Dar es Salaam. Zamani sherehe za kuadhimisha siku za kuzaliwa ‘birthday’ za mastaa wa Bongo Movie na muziki zilikuwa kivutio kikubwa kwa mashabiki na wadau wa burudani.
Ilikuwa ni kawaida kuona mastaa wakijazana kwenye matukio hayo, wakionyesha mshikamano huku kila tukio likigeuka kuwa gumzo mitandaoni. Picha na video zilizosambaa zilionyesha ukaribu na umoja uliokuwepo miongoni mwao.
Hata hivyo, sasa ni tofauti kabisa. Hali imeanza kubadilika kwani hivi karibuni, baadhi ya sherehe za mastaa zimekuwa na mwitikio mdogo wa wasanii wenzao.
Mfano wa tukio la hivi karibuni la ‘birthday’ ya mtoto wa Paula Paul na msanii Marioo umeibua mjadala, baada ya kuonekana mastaa wachache wakihudhuria tofauti na ilivyotarajiwa na mashabiki wengi.
RATIBA ZAATHIRI
Wachambuzi wa burudani wanaeleza moja ya sababu kuu ni ratiba ngumu za wasanii wa sasa.
Ndina ambaye ni msanii wa Bongo Movie, anasema: “Kwa sasa kila mtu anapambana na kazi zake. Kuna shoo, biashara na safari nyingi, hivyo si rahisi kuhudhuria kila sherehe kama zamani.”
USHKAJI UMEPUNGUA
Mbali na ratiba, baadhi ya wadau wanaamini kiwango cha ukaribu kati ya mastaa kimepungua.
Tofauti na zamani walionekana kama familia moja, sasa ushindani wa kibiashara umechukua nafasi kubwa zaidi.
Mdau wa burudani, Mama Igwe ameliambia Mwanaspoti: “Zamani kulikuwa na ule ushikaji wa kweli, lakini sasa kila mtu anatafuta nafasi yake, hivyo sio lazima kuhudhuria kila tukio la mwenzako.”
MITANDAO NA MAISHA YA FARAGHA
Aidha, mabadiliko ya matumizi ya mitandao ya kijamii nayo yamechangia hali hiyo. Wakati zamani mastaa walitumia sherehe kama jukwaa la kujitangaza, sasa baadhi yao wamechagua kuishi maisha ya faragha zaidi.
Hii imepunguza matukio yenye msongamano mkubwa wa mastaa, kwani wengine wanapendelea kusherehekea kwa ukaribu na familia na marafiki wachache.
GHARAMΑ ΝΑ ΜΑΒADILIKO YA VIPAUMBELE
Gharama za kuandaa sherehe kubwa pia zimekuwa zikiongezeka. Hali hii imewafanya baadhi ya mastaa kupunguza ukubwa wa matukio yao na kuamua kufanya sherehe ndogo zisizo na mwaliko mpana.
Wadau wa burudani wanatoa mfano wa baadhi ya mastaa wakubwa waliokuwa wakifanya ‘birthday’ kubwa zilizojaa wasanii, lakini kwa sasa sherehe hizo zimekuwa za utulivu zaidi na kuhudhuriwa na watu wachache wa karibu.
Hali hii inaendelea kuzua mjadala kuhusu mabadiliko ya mshikamano ndani ya tasnia ya burudani.
MWISHO WA ENZI AU MABADILIKO TU?
Pamoja na mjadala unaoendelea, wapo wanaoamini si mwisho wa enzi za ‘birthday’ za mastaa bali ni mabadiliko ya mtindo wa maisha. Badala ya wingi wa watu, sasa kipaumbele kinawekwa kwenye ubora wa tukio.
Swali linalobaki ni je, ushikaji wa mastaa umepungua au ni maisha tu yamebadilika? Wakati majibu yakiendelea kutafutwa, jambo moja linaonekana wazi, ‘birthday’ za mastaa hazipo tena kama zilivyokuwa zamani.