BEKI wa kati wa Geita Gold, Ally Ally amesema ubora na upana wa kikosi hicho ndiyo sababu ya kufanya vizuri msimu huu na kukiri ushindani umekuwa mkubwa kutokana na timu zote kupigania kumaliza nafasi mbili za juu kwenye msimamo.
Nyota huyo aliyejiunga na kikosi hicho akitokea Bigman FC aliyoongoza kwa kuifungia mabao matano msimu uliopita, amesema uwepo wa wachezaji wengi bora katika kila eneo unachangia kufanya vizuri kwa Geita, huku akitoa onyo kwa wapinzani wao.
“Tunachokifanya kwa sasa ni ishara tosha kwa wapinzani wetu kujua tunapambania nini, malengo yetu siyo kupanda Ligi Kuu Bara ila kumaliza mabingwa kwa maana ya nafasi ya kwanza, uwezo huo tunao kutokana na wachezaji waliopo,” amesema Ally.
Nyota huyo aliyewika na timu mbalimbali zikiwemo, KVZ, Yanga, Stand United na KMC, amesema licha ya ushindani mkubwa wa wapinzani wao, hilo kwao haliwatishi, kwa sababu wanachofanya ni kuhakikisha kila mechi wanayocheza wanafanya vizuri.
Licha ya kucheza beki, amefunga mabao manne sawa na wachezaji wenzake wa Geita, Yusufu Mhilu na Omary Hassan Omary, akibakisha bao moja kuifikia rekodi yake ya msimu wa 2024-2025, aliyoiweka akiwa Bigman FC, aliyoifungia mabao matano.
Geita iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, 2024-2025 wa Championship ilimaliza ikiwa nafasi ya nne na pointi 56, chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mohamed Muya na kushindwa kurejea Ligi Kuu Bara, baada ya kufeli mechi za ‘Play-Off’.
Timu hiyo ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudia ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2 kisha kuchapwa ugenini 2-0.
Geita ndiyo timu iliyopoteza mechi chache za msimu huu na kikosi hicho kimechapwa mara moja, kati ya 24, ikiwa ni kichapo cha mabao 2-0, dhidi ya Polisi Tanzania kwenye Uwanja wa Ushirika, Moshi, Februari 20, 2026.
Msimu huu wa 2025-2026, Geita imeshinda mechi 19, sare nne na kupoteza moja kati ya 24, ikiwa kileleni na pointi 61, ikifuatiwa na Kagera Sugar ya pili na pointi 58, baada ya kikosi hicho kushinda 18, sare nne na kupoteza mbili.