Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amelitaka Jeshi la Magereza kuzingatia utekelezaji wa mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai katika maeneo ambayo bado hayajaguswa kikamilifu.
Rais Samia ameyasema hayo leo Mei 9, 2026 katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji kilicho chini ya Jeshi la Magereza Tanzania ambapo imefanyika hafla ya ya kuhitimisha mafunzo ya uongozi ngazi ya juu na uongozi daraja la pili kwa maofisa wa jeshi hilo.
Amebainisha mambo makuu manne yaliyopendekezwa na Tume ya Haki Jinai yanayohitaji msukumo wa haraka ili kuboresha hali ya wafungwa na mahabusu nchini huku akisisitiza kuwa ustawi wa binadamu lazima uzingatiwe hata wanapokuwa mikononi mwa vyombo vya dola.
Rais Samia Suluhu Hassan akionyesha Tuzo ya Kinara wa Dhana ya Urekebishaji wa Wafungwa Magerezani kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, wakati wa hafla ya kuhitimisha Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi Na. 28 pamoja na Uongozi Daraja la Pili Kozi Na. 48 ya mwaka 2025/2026 iliyofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT), Ukonga, Jijini Dar es Salaam.
Pia, amekumbushia suala la ulinzi wa watoto na maadili kwamba pendekezo lake ni kuongeza mahabusu za watoto na shule za maadili ili kuhakikisha watoto hawachanganywi na wafungwa watu wazima.
Rais Samia amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuwajenga watoto kimaadili badala ya kuwaharibu zaidi kwa kuwachanganya na wahalifu sugu.
Amesema pendekezo lingine ni hitaji la bima za afya kwa wafungwa ambapo amewataka watendaji kuanza kulifanyia kazi suala hilo ili kuona namna bora ya kulitekeleza, akiamini kuwa wafungwa nao wanastahili huduma bora za afya wanapokuwa gerezani.
Rais Samia pia amegusia changamoto ya wafungwa wageni ambao nchi zao zinakataa kuwapokea baada ya kumaliza vifungo vyao hapa nchini.
Kwaya ya wafungwa wanawake akiwemo mzungu wakitumbuiza katika hafla ya kuhitimisha Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi namba 28 na Uongozi Daraja la Pili Kozi namba 48 ya mwaka 2025/2026 katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT) Ukonga Jijini Dar es Salaam leo Mei 9, 2026.
“Ingawa taratibu za kawaida ni kuwakabidhi Idara ya Uhamiaji ili warejeshwe kwao, kuna tatizo sugu la baadhi ya nchi kutowapokea raia wao.Sasa tuangalieni kisheria na tulimalize hili. Wanatoka vipi? Tunawakabidhi vipi? Wanakwenda kwao vipi? Tuliangalie hili ambalo pia ni pendekezo la Tume ya Haki Jinai,”
Aweka mkazo matumizi ya Tehama
Katika hotuba yake Rais Samia amesisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia ya kisasa katika utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Magereza, akieleza kuwa hatua hiyo si hiari bali ni lazima katika mazingira ya sasa.
Kuhusu maboresho yanayoendelea, Rais Samia ameeleza kufurahishwa kwake na kuanza kutumika kwa mahakama mtandao ndani ya magereza nchini, hatua inayotekeleza moja ya mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai kwa lengo la kuboresha mfumo wa utoaji haki.
Amesema matumizi ya mfumo huo wa kidigitali yameanza kuleta manufaa makubwa katika sekta ya haki, hususan kwa kupunguza gharama, kuimarisha usalama na kuharakisha usikilizwaji wa kesi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akitoa vyeti kwa wahitimu waliofanya vizuri katika Mafunzo ya Uongozi Ngazi ya Juu Kozi namba 28 na Uongozi Daraja la Pili Kozi namba 48 ya mwaka 2025/2026 katika Chuo cha Taaluma ya Urekebishaji Tanzania (TCT), Ukonga jijini Dar es Salaam Mei 9, 2026.
Rais Samia amebainisha kuwa awali Serikali ilikuwa ikitumia fedha nyingi kusafirisha mahabusu kutoka magerezani kwenda mahakamani, lakini sasa gharama hizo zimepungua kutokana na kesi nyingi kusikilizwa kwa njia ya mtandao bila hitaji la uhamisho wa watuhumiwa.
“Mfumo huo umeongeza usalama kwa mahabusu na askari magereza, kwani unapunguza hatari za kiusalama ikiwemo uwezekano wa matukio ya mashambulizi au majaribio ya kutoroka wakati wa usafirishaji.
Mfumo pia umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kasi ya upatikanaji wa haki, akibainisha kuwa takwimu zinaonesha ongezeko la kesi zinazosikilizwa na kukamilika kwa wakati, hatua inayosaidia wananchi kupata haki zao bila kuchelewa”.
Mageuzi magereza
Awali, Mkuu wa Jeshi la Magereza nchini, Kamishna Jenerali Jeremia Katungu, amesema jeshi hilo limeendelea kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Haki Jinai ya kuboresha vyombo vya haki jinai iliyoundwa Desemba 2022, sambamba na maelekezo ya Serikali ya kuimarisha mfumo wa urekebishaji badala ya kuzingatia adhabu pekee.
Akiwasilisha taarifa mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan, Kamishna Jenerali Katungu amesema Jeremia lengo kuu ni kuhakikisha kila mfungwa anapata nafasi ya kujifunza, kujijenga na kuandaliwa kwa maisha ya baada ya kifungo.
“Dhamira yetu ni kuhakikisha mfungwa anapotoka gerezani anakuwa raia mwenye ujuzi, nidhamu na uwezo wa kujitegemea,” amesema Katungu.
Amebainisha kuwa katika hatua ya msingi ya mageuzi hayo, Jeshi la Magereza limekamilisha mitaala mipya ya mafunzo kwa maafisa na askari wake kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo VETA, Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima Tanzania na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
Mitaala hiyo tayari imeanza kutumika katika vyuo vya mafunzo ya magereza, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha ufanisi na weledi wa watumishi wa jeshi hilo katika eneo la urekebishaji.
Aidha, amesema jeshi hilo limeandaa mwongozo mpya wa kitaifa wa utekelezaji wa programu za urekebishaji magerezani, unaogawa mchakato wa malezi ya wafungwa katika hatua nne kuu: mapokezi, kipindi cha kutumikia kifungo, maandalizi kabla ya kuachiwa, na hatua ya kurejea katika jamii.
“Baada ya uzinduzi wa mwongozo huo, mafunzo maalumu yameanza kutolewa kwa watumishi wa ngazi mbalimbali, ambapo wakuu wa magereza yote nchini na maofisa waandamizi tayari wamepatiwa mafunzo hayo.
“Tunalenga kuhakikisha mwongozo huu unatekelezwa kwa ufanisi na kwa matokeo chanya katika kila gereza nchini,” amesema.
Katika kuimarisha zaidi ujuzi wa wafungwa, Jeshi hilo kwa kushirikiana na VETA limeanzisha mfumo wa kutambua ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu ambapo wafungwa wanaokidhi vigezo hupatiwa vyeti vya ujuzi vinavyotambuliwa kitaifa.
“Machi 11, 2025, jumla ya wafungwa 201 walitunukiwa vyeti vya ujuzi mbalimbali katika hafla iliyofanyika Chuo cha KPF Morogoro, hatua inayolenga kuwasaidia kujiajiri na kuajirika baada ya kifungo.
“Vilevile, kwa kushirikiana na Chuo cha Uhasibu Arusha, wafungwa wamekuwa wakipatiwa mafunzo ya ujasiriamali na stadi za biashara. Tarehe 6 Agosti 2025, wafungwa 176 walihitimu mafunzo hayo na kupatiwa vyeti”amesema Katungu.
Mkuu huyo wa Jeshi la Magereza amesema programu hizo ni endelevu na zimekusudiwa kufikia idadi kubwa zaidi ya wafungwa nchini, ili kuhakikisha kundi hilo linakuwa na ujuzi utakaowasaidia kujenga maisha mapya baada ya kuachiwa.
“Mfano wa mafanikio ya mageuzi hayo umeonekana pia katika mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Msalato mkoani Dodoma, ambapo wataalam wa Jeshi la Magereza walikutana na aliyewahi kuwa mfungwa, Musa Feni Malale, ambaye sasa ameajiriwa kama fundi wa mifumo ya umeme na viyoyozi kutokana na ujuzi alioupata gerezani.
“Tunataka kuona zaidi ya watu waliowahi kuwa wafungwa wakigeuka kuwa wataalamu na wachangiaji katika miradi mikubwa ya kitaifa,” amesema.