Wanawake na wasichana nchini Lebanon wanaendelea kuuawa, kujeruhiwa na kukimbia makazi yao licha ya usitishaji mapigano dhaifu ulioanza kutekelezwa Aprili 17 mwaka huu, limeonya leo Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake UN Women.

Akizungumza kutoka Beirut katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi hiileo, Mkurugenzi wa Kanda ya Nchi za Kiarabu wa UN Women, Moez Doraid, amesema mashambulizi ya anga ya Israel, maagizo ya watu kuhama na vizuizi vya kurejea katika baadhi ya maeneo vinaendelea kuwaathiri raia.

© UNICEF/Fouad Choufany Watoto hucheza katika ua kati ya mahema katika makazi ya muda ya pamoja huko Beirut, Lebanoni.

Kwa mujibu wa Doraid, wanawake 25 wameuawa na wengine 109 kujeruhiwa katika kipindi cha wiki tatu zilizopita wakati raia wakijaribu kurejea nyumbani.

“Hali ya kibinadamu nchini Lebanon bado ni dhaifu na haitabiriki, huku hatari ya kuongezeka tena kwa mapigano ikiendelea kuwepo,” alisema Doraid.

Zaidi ya wanawake na wasichana nusu milioni wamekimbia makazi yao

UN Women imesema zaidi ya wanawake na wasichana laki tano wameendelea kuwa wakimbizi wa ndani kutokana na uharibifu mkubwa wa nyumba na vijiji kusini mwa Mto Litani.

Shirika hilo pia limeonya kuhusu kuongezeka kwa uhaba wa chakula, likisema takribani wanawake na wasichana 144,000 zaidi wanaweza kuingia katika kiwango cha dharura cha njaa katika miezi ijayo, na kufanya jumla ya walioathirika kufikia karibu watu 639,000.

Mwanamke mmoja aliyekimbia makazi yake alinukuliwa akisema amelazimika kutafuta mimea ya porini ili kuwalisha watoto wake.

Licha ya changamoto hizo, Doraid amepongeza juhudi za wanawake na mashirika yanayoongozwa na wanawake kwa kuendelea kusaidia shughuli za kibinadamu, kujenga mshikamano wa jamii na kusaidia maisha ya watu walioathirika.

Tangu Machi 2, UN Women imesema imewasaidia moja kwa moja wanawake na wasichana zaidi ya 15,000 huku watu zaidi ya 70,000 wakinufaika kupitia huduma mbalimbali za kijamii na misaada.

Gaza yaendelea kushuhudia mashambulizi na matatizo ya afya

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Msaada kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema mashambulizi ya anga, mizinga na mapigano yanaendelea katika maeneo mbalimbali ya Ukanda wa Gaza.

© WFP/Maxime Le Lijour Maria, mwenye umri wa miaka 8, ameketi nje ya hema lake katika mji wa Gaza.

Kwa mujibu wa ripoti ya shirika hilo, shule moja ya UNRWA katika eneo la Jabalia ilipigwa risasi huku watu wawili waliokuwa wamekimbia makazi yao wakijeruhiwa ndani ya eneo hilo.

Ripoti hiyo pia imeonya kuwa vizuizi vya kuingiza jenereta, mafuta ya mashine na vipuri vinaendelea kusababisha kuvurugika kwa huduma muhimu za afya, usafi wa mazingira na uondoaji wa vifusi.

UNRWA imesema pia magonjwa ya ngozi kama upele na tetekuwanga yanaongezeka kwa kasi, huku kliniki kadhaa zikianza kuripoti ongezeko la watoto kung’atwa na panya.

Hofu ya mgogoro wa Hormuz kwa uhakika wa chakula duniani

Katika hatua nyingine, mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Huduma za Miradi UNOPS, Jorge Moreira da Silva ameonya kuhusu hatari ya mgogoro wa usafirishaji wa mbolea kupitia Mlango Bahari wa Hormuz kuathiri uhakika wa chakula duniani.

Akizungumza katika mkutano wa mawaziri wa nchi za MED9++ ulioandaliwa kwa pamoja na serikali za Italia na Croatia, alisema Umoja wa Mataifa uko tayari kusaidia kuhakikisha upatikanaji salama wa mbolea na malighafi zake kupitia mfumo wa uwazi, uwajibikaji na uaminifu.

Onyo hilo linakuja wakati mvutano unaoendelea Mashariki ya Kati ukiendelea kuongeza hofu ya kuathiri biashara ya kimataifa, misaada ya kibinadamu na uhakika wa chakula duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *