Takwimu zilizorekodiwa katika mipaka ya Iran zinaonyesha kuwa wakati wa vita vya siku 40 vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Wairani 630,000 waliingia nchini kupitia mipaka ya nchi kavu.
Katika muda wa siku hizo, mamlaka zilirekodi asilimia 62 ya watu walioingia nchini ambao walikuwa wakiishi nje ya nchi, na asilimia 38 ya wale walioihama nchi kupitia mipakani. Kurejea nyumbani Wairani 630,000 kumejiri katika hali ambayo kwa kawaida, na ilivyozoeleka katika aghalabu ya nchi zinazokumbwa na janga la vita, watu huwa wanahama na kuzitoroka nchi zao na kuishia kuwa wakimbizi alimradi tu waweze kubaki salama na kunusurika na maafa mabaya ya vita. Katika vita ilivyopigana Syria na magenge ya kigaidi, zaidi ya watu milioni sita waliihama nchi yao na kwenda kuishi ukimbizini.
Katika vita kati ya Russia na Ukraine, ndani ya muda wa wiki moja tu, zaidi ya Waukraine milioni moja waliihama nchi yao. Kwa hiyo, mwenendo ulioonyeshwa na Wairan wa kuamua kurudi nchini mwao sambamba na kuanza vita ni kinyume na mazingira yaliyozoeleka kimataifa.
Suali la kujiuliza hapa ni, mwenendo huu ulioonyeshwa na Wairan unafikisha ujumbe gani, na kwa nini una umuhimu wa kutafakariwa?
Moja ya jumbe muhimu zaidi zinazopatikana katika kadhia hii ni jinsi Wairan wanavyotiwa wasiwasi na hali ya nchi yao, wawe ni wale walioko ndani au wanaoishi nje ya nchi. Ukweli ni kwamba, sio tu hakuna tofauti kati ya Wairan wa ndani na walioko nje ya Iran, lakini wote hao wana jambo moja linalowaunganisha, ambalo ni: daghadagha na wasiwasi juu ya nchi yao.
Wasiwasi huo ni ithibati tosha ya kuonyesha kwamba, utambulisho wa utaifa uko imara, umekita mizizi, na umewakolea wananchi wa Iran. Utambulisho huo wa utaifa hauonekani kwa njia ya Wairan kurejea nchini mwao tu, lakini unadhihirika pia na kwa uwazi kwa namna mamilioni ya wananchi walioko ndani wamekuwa wakijitokeza na kumiminika mitaani kwa takribani siku 70 tangu vilipoanza vita hivyo.
Ujumbe mwingine muhimu unaopatikana katika suala hili ni hisia kali za mshikamano wa kijamii walizonazo Wairan. Kurejea nchini wakati nchi inaandamwa na vita vikali visivyo na milingano ni ishara ya mfungamano wa kina ulioko baina ya wananchi. Ikiwa vita vitasababisha watu walioko ndani kuharibiwa maisha yao na kubaki bila makazi, na kama raia walioko nje ya nchi hawataonyesha mjibizo wa kulaani mashambulizi ya mabomu na vita dhidi ya nchi yao, wavamizi hupata uthubutu zaidi wakajusuru kuendeleza vita. Kurudi nchini Wairan waliokuwa wameihajiri nchi kulionyesha kuwa wananchi hao wana daghadagha na wasiwasi mkubwa juu ya hatima ya nchi yao, pamoja na maisha na mali za wananchi wenzao.
Ujumbe mwingine muhimu ulikuwa ni wa kuonyesha wajibu na masuulia ya pamoja ya kijamii waliyonayo wananchi wa ndani na nje ya Iran wa kuilinda nchi na kutoa msukumo kwa vikosi vya ulinzi vilivyoko kwenye medani ya vita. Ukweli ni kwamba, watu wanaomiminika mabarabarani, wale wanaoitetea nchi yao kupitia mitandao ya kijamii, na wale waliokuwa wamehama na sasa wakaamua kurudi nchini ili kudhihirisha upinzani wao kwa vita vilivyoanzishwa dhidi ya nchi yao, kwa upande mmoja, wananchi wote hao wanaonyesha jinsi walivyo na imani kamili kwa utendaji wa vikosi vyao vya ulinzi katika kuilinda nchi; na kwa upande mwingine, wanasimama bega kwa bega na vikosi hivyo katika kulinda umoja wa ardhi yote ya nchi yao; na hii ndiyo maana hasa na muhimu ya uzalendo.
Sifa hii muhimu inaonekana katika nchi nyingine chache tu za eneo la Asia Magharibi.
Nukta ya kumalizia ni kwamba, mantiki na urazini walioonyesha wananchi wa Iran katika kukabiliana na vita na wavamizi ulikuwa ni wa namna ambayo, mbali na mamlaka za nchi jirani ikiwemo Uturuki, Ofisi ya Shirika la Kimataifa la Wahajiri nayo pia imetangaza na kukiri kwamba vita vya kichokozi dhidi ya Iran havikuwafanya wananchi waihame nchi yao na kukimbilia ughaibuni…/