
Nchini Tanzania Umoja wa Mataifa kupitia shirika lake la Chakula na Kilimo (FAO) linaendelea kuhakikisha kuwa Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs ikiwemo kutokomeza umaskini na kuendeleza wanawake yanaendelea kutekelezwa ipaswavyo ifikapo mwaka 2030.
Miongoni mwa hatua za FAO ni awamu ya pili ya Mradi wa Pamoja wa Kigoma, (KJP) na Mradi wa kuimarisha sekta ya uvuvi, Fish4ACP unaotekelezwa mkoa wa Kigoma ulioko kaskazini-magharibi mwa Tanzania, ambako ujio wa wakimbizi ulileta changamoto si kwao tu bali pia kwa wenyeji.
Hivi karibuni, Mwakilishi Mkazi wa FAO Tanzania Nyabenyi Tito Tipo alitembelea mkoa huo kuona hali ya utekelezaji na mgao wa vifaa vya kuimarisha sekta ya uvuvi ambapo ziara ilianzia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, ambapo mazungumzo yalijikita katika kuimarisha ushirikiano na kupitia utekelezaji wa programu.
Mtambo wa kutengeneza barafu huku ukikausha samaki
Kisha Mwakilishi Mkazi wa FAO Bi. Nyabenyi alishiriki hafla ya makabidhiano ya Kiwanda cha Barafu cha Katonga chini ya mpango wa Fish4ACP. Walikata utepe kuzindua mtambo wa kutengeneza barafu.
Hassan Rugwa Katibu Tawala Mkoa wa Kigoma akatoa maelezoa akisema kuwa, “sasa huu mtambo walivyoujenga unapokuwa unafanya kazi pia, si huku ndani unapooza, lakini kuna joto ambalo linazalishwa. Sasa lile joto, huu mtambo unaouona hapa kazi yake inakuwa ni kukausha. Na wenyewe unaweza kukausha dagaa wabichi kilo 500 ambao unaweza ukapata kilo 300 za dagaa wakavu kwa siku.”
Hapa Katonga na Kibirizi, teknolojia bora za usindikaji samaki zilionekana zikitumika, ikiwemo uhifadhi kwa barafu na vikaushio vya jua. Ambatamisye Issa Mwakalambile ni mdau wa uvuvi Ziwa Tanganyika.
Hakuficha furaha yake akisema, “sisi kabla hujapata huu mradi, kwa kweli tulikuwa na tatizo la upatikanaji wa samaki weng, lakini katika utunzaji wake wa barafu kulikuwa na matatizo. Huwezi ukachukua samaki Kigoma bila kuziweka kwenye barafu kuzipeleka Dar es Salaam au Tabora zinakuwa zimechoka. Sasa kwa sababu tumepata mradi. tunashukuru sana Serikali ya Tanzania na FAO kwa kutuletea mradi huu. Na FAO ni wafuatiliaji sana, wanatusaidia sana katika Mkoa wetu wa Kigoma, tumeshakaa nao vikao vingi sana wameisha tuwezesha sana. Kwa kweli tunashukuru sana.”
Tunapunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Mohammed Sheikh akatoa shukrani akisema, “tunashukuru sana. Miradi kama hii kwa sasa ndiyo ambayo tunaipa kipaumbele ili kupunguza upotevu wa mazao. Kwa hiyo, mradi huu tumeupokea kwa furaha kubwa sana. Serikali inaongeza uzalishaji lakini upotevu wa mazao baada ya mavuno ni tatizo. Kwa hiyo, juhudi zote za kupunguza upotevu wa mazao sisi tunachukua kama ni mapinduzi katika sekta ya uvuvi.”
Na Bi. Tipo hakuficha furaha yake akieleza kuwa “baada ya kushirikiana pamoja tumeona matokeo. Hii si kazi ya mtu mmoja ni kazi ya watu wote. Nashukuru hata watu waliofika kwani wamekuja kuonesha mshikamano. Asante sana.”
Ujumbe ukabisha hodi kituo binafsi cha mafunzo cha Kasangezi ambako wakulima hujumuika kupata mbinu mbalimbali za kilimo na mafunzo ya mapishi ya lishe bora, na azungumzaye ni mmiliki wa kituo ambaye ameeleza kuwa wananchi wengi wanavutiwa na ufugaji wa kuku.
Kituo cha mafunzo kwa wakulima
Kutoka hapa, msafara ukaelekea wilaya ya Buhigwe, ambako ulitembelea Kituo cha Rasilimali za Kilimo cha Kata ya Kibwigwa, ambacho kinaendelezwa kuwa kituo cha mafunzo na huduma za ugani kwa wakulima. Walitembelea mashamba darasa na mifumo jumuishi ya uzalishaji.
Changamoto katika mbinu za kilimo na usimamizi baada ya mavuno zililibainishwa, na ushauri wa kitaalamu ulitolewa papo kwa papo. Boniface Mpepo ni Afisa Ushirika akaeleza bayana kwamba kabla ya kuwezeshwa kutoka FAO kituo kilikuwa hakifanyi kazi.
“Lakini baada ya kupata ufadhili kutoka FAO kama mnavyoona kituo kimebadilika na kinafanya kazi na miundombinu mbalimbali imetengenezwa na kimekuwa ni chachu kubwa kwa wakulima wa Buhigwe. Wanakuja kupata mafunzo na sio tu wakulima hata wataalamu kwa maana ya wafanyakazi pia ambao wana mashamba yao na kuja kuchukua ujuzi na kuweza kuboresha kilimo chetu cha pili. Na pia tuna maktaba hapa kwa maana ya sehemu ya kujisomea, na pia tuna mifumo ya intaneti ambao pia kwa wakulima ambapo sehemu hawajaelewa wanaweza wakaingia mtandaoni kuweza kuwa search au matirio, na aina gani ya mbolea inataka kutumika.”
Na kisha hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwenye kituo cha MATI Mubondo. Hapa athari za mabadiliko ya tabianchi zilionekana dhahiri kwenye mashamba ya majaribio yaliyoharibiwa na mvua za mawe.
Sasa gereza la Ilagala halitumii tena kuni, kulikoni?
Hatimaye Gereza la kilimo Ilagala, miradi inayoungwa mkono na FAO katika uzalishaji wa mbegu, ufugaji, na nishati ya kuzalishwa kwa samadi au biogas, inaboresha uzalishaji na kupunguza matumizi ya kuni. Bakari Hanga ni Mkuu wa Gereza akaeleza kuwa, “kabla ya mradi huu wa gesi vunde, kwa kweli tulikuwa tunatumia kuni ambazo zinaleta uharibifu mkubwa wa mazingira. Lakini baada ya kuipata hii ukweli tumesimama sasa kutokana na uharibifu wa mazingira. Tuliingia kutunza mazingira yetu vizuri.”
Halikadhalika amesema kuwa nguvukazi ambayo tulikuwa tunaitumia katika kutafuta kuni, imehamia pia katika uzalishaji wa sehemu nyingine za mazao. “Tulikuwa tunatumia tani mbili kwa wiki na sasa hivi hatutumii kabisa. Tunaendelea kutunza mazingira yetu kwa ajili ya kuweza kuzuia uharibifu wa mazingira na kupata mvua, kama vile mazingira ya kutusaidia.”
Tamati ya ziara, Mwakilishi wa FAO Bi. Nyabenyi akazungumza.“Tumetembelea gereza la Ilagala na tulichokiona hapa kinavutia sana. Namaanisha kazi iliyofanywa na Mradi wa Pamoja wa Kigoma hususan sehemu ya FAO ni aina ya mpango jumuishi. Msaada tulioupata, unajua, ni ushirikiano—haukuwa wa FAO pekee—bali ni kutokana na juhudi na uongozi uliopo hapa, ndiyo maana mradi huu umefanikiwa. Pia nimebaini kwamba bado kuna changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinazozuia uzalishaji wa mazao wanayotumia. Hili ni jambo tunalopaswa kulijadili kwa pamoja ili kuona jinsi ya kukabiliana na changamoto hizi. Asanteni sana.”