Nahodha wa Real Madrid, Fede Valverde ataukosa mchezo dhidi ya Barcelona ‘El Classico’ Jumapili mwishoni mwa wiki hii kufuatia maumivu aliyoyapata baada ya kupigana na Aurelien Tchouameni katika mazoezi ya timu hiyo jana Jumatano, Mei 6, 2026.

Inaripotiwa kwamba baada ya ugomvi huo, Valverde alionekana kuzidiwa na kukimbizwa hospital kwa matibabu zaidi na hali hiyo inamfanya akose mechi ya Jumapili.

Japo Real Madrid haijatoa taarifa yoyote hadi sasa, inasemekana kwamba hali ya Valverde bado haijawa sawa kiasi cha kumfanya awe na utayari wa kucheza mechi hiyo.

Na Tchouameni pia inadaiwa naye ataukosa mchezo huo kutokana na adhabu ya klabu baada ya kufanya kosa hilo.

Wawili hao inadaiwa walianza kurushiana maneno na kisha wakageuza uwanja wa mazoezi ulingo wa masumbwi pindi timu ilipokuwa na program ya kujiandaa na mchezo wa El Classico.

Tukio hilo limeonekana kuibua mijadala katika maeneo mbalimbali duniani huku wengi wakiinyooshea kidole Real Madrid kuwa imeshindwa kudhibiti nidhamu za wachezaji wake katika miaka ya hivi karibuni.

Mchezo dhidi ya Barcelona katika Uwanja wa Nou Camp Jumapili hii ni muhimu kwa Real Madrid kuibuka na ushindi ili ibaki na matumaini finyu ya kutwaa ubingwa wa La Liga msimu huu.

Zikiwa zimebaki mechi nne, Real Madrid iliyopo nafasi ya pili kwenye msimamo wa La Liga, imezidiwa kwa pointi 11 na Barcelona inayoongoza msimamo ikiwa na pointi 11.

Matokeo ya ushindi au sare ya aina yoyote katika mchezo huo, yataihakikishia Barcelona ubingwa wa msimu huu ambao itakuwa ikitwaa kwa mara ya pili mfululizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *