Baada ya kupoteza mechi sita mfululizo za Ligi Kuu England (EPL), Chelsea leo Jumamosi, Mei 9, 2026 imefurukuta na kuondoka na pointi moja ugenini dhidi ya Liverpool katika Uwanja wa Anfield.

Ikionekana kama ingeendeleza nuksi ya kupoteza mechi mfululizo baada ya bao la dakika ya sita la Ryan Gravenberch, Chelsea imeondoka na pointi moja ikishukuru bao la dakika ya 35 la Enzo Fernandez, mechi iliyoisha kwa sare ya 1-1.

Sare hiyo imezidi kuiweka Chelsea katika uwezekano mgumu wa kupata tiketi ya kushiriki ama Kombe la Europa League au UEFA Conference League msimu ujao.

Timu hiyo ambayo ipo katika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa EPL, sasa kwa kiasi kikubwa inategemea ubingwa wa Kombe la FA pekee uipe tiketi ya kucheza Europa League msimu ujao.

Kwa upande wa Liverpool, sare hiyo imewafanya wafikishe pointi 59 na hivyo kuendelea kuwepo katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa EPL.

Kabla ya sare ya leo, mechi sita za EPL ambazo Chelsea ilipoteza zilikuwa dhidi ya Nottingham Forest, Man City, Brighton, Man United, Everton na Newcastle United.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *