KOCHA Mkuu wa Gunners FC ya Dodoma, Henry Mkanwa amesema licha ya kukabidhiwa timu hiyo katikati ya msimu wa 2025-2026, ila ameshangazwa na uwezo mkubwa wa wachezaji wa kikosi hicho, kinachoshiriki Ligi ya Championship kwa mara ya kwanza.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mkanwa amesema wachezaji wengi ni vijana na wanashiriki ligi hiyo kwa mara yao ya kwanza, ila mwenendo na ushindani wanaoendelea kuuonyesha kutoka kwenye timu nyingine ni ishara tosha ya ukomavu mkubwa.

“Malengo ya timu ni kupambana ili ibakie kwenye ligi msimu ujao, hadi sasa mwenendo wetu siyo mbaya na tuko bado nafasi za katikati ambazo tukiendelea na ushindani huu ni dhahiri tutatimiza malengo tuliyoweka,” amesema Mkanwa.

MKAN 01

Mkanwa aliyezifundisha Biashara United na Pamba Jiji, amepewa jukumu hilo hadi mwisho wa msimu huu, baada ya aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Mathias Wandiba kujiunga na Fountain Gate, akiwa ni msaidizi wa Kocha Fredy Felix ‘Minziro’.

Awali timu hiyo ilianza msimu huu chini ya Kocha Juma Ikaba, aliyeondoka kwa makubaliano ya pande zote mbili, kisha nafasi yake kuchukuliwa na Mathias Wandiba aliyejiunga na Fountain Gate ya Ligi Kuu Bara.

Ikaba aliyefundisha Gwasa, Usalama na Baobab Queens, aliiongoza Gunners tangu ikiwa Ligi ya Mkoa (RCL) hadi Championship, ingawa, aliachana nayo tangu Januari 2026, kisha timu kukabidhiwa Wandiba.

MKAN 02

Gunners imepanda Championship msimu huu baada ya kuongoza First League kundi B na pointi 35, ikishinda mechi 11, sare mbili na kupoteza moja, ikiungana na Hausung kutoka Njombe, iliyoongoza kundi A na pointi 25.

Baada ya timu hizo kuongoza makundi yao na kupanda Championship, zilicheza mechi ya fainali kusaka bingwa mpya wa First League msimu wa 2024-2025 na Gunners ilitwaa ubingwa huo kwa kuifunga Hausung mabao 3-0.

Katika mechi 24, ilizocheza msimu huu timu hiyo imeshinda nane, sare tano na kupoteza 11, ikiwa nafasi ya tisa na pointi 29, huku safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho kutoka Dodoma kikifunga mabao 23 na kuruhusu 34.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *