
Mbunge wa Viti Maalumu, Asha Baraka ameiomba Wizara ya Elimu kuangalia upya utaratibu wa elimu ya awali na msingi ili kupunguza mzigo kwa watoto wanaotembea umbali mrefu kwenda shule.
Akichangia bajeti ya Wizara ya Elimu kwa mwaka wa fedha 2026/27 bungeni jijini Dodoma leo Alhamisi, Mei 7, 2026, Asha amesema watoto wengi huamka alfajiri na kutembea umbali mrefu wakiwa na mizigo mizito ya madaftari, hali inayowaathiri kiafya na kisaikolojia.
Ameeleza kuwa baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na awali hujikuta wakitembea au kusubiri usafiri wakiwa wamechoka, hususan wale wanaosoma mbali na makazi yao katika maeneo ya mijini.
“Ningeshauri watoto wabebeshwe madaftari kulingana na siku husika ya masomo, ili kupunguza mzigo mkubwa wanaoubeba kila siku,” amesema Asha.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha watoto wanasoma katika shule zilizo karibu na makazi yao ili kupunguza changamoto za usafiri na uchovu.
Pamoja na hayo, ameipongeza Wizara ya Elimu kwa mafanikio makubwa katika kuboresha sekta ya elimu nchini, na kuunga mkono bajeti hiyo kwa mwaka huo wa fedha.