Kibaha. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Mkoa wa Pwani kimesema kasoro zilizobainishwa katika ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zimekuwa zikikwamisha maendeleo ya halmashauri pamoja na Mkoa wa Pwani kutokana na usimamizi usioridhisha wa mapato ya umma.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi, Mei 7, 2026, mjini Kibaha wakati wa mkutano wa chama hicho wa kuchambua vipengele vya ripoti ya CAG vinavyohusu Mkoa wa Pwani.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Pwani, Bumija Semkondo, amesema ni muhimu kwa mamlaka husika kuwachunguza wote waliotajwa katika ripoti hiyo na kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.

“Kasoro hizi za usimamizi mbovu wa mapato zimekuwa zikichelewesha maendeleo ya halmashauri husika na Mkoa wa Pwani kwa ujumla, hivyo waliohusika wanapaswa kuchunguzwa na hatua za kisheria zichukuliwe,” amesema Semkondo.

Kwa upande wake, Katibu wa Chadema Mkoa wa Pwani, Richard Mbalase, amesema chama hicho kinaamini kuwa mchakato wa Katiba Mpya unapaswa kuharakishwa ili kuimarisha misingi ya utawala bora nchini.

“Chadema inaamini kuwa mchakato wa Katiba Mpya unapaswa kuharakishwa ili kuimarisha utawala bora nchini na kuhakikisha ifikapo mwaka 2027 katiba hiyo imekamilika,” amesema Mbalase.

Naye Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema Taifa, Azaveli Lwaitama, amesema changamoto nyingi zinazojitokeza katika mifumo ya uongozi na uwajibikaji zinaweza kupatiwa ufumbuzi kupitia kukamilika kwa Katiba Mpya.

“Dawa ya kuondoa kasoro ambazo zimekuwa zikijitokeza ni kukamilika kwa Katiba Mpya ambayo itaweka misingi imara ya uwajibikaji na usimamizi wa rasilimali za umma,” amesema Profesa Lwaitama.

Mkutano huo umefanyika ikiwa ni sehemu ya mjadala wa kisiasa unaoendelea nchini kuhusu uwajibikaji wa viongozi wa umma na utekelezaji wa mapendekezo yanayotolewa kila mwaka katika ripoti za CAG.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *