Dar es Salaam. Wadau wa sekta ya ujenzi wa meli nchini wametaka kuwepo kwa udhibiti madhubuti ili kuondoa watu wasiokuwa na taaluma wanaojihusisha na kazi hiyo na kuhatarisha usalama wa vyombo vya majini.
Baadhi ya washiriki kutoka sekta binafsi wameeleza pamoja na umuhimu wa kanuni mpya, bado kuna haja ya kutoa elimu kwa wananchi ili wamiliki wa vyombo vya majini waelewe umuhimu wa kufuata taratibu rasmi za ujenzi.
Wamesema bila elimu ya kutosha baadhi ya watu wanaweza kukimbilia kutumia mafundi wasio rasmi ili kukwepa gharama na taratibu jambo ambalo linaweza kuongeza ajali na changamoto za kiusalama katika usafiri wa majini.
Hayo yamesemwa katika kikao cha kwanza cha wadau wa sekta hiyo kilichoandaliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) jijini Mwanza.
Akizungumza Mei 7, 2026 Mkurugenzi wa Udhibiti, Ulinzi, Usalama na Utunzaji wa Mazingira ya Usafiri Majini wa Tasac, Leticia Mtaki amesema Tanzania haiwezi kuendelea kutegemea kuagiza vyombo vya majini kutoka nje wakati mahitaji ya usafiri wa majini yanaongezeka kila siku.
Amesema kikao hicho ni kinalenga kujadili fursa zilizopo katika sekta ya ujenzi wa meli pamoja na namna ya kujenga sekta imara ya utengenezaji wa vyombo vya majini.
Mkurugenzi wa Kampuni ya HB Marine Expert Limited ya Kigoma, Hemed Hemed
Mtaki amesema ongezeko la biashara kupitia bandari, maendeleo ya uchumi wa buluu, shughuli za uvuvi, mafuta na gesi pamoja na usafiri wa majini vinaonyesha wazi kuwa mahitaji ya vyombo vya majini yataendelea kuongezeka nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
“Kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikiagiza vyombo vya majini kutoka nje ya nchi. Hali hii imekuwa ikisababisha matumizi makubwa ya fedha za kigeni na changamoto za upatikanaji wa huduma za matengenezo pamoja na vipuri,” amesema Mtaki.
Amesema hali hiyo inapaswa kuwa fursa ya kujenga uwezo wa ndani katika ujenzi, ukarabati na utengenezaji wa meli pamoja na vyombo vingine vya majini.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kuimarisha uchumi wa buluu pamoja na maendeleo ya viwanda.
Amesema sekta ya usafiri wa majini imepewa nafasi muhimu katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inayolenga kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kisasa, shindani na unaotegemea viwanda pamoja na teknolojia.
“Serikali imeweka msisitizo mkubwa katika kuimarisha miundombinu ya usafiri wa majini, kukuza uchumi wa buluu kwa matumizi endelevu ya bahari, maziwa na mito pamoja na kuongeza ajira kwa vijana kupitia ujuzi wa ufundi na teknolojia,” amesema.
Meneja wa Ukaguzi na Usajili wa meli Tasac, Said Kaheneko amesema uwasilishaji wa michoro ya vyombo vya majini kwa si jambo la hiari bali ni lazima kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Amesema shirika hilo tayari limetoa mwongozo kupitia Merchant Shipping Notice namba 28 ya mwaka 2024 unaobainisha michoro yote inayotakiwa kuwasilishwa kabla ya ujenzi wa chombo kuanza.
“Tasac pia imeandaa kanuni za matumizi ya taasisi zinazotambulika kimataifa za ukaguzi wa viwango vya ujenzi wa meli (Classification Societies) ili kuhakikisha vyombo vinavyojengwa vinakidhi viwango vya usalama na ubora,”amesema Kaheneko.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kampuni ya HB Marine Expert Limited ya Kigoma, Hemed Hemed amesema sekta hiyo imevamiwa na watu wasiokuwa na utaalamu jambo linalochangia kujengwa kwa vyombo visivyokidhi viwango.
Amesema baadhi ya watu wanaofanya kazi hizo hutumia vifaa visivyokidhi viwango hali inayoweza kuhatarisha usalama wa vyombo vya majini.
“Tasac inapaswa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini watu wanaofanya kazi hizo bila utaalamu na kuwachukulia hatua,”amesema Hemed.
Meneja wa Ukaguzi na Usajili wa Meli Tasac, SaId Kaheneko akizungumza na wadau wa ujenzi wa meli hawapo pichani jijini Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mkombozi Fishing and Marine Transport Limited, Ibrahimu Chacha amesema serikali inapaswa kuwaunga mkono zaidi wawekezaji wa ndani ili waweze kukuza sekta hiyo.
Amesema kampuni yake inamiliki meli 10 katika Ziwa Victoria lakini bado wawekezaji wa ndani wanahitaji kuwezeshwa zaidi ili kufanya vizuri katika sekta ya ujenzi wa meli.