Songwe. Tabasamu na matumaini vimeanza kuonekana kwa wakulima wa zao la ufuta katika Wilaya ya Momba, mkoani Songwe, kufuatia kufanyika kwa mafanikio mnada wa kwanza wa zao hilo kupitia mfumo wa soko la kidijitali.
Kwenye mnada huo wa kwanza katika Wilaya ya Momba ambao umefanyika leo Mei 9, 2026, jumla ya tani 928 za ufuta zimefikishwa sokoni na kuuzwa zote.
Bei iliyopatikana pia imepokewa vyema na wakulima, bei ya juu ikiwa Sh2,740 na ya chini Sh2,655 na hivyo kupata wastani wa Sh2714.90 kwa kilo moja.
Ofisa Mwandamizi wa Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), Justa Martini amesema zaidi ya kampuni 10 zimeshiriki katika mnada huo na kuonyesha ushindani mkubwa wa ununuzi wa zao hilo.
Ameeleza kuwa matokeo ya mnada huo yanaonyesha dalili njema kwa wakulima, hasa kutokana na kuimarika kwa bei ukilinganisha na minada iliyofanyika hapo awali.
“Tumepeleka sokoni tani 928 na zote zimenunulika. Tunashukuru kuona bei zimeimarika ukilinganisha na mnada uliopita. Tofauti ya bei mara nyingi inachangiwa na ubora wa zao uliopo ghalani pamoja na namna wakulima wanavyoandaa shehena zao kabla ya kuzipeleka sokoni,” alisema.
Ameongeza kuwa ubora wa mazao pamoja na wingi wa bidhaa sokoni vina mchango mkubwa katika kupata bei nzuri.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano ya Umma na Mawasiliano wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko, Theresia Christian amesema mnada huo umeonyesha namna ambavyo teknolojia ya kidijitali inaweza kuwaleta pamoja wakulima na wanunuzi kwa uwazi zaidi.
“Leo tumeweza kuona namna ambavyo wakulima pamoja na wanunuzi wameweza kukutana kidijitali na kushiriki mnada wa kwanza katika wilaya hii. Kupitia mnada huu tumeona wakulima wamekubali kuuza ufuta wao kwa wastani wa bei ya Sh2, 714.90 kwa kilo,” alisema.
Amefafanua kuwa baada ya mnada kumalizika, wamefanya kikao na viongozi wa vyama vya msingi vya wakulima ili kuwajengea uelewa zaidi kuhusu mfumo wa soko na mwenendo wa bei na kusikiliza changamoto zao.
“Baada ya mnada tumekaa na viongozi wa vyama vya msingi na kuwajengea uwezo kuhusu mwenendo wa bei, namna bei inavyopatikana sokoni na jinsi mfumo huu wa kidijitali unavyofanya kazi.
“Pia tumegusia masuala ya masoko na ubora wa mazao, na kwa kweli mwitikio umekuwa mkubwa na elimu imewafikia wakulima,” alieleza.
Kwa upande wa wakulima, mnada huo umeonekana kuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa katika biashara ya ufuta.
Jumapili Daud, mkulima wa zao hilo katika Wilaya ya Momba, amesema wameridhishwa na bei zilizopatikana kulingana na mwenendo wa hali ya soko ilivyo hivi sasa.
“Bei zipo vizuri ukilinganisha na minada mingine iliyopita. Zamani tulikuwa tunapishana sana na wenzetu wa maeneo mengine, lakini sasa tofauti imeanza kupungua. Tuna kila sababu ya kuwashukuru Copra kwa kusimamia ubora wa zao letu,” alisema.
Ameeleza kuwa mfumo wa mnada umeondoa changamoto iliyokuwa ikiwakumba wakulima kwa muda mrefu, hasa uwepo wa madalali waliokuwa wakinunua mazao kwa bei ya chini.
“Awali, kulikuwa na mtu kati. Mkulima alikuwa anaamini ni mtu sahihi lakini mara nyingi alikuwa anapunjwa. Mfumo huu wa mnada unampa mkulima nafasi ya kuuza moja kwa moja bila kudhulumiwa,” alifafanua.
Mkulima mwingine, Nesi Kalinga amesema zamani wakulima walilima ufuta kwa gharama kubwa, lakini walikosa soko la uhakika na hivyo kulazimika kuuza kwa walanguzi.
“Zamani tulipata shida sana. Tulikuwa tunalima kwa gharama kubwa, lakini wanunuzi waliokuja walikuwa walanguzi waliokuwa wanapima kwenye madebe makubwa na mara nyingi tulipata hasara,” alisema.
Hata hivyo, amesema ujio wa mfumo wa minada wa mauzo kidijitali kupitia ushirikiano wa Copra na TMX, umeleta mabadiliko makubwa kwa wakulima.
“Sasa tumepata faida. Ufuta wetu umeuzwa kwa bei nzuri na tunaona mafanikio yake. Mfumo huu umetusaidia sana,” alisema.
Kalinga pia amewahimiza wanawake kujitokeza zaidi katika shughuli za kilimo na kujiunga na vyama vya ushirika ili kunufaika na masoko ya pamoja.
“Nawashauri kina mama tujitahidi kujiunga na vyama vya ushirika na tusibaki majumbani tu lakini kwa sasa tunafahamu thamani ya zao,” alisema.
Kwa upande wake mkulima Shadrack Mgala amesema ameridhika na bei iliyopatikana katika mnada huo, ingawa aliomba maboresho zaidi katika muda wa malipo.
“Kwa bei ya leo nimeridhika nayo. Nimepiga hesabu zangu na kuona ipo sawa. Tunachoomba ni malipo yaingie kwa wakati,” alisema.
Amekumbusha kuwa katika baadhi ya misimu iliyopita wakulima walikumbwa na changamoto ya kucheleweshewa malipo baada ya kuuza.
Wakulima wengine pia wameeleza kuwa mfumo mpya umeondoa udanganyifu uliokuwa ukifanywa na baadhi ya walanguzi waliotumia vipimo visivyo sahihi.
“Zamani mtu anakuja nyumbani na ndoo kununua ufuta. Debe linakuwa na wastani wa kilo 15 lakini yeye anapima hadi kilo 16, hivyo anakwibia kilo moja. Lakini sasa tunapima kwenye mizani na tunaona wazi uzito wa mazao yetu,” alisema mkulima huyo.
Hivyo, wakulima wa Momba wanaamini kuwa mfumo wa mauzo kidijitali umeanza kuleta haki na uwazi katika biashara ya ufuta, hali inayotarajiwa kuongeza ari ya uzalishaji na kuboresha maisha yao kupitia kilimo.