PALE Simba kuna balaa jipya linakuja taratibu likiwahusisha viungo wawili ambao kwa sasa wako moto.

Viungo hao ni Clatous Chama na Elie Mpanzu na jamaa ni kama wameshajipata baada ya kubezwa fulani hivi na sasa wameliamsha kombinesheni la kibabe likipasua wapinzani.

Viungo hawa wawili wamekuwa tishio wakitengeneza kitu hatari ambapo ukiona Chama ana mpira na anataka kupiga pasi basi kama Mpanzu yupo uwanjani chunga haraka, unapigwa wakati wowote na kinyume chake.

Ilianzia hapa; Ile mechi ya Simba ikiwa ugenini dhidi ya Singida Black Stars Machi 11, 2026, dakika ya 84 Chama anapokea pasi kutoka kwa Yusuf Kagoma, anampunguza mmoja kisha anainua kichwa anaangalia hesabu za Mpanzu na kumuinulia pasi fulani, kisha Mkongomani huyo kumaliza kikatili kwa shuti la mguu wa kushoto, Wekundu hao wakitengeneza ushindi muhimu.

CHAM 02

Bao la pili likafuata dhidi ya Yanga Mei 3, 2026 pale Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Simba ikiwa nyumbani, Mpanzu anaanzisha shambulizi lakini mabeki wa Yanga wanalizima kisha mpira kumkuta Chama, akapiga pasi ya kuufungua ukuta wa Yanga na kumkuta tena Mkongomani huyo.

Mpanzu akatulia na kupiga hesabu kali kwa pasi yake ya kuinua ikitoka mguu wa kushoto inamkuta Chama akiwa amegeuka lakini akapiga tik tak fulani ya kiufundi wakitengeneza bao dakika ya 10 ya mchezo huo, likiwa pia bao la pili kwa Simba kwenye mechi ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Juzi tena wawili hao wakatengeneza bao lingine zuri na pekee la ushindi dhidi ya JKT Tanzania na dakika ya 53 Mpanzu alitengeneza asisti nzuri kwa mguu wake wa kulia ikimkuta Chama pembeni kidogo akatishia kama anapiga kwa mguu wa kulia lakini akaupeleka mguu wa kushoto na kupiga shuti lililojaa wavuni, Simba ikishinda. Kumbuka mechi hizo mbili dhidi ya Yanga na JKT Tanzania, Chama zote ameibuka mchezaji bora.

Kocha Steve Barker amechekelea muunganiko wa viungo hao akisema unazidi kuleta faida kwa kutengeneza mashambulizi makali yanayozalisha mabao kwenye mechi za wekundu hao.

CHAM 01

Barker amesema Chama amekuwa akitumia uzoefu wake na ufundi kutengeneza ubunifu wakati wa kutengeneza mabao na hata kufunga huku Mpanzu akizidi kuimarika baada ya kuanza taratibu msimu huu.

“Ndiyo kuna muunganiko mzuri wa Mpanzu na Chama, nadhani sihitaji kuongea sana kuhusu Chama, kila mmoja anajua namna alivyo mbunifu uwanjani, ana utulivu na uzoefu wa kutosha, amekuwa kwenye ubora mkubwa kwa sasa,” amesema Barker.

“Ukiangalia Mpanzu naye alianza taratibu lakini wakati wote nilikuwa nasisitiza hapa ni mchezaji anayetakiwa kuendelea kuitumikia Simba, sasa ameimarika, ameendelea kutengeneza na hata kufunga na wanashirikiana vizuri na wengine akiwemo Chama.

Chama mpaka sasa ameshafunga mabao matano ambapo kati ya hayo mawili aliyafunga akiwa Singida Black Stars na matatu Simba aliyojiunga nayo Januari 2026. Pia ana asisti tatu na kumfanya kuhusika kwenye jumla ya mabao nane.

Mpanzu hadi sasa amefunga mabao matatu lakini katika timu hiyo akiwa kinara wa kutengeneza asisti akifikisha saba na kumfanya kuhusika kwenye jumla ya mabao 10 ya Ligi Kuu Bara msimu huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *