Morogoro. Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, Danstan Kyobya amewataka viongozi wa vyama vya msingi katika bonde la mto Kilombero, kuhakikisha mizani mpya za kidijitali zinatumika kwa usahihi ili kuepuka udanganyifu.

Kyobya ametoa wito huo leo Jumapili, Mei 10, wakati akizindua ugawaji wa mizani 50 mpya za kidijitalikwa Chama Kikuu cha Ushirika cha Ulanga na Kilombero (UKICU), zilizotolewa na Kampuni ya Rotai Company LTD.

Mkuu huyo wa wilaya amesema mizani hizo zitaondoa changamoto zinazowakumba wakulima wauzapo mazao yao na kuondoa udanganyifu unaotokea katika kipimo cha mazao.

“Kila kiongozi wa chama cha msingi katika bonde la Kilombero ahakikishe mizani hii inatunzwa na kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa, ili iwanufaishe wakulima kwa muda mrefu. Hakikisha hakuna anayejaribu kufanya udanganyifu kwa sababu mfumo utabaini tu,” amesema Kyobya.

Viongozi wa vyama vya msingi na vyama vikuu vya ushirika wilaya ya Ulanga na Kilombero wakipiga makofi kufurahia uzinduzi wa kazi ya ugawaji wa mizani 50 ya kidigital itakayotumiwa na vyama hivyo. Picha Hamida Shariff

Aidha, amesisitiza usimamizi wa ubora wa mazao, ikiwamo ukaguzi wa mara kwa mara kuhakikisha hakuna udanganyifu unaofanywa kama kuongeza uzito kwa kuweka mawe au mchanga.

Kwa upande wake, Gidion David, Mkurugenzi wa Fedha wa Rotai Company Limited amesema matumizi ya mizani ya kidijitali yataongeza usahihi wa taarifa za mazao, kusaidia wakulima kupata risiti sahihi na kuondoa malalamiko ya kupunjwa kwa mazao.

“Mfumo huu unahitaji uadilifu na uaminifu kwa watendaji wote ili kuhakikisha wakulima wanapata haki zao stahiki. Mizani hii ikiwa itachezewa au kudanganywa, haiwezi kufanya kazi hadi mtaalamu atakapokuja kuangalia,” amesema David.

David amebainisha kuwa mizani 50 zilizotolewa ni za kisasa, zikiwa na usalama wa kipekee, ambapo mtu yeyote atakayejaribu kuichezea ataizuia kufanya kazi.

Kwa upande wake, Mrajisi Msaidizi wa Mkoa wa Morogoro, Secilia Sosteness amesema mizani hiyo italeta ufanisi mkubwa katika upatikanaji wa takwimu sahihi za mazao yanayozalishwa na wakulima, tofauti na hali ya awali ambapo udanganyifu ulisababisha ukosefu wa takwimu sahihi.

Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Dunstan Kyobya (aliyeshika mzani) akiwa na viongozi wa vyama vya ushirika vya msingi na vyama vikuu vya ushirika wilaya ya Ulanga na Kilombero (UKICU) wakati wa uzinduzi wa ugawaji mizani 50 ya kidigital itakayotumiwa na vyama hivyo. Picha Hamida Shariff

“Mafanikio tunayoyapata kupitia mizani hii ni kwamba sasa tuna takwimu sahihi za mazao ya wakulima, mauzo yake na uhakika wa masoko tofauti na ilivyokuwa zamani,” amesema Sosteness.

Aidha, Dk Rozaria Rwegasira, Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Morogoro anayeshughulikia uchumi na uzalishaji mali, ametoa wito kwa viongozi wa vyama vya ushirika na maafisa ugani kuendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi sahihi ya mizani hiyo.

Naye Mwenyekiti wa UKICU, Hawa Lubiki, ameomba mafunzo zaidi kwa watumiaji wa mizani ili kuhakikisha mfumo unatumika kwa usahihi na kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa wakulima na vyama vya ushirika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *