
Dujarric ametoa kauli hiyo muda mfupi baada ya Mkuu wa Idara ya Masuala ya Siasa na Ujenzi wa Amani, Rosemary DiCarlo, kuhutubia wajumbe wa Baraza la Usalama wakati wa kikao cha faragha kilichokutana kujadili mashambulizi ya siku ya Jumatatu ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
UAE imesema kwamba Iran ndiyo iliyohusika na mashambulizi hayo, lakini jana Jumanne Iran ilikanusha kuhusika.
“Bi. DiCarlo amesisitiza kwamba tangu mwanzo wa mgogoro huo tarehe 28 Februari, Katibu Mkuu alilaani mashambulizi yote yasiyo halali katika Mashariki ya Kati na kwingineko,” amesema Dujarric.
Ushirikiano wa kidiplomasia unaoendelea
Amemnukuu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akisema kuwa “naye amesisitiza kwamba azimio la Baraza la Usalama 2817 (2026) lazima liheshimiwe na raia pamoja na miundombinu ya kiraia lazima ilindwe.”
Azimio hilo, lililopitishwa mwezi Machi mwaka huu, lilitolewa kufuatia mashambulizi ya Iran dhidi ya nchi kadhaa jirani.
Dujarric amesema Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu kwa mgogoro wa Mashariki ya Kati, Jean Arnault, anaendelea na mashauriano ya kidiplomasia katika eneo hilo na alipangwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki Jumatano.
Amesisitiza kwamba “Umoja wa Mataifa unaendelea kujitolea kuunga mkono juhudi zote zinazolenga suluhisho la kina na la kudumu la mgogoro huu.”
Tishio dhidi ya usalama wa kikanda: Bahrain
Kikao hiki cha faragha cha Baraza la Usalama kinafuatia ombi la Bahrain baada ya mashambulizi ya Iran dhidi ya UAE yaliyolenga kituo cha mafuta huko Fujairah, na kusababisha uharibifu pamoja na majeruhi miongoni mwa raia.
Wawakilishi wa Kudumu wa Bahrain na UAE wote walizungumza na waandishi wa habari kabla ya kikao.
Mwakilishi wa Kudumu wa Bahrain kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Jamal Fares Alrowaiei amesema “mashambulizi hayo ya kikatili” ni “sehemu ya mwenendo wa makusudi na unaoongezeka wa vitendo vya kuvuruga utulivu ambavyo vinatishia usalama na uthabiti wa eneo la Ghuba.”
Halikadhalika, amesema ni “ukiukaji wa wazi” wa azimio 2817 (2026) “na yanaonesha kitendo cha Iran kuendelea kutotekelezwa azimio hilo.”
Si tukio la pekee: UAE
Mwakilishi wa Kudumu wa UAE, Balozi Mohamed Abushahab, aliwaambia waandishi wa habari kwamba Iran ilirusha makombora 12 ya masafa marefu, makombora matatu ya aina ya ‘cruise’, na ndege nne zisizo na rubani , jambo lililosababisha moto katika eneo la viwanda vya mafuta la Fujairah na kuathiri vibaya miundombinu muhimu ya nishati ya kiraia.
“Ulinzi wa anga wa UAE uliweza kuzuia vitisho vingi hivyo, hivyo kupunguza uharibifu. Hata hivyo, raia watatu walijeruhiwa,” amesema.
Amesisitiza kwamba “hili halikuwa tukio la pekee” kwani UAE “imezuia zaidi ya makombora 500 ya masafa marefu, karibu makombora 30 ya ‘cruise’ na zaidi ya ndege zisizo na rubani 2,000 zilizorushwa kutoka Iran” tangu tarehe 28 Februari, mgogoro katika Mlango wa Hormuz ulipoanza.
Meli bado zinashambuliwa
Zaidi ya hayo, meli za kibiashara katika njia hiyo muhimu ya bahari zinaendelea kushambuliwa.
“Na kinachotokea katika Mlango wa Hormuz hakiishii huko tu,” amesema. “Kinathiri vibaya masoko ya nishati, minyororo ya ugavi, bei za chakula na uthabiti wa uchumi duniani kote.”
Mwakilishi wa kudumu wa UAE amelitaka Baraza la Usalama “kuchukua hatua madhubuti kujibu ukiukaji wa Iran na tishio wazi kwa amani na usalama wa kimataifa,” akisisitiza kwamba “ndiyo maana wakati huu ni muhimu.”
Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya bahari, (IMO) limethibitisha shambulizi la Jumanne dhidi ya meli ya Ufaransa, San Antonio, katika Mlango wa Hormuz, shambulio ambalo liliwajeruhi mabaharia wanane. Shirika hilo limethibitisha matukio 32 na vifo 10 hadi sasa.