Katika hali isiyo ya kawaida na ya nadra kuwahi kushuhudiwa, wajumbe 29 wa Baraza la Wawakilishi la Marekani wamemwandikia barua Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio wakiitaka Washington ifichue na kuweka hadharani mpango wa silaha za nyuklia wa Israel. Barua hiyo inataka kukomeshwa sera ya kiitwacho “kimya rasmi” kuhusu uwezo wa nyuklia wa Israel.

Wabunge hao wa Baraza la Wawakilishi la Marekani kutoka chama cha Democratic wameihusisha barua yao na kanuni ya ulazima wa kuwepo uwazi, na kufafanua kwa kusema: “hatari za kufanya mahesabu kimakosa, kushadidisha mivutano, na utumiaji wa silaha za nyuklia katika mazingira haya haliishii kwenye hali ya kinadharia tu.”
Wabunge hao 29 wa Marekani wameashiria mgongano uliopo katika sera za Marekani na kusema: “Hatuwezi kupanga sera thabiti ya kuzuia ueneaji wa silaha za nyuklia katika Mashariki ya Kati huku tukiwa tunaendeleza sera rasmi ya ukimya kuhusu uwezo wa silaha za nyuklia wa mhusika mkuu katika mgogoro unaoendelea hivi sasa.” 
Kwa mujibu wa Jeremy Shapiro, afisa wa zamani katika serikali ya Obama, hatua hiyo ni ishara ya kufifia kwa kiwango kikubwa sana uungwaji mkono wa jadi kwa Israel ndani ya chama cha Democratic. Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na Kituo cha Utafiti cha Pew yanaonyesha kuwa, asilimia 80 ya Wademocrat hivi sasa wanaitazama Israel kwa jicho baya na wanataka iwajibishwe kwa kutumia vipimo vilevile vya kimataifa vinavyotumika kuziwajibisha nchi zingine.
Wademocrat wametaka kuwepo na uwazi katika sera za Marekani kuhusiana na utawala wa Kizayuni katika hali ambayo, moja ya masuala nyeti na hasasi zaidi katika uga wa siasa za Marekani ni suala la utawala wa Kizayuni na sera yake yenye utata ya nyuklia. Marekani imeanzisha vita kamili kwa lengo la kuuangamiza mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, nchi iliyosaini na inayotekeleza mkataba wa NPT na inayoendesha shughuli zake za nyuklia chini ya usimamizi kamili wa Wakala wa Atomiki wa IAEA, wakati mshirika wa Washington, yaani Israel yenye mamia ya vichwa vya nyuklia ambavyo havijatangazwa, sio tu haijawahi katu kuwekewa vikwazo, lakini pia inapokea kila mwaka msaada wa kijeshi wa mabilioni ya dola. Wakati huohuo, Iran, ambayo imethibitishwa mara kadhaa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kwamba inatekeleza majukumu yake ipasavyo, imekuwa mlengwa wa vikwazo vikali kabisa na hujuma za mashambulizi ya kijeshi.
Lakini mkabala wake, kinu cha nyuklia cha Dimona kilichoko kwenye Jangwa la Negev, ambacho hakijawahi kumruhusu kuingia ndani yake hata mkaguzi mmoja wa kimataifa, kinajulikana kwa jina la “Siri Iliyo Wazi.” Siri ambayo Marekani na washirika wake wa Ulaya wako tayari kukiuka sheria zote za kimataifa ili kuitunza. Huu ni mfano mmoja tu wa utumiaji vipimo vya kindumakuwili; huu ni usanifu wa kimfumo wa kulinda ukiritimba wa nyuklia wa utawala mtenda jinai na muuaji wa watoto, yaani Israel. 

Scott McConnel, mwanasiasa wa mrengo wa kulia nchini Marekani ametamka kinagaubaga ukweli ambao ni nadra kusikika huko Washington aliposema: “Sisi tumepigana vita viwili katika karne hii kwa ajili ya kulinda ukiritimba wa nyuklia wa Israel. Labda tunaweza angalau kuzungumza kuhusu hilo.”
Kauli hiyo inaweka hadharani ukweli mchungu wa kwamba, doktrini iitwayo “utata wa nyuklia” hivi sasa si sera tu, bali ni “uongo mkubwa” ambao umegharimu roho za maelfu ya raia nchini Iran, Ghaza na Lebanon. 
Barua ya wajumbe wa chama cha Democrat katika Baraza la Wawakilishi la Marekani inaibua pia suali la kisheria ambalo Washington imekwepa kulijibu kwa muda wa karibu miongo sita. Kwa mujibu wa kifungu cha Marekebisho ya Symington ni marufuku kutoa msaada wowote wa kiuchumi au kijeshi kwa nchi inayopokea au kuhamisha teknolojia ya urutubishaji wa kinyuklia nje ya taratibu za ukaguzi wa kimataifa. Matini ya sheria hii iko wazi kabisa. Hata hivyo, hadi sasa hakuna serikali yoyote ya Marekani, iwe ya Wademocrat au Warepublican, ambayo imethubutu kufanya uchunguzi kama huo kuhusiana na Israel. Na ndio maana msaada wa kila mwaka wa dola bilioni 3.8 kwa utawala huo wa kizayuni ungali unaendelea kutolewa, wakati sheria sawa na hizo zimeidhinishwa ili kuiwekea vikwazo Pakistan. Maudhui hii ya kisheria si suala la kuaibisha tu, bali la kufedhehesha pia. Serikali ya Washington inadharau sheria iliyotungwa na Bunge lake yenyewe kwa ajili ya kulinda usalama wa Israel.
Kinachougeuza unafiki na uzandiki huu kutoka kwenye hali ya kashfa ya kisiasa na kuwa tishio dhidi ya uwepo kiuhai ni doktrini ya nyuklia ya Israel. Mwongozo huo wa nyuklia wa utawala wa kizayuni unavichukulia vita vya kikanda kama tishio dhidi ya uwepo wake, ambao katika istilahi za kimkakati unajulikana kama “Chaguo la Samson,” yenye maana ya kutoa kitisho cha kutumia silaha za aina zote ili kuepuka kushindwa. 
Gazeti la Washington Post limechapisha barua ya wabunge wa chama cha Democrat kwa Marco Rubio na kuripoti kuwa, wasiwasi huo uliopo uliongezeka baada ya jibu la mashambulizi ya makombora lililotolewa na Iran kwa uchokozi wa kijeshi ulioanzishwa na utawala wa Kizayuni na Marekani, makombora ambayo yalilenga maeneo yaliyoko karibu na kinu cha nyuklia cha Israel huko Dimona, ikiwa ni kujibu mapigo kwa mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran. Mashambulizi hayo ya Iran yalidhihirisha namna mfumo wa ulinzi wa anga wa utawala haramu wa Israel ulivyo dhaifu.
Ripoti za kuaminika zinaeleza kuwa, maafisa wa Marekani wanafikiria sinario tofauti, ambapo kama itatokezea Israel kukaribia kushindwa katika vita vya kawaida, vipi itaweza kutumia silaha za nyuklia. Mabadiliko ya msimamo wa Wademocrat si kitu kilichotokea kwa bahati mbaya. Suali linaloulizwa na wengi duniani hivi sasa ni la kuhoji kwamba “mfumo wa kimataifa unaozingatia sheria” ambao Marekani inadai kuuongoza una itibari na thamani gani ikiwa Marekani yenyewe inazikiuka waziwazi sheria hizo? 
Japokuwa barua ya wabunge Wademocrat kwa waziri wa mambo ya nje wa Marekani inaonekana kuwa na uzito mdogo kutokana na uchache wa idadi ya waandishi wake lakini inatoa wito wa indhari ya kihistoria. Barua hiyo inadhihirisha wazi hakika tatu muhimu: Kwanza ni kwamba, ukiritimba wa nyuklia wa Israel hauna tena sura ya “mwiko mtakatifu” wa sera za nje za Marekani. Pili, gharama zilizokuwa zimefichwa za ukiritimba huo, vita vyake, vikwazo, na hasara za maafa ya roho za watu hazifichiki tena. Na tatu ni kuwa, kama Marekani, ambayo ni mpiga upatu mkubwa wa marufuku ya uenezaji silaha za nyuklia, haitabadilisha hivi sasa hivi muelekeo wake juu ya suala hilo, itibari yake itapotea moja kwa moja…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *