Dar es Salaam. Baadhi ya wafungwa wenye ujuzi mbalimbali wanaokaribia kumaliza vifungo vyao wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuangalia namna ya kuwawezesha mitaji ili kuendeleza vipaji vyao wakiwa uraiani.
Mbali na hilo, wamemueleza kuangalia wafungwa waliokaa muda mrefu magerezani, wakimuomba kuangalia uwezekano wa vifungo vya nje ili kupunguza msomangamano magerezani.
Pia, wamesema licha ya kuwa na ujuzi wa fani wanaopata wakiwa magerezani, changamoto kubwa wanaoipata ni mitaji ya kujiendeleza hali inayosababisha baadhi kujikuta wakirejea kwenye vitendo vya kihalifu na kurudi tena magerezani.
Wafungwa walitoa maombi hayo leo Jumamosi Mei 9,2026 mbele ya Rais Samia aliyepita katika mabanda yao kuangalia bidhaa walizozitengeneza kutokana na ujuzi walioupata wakiwa katika magereza mbalimbali likiwemo la Ukonga jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa wafungwa hao ni Lista Chisoma ambaye alitumia fursa hiyo kumueleza changamoto zinazowakabili wafungwa wengi waliokifungoni na wanaomaliza vifungo vyao.
Kwa ujasiri uliochanganyika na unyenyekevu, Chisoma ameeleza kuwa ingawa wafungwa wengi hupata ujuzi wakiwa gerezani, changamoto kubwa huja baada ya kuachiwa kukosa mitaji na vifaa vya kuanzisha maisha mapya, hali inayowarudisha tena kwenye mzunguko wa uhalifu.
“Mheshimiwa, bado tunaomba mtuangalie kwa jicho la huruma… tumebadilika na tunajifunza,” amesema Chisoma, akisisitiza mabadiliko yanayoendelea ndani ya magereza.
Chisoma, ambaye kwa sasa ni fundi wa ushonaji, ameeleza kuwa ametumikia kifungo kwa miaka 13 na katika kipindi hicho familia yake imetawanyika, hali iliyomfanya aombe msamaha wa muda uliobaki ili aweze kurejea mapema na kuijenga upya familia yake.
Rais Samia Suluhu Hassan akizungumza na wafungwa, Grace Chiduo na Irene Mseluka, waliopata ujuzi wa kushona bidhaa mbalimbali wakiwa gerezani, katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga jijini Dar es Salaam.
Amesema alihukumiwa mwaka 2013 kutumikia kifungo cha miaka 30 kwa kosa la kulawiti, lakini baadaye alipata msamaha na punguzo la miaka mitano kupitia uamuzi wa Rais mwaka 2021.
Kwa mujibu wa hesabu yake, sasa amebakiza takribani miaka miwili kumaliza kifungo chake, kinachotarajiwa kuisha mwaka 2028.
Licha ya changamoto hizo, Chisoma ameitumia miaka yake gerezani kujijenga kielimu na kiufundi.
“Nimeingia nikiwa na elimu ya darasa la saba, lakini kwa msaada wa walezi wa magereza aliweza kufanya mtihani wa kidato cha nne akiwa ndani ya Gereza la Ukonga.Tulikuwa watano, wanne tukapita… kwa kweli tunashukuru,” amesema.
Chisoma hakuishia hapo ameeleza athari za muda mrefu wa kifungo akijitolea mfano yeye kuwa familia yake imeparanganyika kutokana na miaka 13 aliyokaa gerezani.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akitoa vyeti kwa wahitimu waliofanya vizuri katika Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi namba 28 na Uongozi Daraja la Pili Kozi namba 48 ya mwaka 2025/2026 katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT), Ukonga jijini Dar es Salaam Mei 9, 2026.
“Mama ninaomba hii miaka miwili iliyobaki unisukumie nje nipate nafasi ya kurejea mtaani mapema na kuanza upya maisha, hiki ndiyo kilio cha wafungwa wengi wanaotamani nafasi ya pili ya maisha,” amesema Chisoma.
Akijibu kuhusu uwezeshwaji wafungwa wenye ujuzi baada ya kutoka gerezani Rais Samia amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kuliagiza Jeshi la Magereza kuanzisha utaratibu wa kuwa na mfuko maalumu utakaowasaidia wafungwa wanaomaliza vifungo vyao na wenye ujuzi kupata mitaji ya kuanzia maisha mapya.
Agizo hilo limetolewa kwa lengo la kuhakikisha kuwa wafungwa hao hawajihusishi tena na uhalifu kutokana na kukosa mwelekeo pindi wanaporejea mitaani, jambo ambalo limekuwa likisababisha baadhi yao kutamani kurudi gerezani kwa makusudi.
“Nimepata nafasi ya kuzungumza na mfungwa mmoja akaniambia kwamba wengi wanaorudi (gerezani)..wanarudi kwa sababu kule nje hawajui wafanyeje, hawajui waanzie wapi. Wanafanya kwa makusudi uhalifu akamatwe ashtakiwe, arudi huku anakolala na kula bure,” amesema.
Kutokana na hali hiyo, Rais Samia amemuagiza Mkuu wa Jeshi la Magereza Kamishna Jenerali Jeremia Katungu kufanya utafiti wa kina juu ya suala hilo na kuona namna ya kuanzisha mfuko huo utakaowawezesha wafungwa wenye ujuzi kupatiwa vifaa au mtaji kidogo wa kuanzia.
Amesisitiza kuwa serikali inaendelea kufanya mageuzi ya mifumo ya magereza ili kuweka vipaumbele katika urekebishaji wa tabia unaofungamanishwa na ujuzi, lengo likiwa ni kumfanya mfungwa awe raia mwema anayeweza kuchangia katika maendeleo ya jamii atakapohitimu adhabu yake.
Rais Samia alikwenda katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji kilicho chini ya Jeshi la Magereza Tanzania ambapo imefanyika hafla ya ya kuhitimisha mafunzo ya uongozi ngazi ya juu na uongozi daraja la pili kwa maofisa wa jeshi hilo.