

Akizungumza leo Jumatatu Mei 4, 2026 na Mwananchi kuhusu mchakato ulipofikia ndani ya chama hicho katika uchaguzi huo, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Chaumma, John Mrema amesema, hadi kufika jana wanachama watatu walikuwa wamejitokeza.

Shughuli ya uchukuaji na urejeshaji fomu ndani ya chama hicho ulikoma ulikoma jana saa 10:00 jioni.

“Hadi jana saa kumi kamili jioni ambapo tulitangaza ingekuwa mwisho kwa wanachama wote wenye nia ya kugombea nafasi hiyo, wawe wamechukua na kurejesha fomu, watatu walikuwa wameshafanya hivyo.

“Hivyo kinachofuata ni kamati kuu kuketi kesho (Mei 5, 2026), kwa ajili ya kuteua jina la mtu mmoja ambaye atapepereshusha bendera katika uchaguzi huo akikiwakilisha chama,”amesema Mrema.

Kuhusu uchaguzi mdogo katika kata, Mrema amesema kati ya kata 12 zilizotangazwa na INEC, Kata 10 wamepata wagombea huku Kata ya Mzimuni iliyopo Wilaya ya Kinonodoni jijini Dar es Salaam ikiongoza kuwa na wagombea wengi.

Kwa mujibu wa Mrema katika kata hiyo wagombea watano wameweza kujitokeza, ambao nao kesho katika Kamati watachagua jina moja la atakayegombea.

Hata hivyo, Mrema aliwataka wananchi na jamii kwa jumla kujua kwamba katika uchaguzi huo ikiwamo ule wa ubunge, Chaumma hawaendi kufanya majaribio na kueleza kuwa wana uhakika wa ushindi.

“Kama kuna watu wanadhani tunakwenda Isimani kufanya majaribio, wakae wakijua sisi tunaenda kwa nia ya kuchukua jimbo na tuna uhakika tunalipata kwa kuwa watu ambao wamejitokeza kulitaka ni watu makini wenye kuaminiwa kwenye jamii,” amesema.

Alipoulizwa kwa namna jimbo hilo lilivyokaliwa kwa muda mrefu na Chama cha Mapinduzi (CCM) hawaoni kama watakuwa na kibarua kigumu.

Katika majibu yake, Mrema amesema hilo haliwatishi kwa kuwa wanachoona wote pamoja na hao CCM wanakwenda kama wagombea wageni.

Amesema hii ni kwa sababu miaka yote 30 iliyokaliwa na Mbunge wa chama hicho hakuna jipya watakalokwenda kuwaeleza wananchi wawaelewe kwa kuwa hakuna walichowafanyia.

“Sisi Chaumma nadhani sera na agenda zetu zinajulikana, kikubwa ni kujenga ushawishi kwa wananchi waweze kutuelewa na hatimaye watuunge mkono na tunaamini watafanya hivyo,” amesema Mrema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *