Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Biashara, Dar es Salaam, imekataa ombi lililowasilishwa na benki za kimataifa za Standard Chartered Bank (Hong Kong) Limited na Standard Chartered Bank Malaysia Berhad, lililokuwa likiomba kuongezewa muda wa kuwasilisha notisi ya rufaa dhidi ya uamuzi wa awali wa mahakama hiyo kuhusu usajili wa hukumu ya kigeni.

Maombi hayo yaliwasilishwa mahakamani hapo dhidi ya Kampuni ya Kufua Umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL),Pan African Power Solutions (PAP) na VIP Engineering and Marketing Limited.

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Musa Pomo, Mei 5, 2026, katika shauri la maombi ya kibiashara namba 1361/ 2026, ambalo lilitokana na mgogoro wa awali wa kesi namba 67 na 75 za mwaka 2017.

Katika shauri hilo, benki hizo zilikuwa zikiomba Mahakama Kuu iruhusu kuongezwa muda wa kuwasilisha notisi ya rufaa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu iliyoahirisha kusajili hukumu yake ya Mahakama ya Nje, baada ya muda wa kisheria uliowekwa kupita.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote za pande zote mbili, Mahakama ilitupilia mbali ombi la benki hizo, ikisema kuwa hazikutoa sababu za msingi za kuongezewa muda

Historia ya mgogoro

Kulingana na kumbukumbu za mahakama, mgogoro huu unatokana na hukumu ya kigeni iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Haki ya Uingereza mnamo Novemba 2016 dhidi ya mjibu maombi wa kwanza, kutokana na makubaliano ya mkopo kati ya pande husika.

Baada ya hukumu hiyo, benki hizo ziliwasilisha maombi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kitengo cha Biashara, wakitaka hukumu hiyo isajiliwe nchini Tanzania ili iweze kutekelezwa.

Mahakama hiyo katika uamuzi wake wa upande mmoja uliotolewa na Jaji Barke Sehel Februari 9, 2017, ilisajili hukumu hiyo na kuwa hukumu ya mahakama hiyo.

Hata hivyo IPTL, PAP na VIP walifungua shauri la maombi wakiiomba mahakama hiyohiyo kuufuta usajili wa hukumu hiyo.

Pamoja na sababu nyingine walidai kuwa utekelezaji wa hukumu hiyo ungekiuka Sera ya Umma ya Tanzania kwa kudhoofisha mashauri yanayoendelea ndani ya nchi, likiwemo shauri la madai namba 229 la 2013 linalopinga uhalali wa uhamisho na ubadilishaji wa mkataba wa mkopo.

Pia walidai kuwa usajili wa hukumu hiyo haukufuata taratibu sahihi na ulipuuzia mashauri sambamba yanayoendelea nchini Tanzania.

Wajibu maombi, benki hizo kupitia wakili wake, Gaspar Nyika, walipinga hoja za waombaji wakidai kwamba utekelezaji wake haukukiuka sera ya umma; na kwamba masharti yote ya kisheria ya usajili yalitimizwa.

Mahakama hiyo katika uamuzi uliotolewa na Jaji Butamo Phillip Agosti 26, 2017, iliufuta usajili huo ikisema kuwa  shauri namba 229/2017 nchini ambalo bado lilikuwa linaendelea mahakamani nchini lilitangulia shauri la Uingereza.

Pia mahakama ilisema kuwa usajili wa hukumu hiyo  haukuzingatia shauri hilo lililokuwa linaendelea nchini, jambo lililofanya utekelezaji huo kuwa usiofaa kwa kuwa ungeweza kuleta hatari ya mgongano wa uamuzi wa kimahakama.

Safari ya rufaa

Baada ya uamuzi huo, benki hizo ziliwasilisha notisi ya rufaa na baadaye kufungua rufaa ya Madai namba 386/2022 katika Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.

Hata hivyo, rufaa hiyo ilikumbwa na changamoto za kiutaratibu,wakati wa usikilizwaji wa rufaa, wajibu rufaa waliwasilisha pingamizi la awali wakipinga uhalali wa rufaa hiyo, wakidai kuwa kulikuwa na kasoro katika utaratibu wa kuwasilisha nyaraka muhimu.

Januari 9, 2026, Mahakama ya Rufaa ilikubaliana na pingamizi hilo na kuifuta rufaa hiyo kwa kukosa uhalali wa kisheria.

Kufuatia hatua hiyo, benki hizo ziliamua kurejea Mahakama Kuu kuomba muda wa ziada ili ziweze kuwasilisha notisi mpya ya rufaa.

Hata hivyo, muda wa kisheria ulikuwa tayari umepita, hivyo waliwasilisha maombi ya kuongezewa muda chini ya kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa.

Hoja za waombaji

Kupitia mawakili wao, waombaji walieleza kuwa kuchelewa kwao hakukutokana na uzembe bali kulisababishwa na mchakato wa kisheria uliokuwa unaendelea katika rufaa ya awali.

Walidai kuwa walikuwa wamefanya juhudi zote kwa wakati na kwamba rufaa yao ilifutwa kwa misingi ya kiutaratibu tu, si kwa msingi wa hoja za kimaudhui.

Pia walieleza kuwa mara baada ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, walichukua muda mfupi kupata ushauri wa kisheria na kuandaa maombi mapya, jambo ambalo walidai ni la kawaida katika mchakato wa kisheria.

Wakirejea baadhi ya kesi za awali za Mahakama ya Rufaa, mawakili wa benki hizo walisisitiza kuwa Mahakama ina mamlaka ya kuongeza muda pale ambapo kuna sababu za msingi, hasa pale ambapo hakuna ucheleweshaji wa makusudi.

Wajibu maombi

Kwa upande wao wajibu maombi walipinga vikali ombi hilo, wakidai kuwa benki hizo zilikuwa zimechelewa bila sababu za msingi na kwamba uzembe wao katika kufuata taratibu za kisheria hauwezi kusamehewa.

Walidai kuwa kushindwa kuwasilisha nyaraka muhimu kwa wakati kulisababisha kufutwa kwa rufaa ya awali, hivyo hali hiyo haipaswi kugeuzwa kuwa sababu ya kuomba msamaha wa muda.

Aidha, walieleza kuwa waombaji hawakutoa maelezo ya kina kuhusu kipindi chote cha kuchelewa na pia walishindwa kuambatanisha nyaraka muhimu, ikiwa ni pamoja na uamuzi wanaotaka kukata rufaa dhidi yake.

Uamuzi wa Mahakama

Katika uamuzi wake, Jaji Pomo alibainisha kuwa sheria inahitaji mwombaji wa aina hii ya maombi kutoa sababu za msingi na za kuridhisha zinazoonyesha kwa nini alichelewa na kwa nini Mahakama inapaswa kutumia busara yake kumpa muda wa ziada.

Mahakama ilisisitiza kuwa kifungu cha 11(1) cha Sheria ya Mamlaka ya Rufaa ndicho kinachoongoza maombi ya aina hii, na kwamba masharti yake lazima yazingatiwe kikamilifu.

Jaji Pomo amesema kuwa ingawa Mahakama ina mamlaka ya kuongeza muda, mamlaka hayo hayapaswi kutumika kiholela bali kwa kuzingatia uhalali wa sababu zilizotolewa.

Katika uchambuzi wake, Mahakama ilibaini kuwa waombaji walishindwa kueleza kwa kina kila hatua ya kuchelewa kwao, na pia hawakutoa ushahidi wa kutosha unaoonyesha kuwa walikuwa makini katika kufuatilia haki zao ndani ya muda uliowekwa.

Mahakama pia ilikataa hoja kwamba kuchelewa kulikuwa “kiufundi tu,” ikisema kuwa hata ucheleweshaji wa kiufundi lazima uelezwe kwa uwazi na kuungwa mkono na ushahidi wa kutosha.

Baada ya kuzingatia hoja zote za pande zote mbili, Mahakama Kuu iliamua kutupilia mbali ombi la benki hizo, ikisema kuwa hazikutoa sababu za msingi za kuongezewa muda.

Mahakama pia haikutoa amri ya gharama kwa upande wowote, lakini ilisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu za kisheria kwa umakini, hasa katika masuala ya rufaa za kimataifa na usajili wa hukumu za kigeni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *