
Simba imeuhama Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo na sasa itautumia Uwanja wa KMC Complex kwa mechi zake zilizobaki msimu huu.
Taarifa ya Simba imesema kuwa sababu ya kuhama Uwanja ni kutokana na hali mbaya ya hewa.
“Kutokana na hali ya hewa ya mvua kuendelea kunyesha jijini Dar es Salaam kikosi chetu kimerejea kucheza mechi za nyumbani katika Uwanja wa KMC
Complex.
“Hii ina maana kuwa mechi zetu zilizosalia za msimu wa Ligi Kuu ya NBC 2025/2026 ambazo tutakuwa nyumbani tutacheza katika Uwanja wa KMC Complex.
“Mchezo wetu wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Tanzania Prisons utapigwa Jumapili Mei 10 utakuwa wa kwanza kupigwa katika Uwanja
wa KMC Complex,” ilifafanua taarifa ya Simba jana.
Uamuzi wa Simba kuuhama Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo umefanywa siku moja baada ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC iliyofanyika katika uwanja huo.
Simba ilihamia katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, Oktoba mwaka jana baada ya serikali kutangaza kuufungia Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Imecheza idadi ya mechi tisa katika Uwanja huo ikipata ushindi katika mechi saba na kutoka sare mbili.