
Mbeya. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa, kimeeleza kusikitishwa na kusuasua kwa ujenzi wa miradi miwili ya kimkakati, huku kikitoa msimamo wake kuhusu mchakato wa maridhiano ya kitaifa.
Akizungumza leo Jumapili, Mei 10, 2026, katika mkutano wa hadhara, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’, amesema maisha ya wananchi yamezidi kushuka kutokana na kukosekana kwa viongozi wasiojali maslahi ya wananchi.
Kuhusu bei ya mafuta, Sugu ameikosoa serikali akidai kuwa imeshindwa kuonyesha huruma kwa wananchi wake.
Amesema mafuta yakiagizwa huchukua siku 60 hadi yaingie nchini, lakini ndani ya muda huo bei imepanda kwa kasi isiyokubalika.
“Nchi imegoma kwenda, kwa kuwa hakuna fedha. Mfano hapa Mbeya, maji ni shida. Nilishauri suluhisho la maji ni mto Kiwira, lakini miruzi inapigwa, tunanuka kwa wananchi,“ amesema Sugu.
Aidha, akizungumzia ujenzi wa barabara ya njia nne, kiongozi huyo amesema hauna ufanisi na kwamba, barabara ya awali ingeweza kuwa bora kuliko hiyo inayojengwa sasa akidai haina mpangilio.
Maridhiano
Akizungumzia haoja ya maridhiano ya Kitaifa kwenye mkutano huo wa hadhara uliohudhuria na watu wengi jijini Mbeya, Sugu amesema Chadema haitashiriki iwapo mwenyekiti wao, Tundu Lisu, hatashiriki moja kwa moja kutokana na kushikiliwa kwake gerezani.
Amesema mbali ya Lissu, Chadena kinahitaji mpatanishi anayekubalika na pande zote ambaye ataoka SADC au Umoja wa Afrika (AU).
“Wamemshikilia kiongozi wetu wa Taifa Lisu, wanaogopa kumtoa. Lakini wanajua kubaki kwake ndani ni moto na kutoka pia ni moto. Hakuna mazungumzo bila mwenyekiti wetu na ikitokea, tunataka awepo mpatanishi anayekubalika na pande zote,” amesema Sugu.
Amesisitiza hakuna haja ya kutumia mabilioni kuandaa katiba mpya, bali rasimu ya Jaji Warioba inaweza kutumika, huku akitaka uwajibikaji kwa waliohusika katika matukio ya Oktoba 29, na watu waliotekwa au kufungwa wachiwe huru bila masharti.
Pia, amekosoa ripoti ya Tume ya Rais ya kuchunguza matukio ya uchaguzi mkuu, akieleza kuwa ripoti hiyo haikuwa sahihi akidai wajumbe wote walikuwa watumishi wa serikali.
“Chadema haitasita kusema ukweli. Umma hauiamini tena serikali, kwani walioteuliwa kwa majukumu ya kitaifa hawana imani ya wananchi. Wazee wanaopaswa kupewa jukumu la kitaifa wanapaswa kuwa watu wanaoaminika, kama mzee Warioba,” amesema Sugu.
Kuhusu matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Sugu amesema yamesababisha nchi kukwama na gharama za maisha zimepandishwa na Serikali ya CCM aliyodai imeshindwa kuwatumikia wananchi ipasavyo.
“Uchaguzi wa 2025 haukufanyika kikamilifu, kwa kuwa hadi saa 5 asubuhi watu walikuwa wameondoka vituoni. Njia bora nikurudia uchaguzi huo na si kujitangaza kwamba wao wamepata ushindi,” amesema.
Amesema vijana wa kizazi kipya, hawamjui Rais wa kwanza, Hayati Mwalimu Nyerere, wala utawala wa Ukoloni, bali wanaiona CCM kama mkoloni anayewanyima ajira.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Tabia Mwakikuti, Mwenyekiti wa Bawacha Kanda ya Nyasa ameitaka serikali kumuachia huru Lissu, akisema kufanya hivyo ni kwa maslahi ya wananchi.
“Neno letu wanawake liwe moja: kumuombea Lissu aachiwe huru, kiongozi wetu si mwizi wala mhaini,“ amesema Tabia.
Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Kalori Masaga kwa upande wake amesemahali ya maisha kwa wananchi ni mbaya, huku akisisitiza kuwa hakuna uchaguzi halali uliofanyika Oktoba 29, mwaka jana.
“Tunayo maumivu lakini bado tunapewa kauli mbaya, tusikubali. Tusemelee kwa Mungu atutendee haki, tupate katiba mpya na kampeni ya ‘Free Lisu‘,” amesema Masaga.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chama hicho Mkoa wa Mbeya (Bavicha), Elisha Chonya amesema kwa sasa hakuna serikali inayoweza kuiwajibisha serikaki hiyo hiyo kutokana na uteuzi wa mtu mmoja.
“Bunge ni serikali, muhimili wa mahakama unaopaswa kutenda haki nao ni serikali, wote wanateuliwa na Rais, hivyo uzembe wote hakuna wa kuwajibika, sasa chama chenu (Chadema) tumerudi.”
“Tutazunguka mtaa kwa mtaa, kata kwa kata na nyumba kwa nyumba kuwasemea wananchi, hakuna atakayepitwa, tumejipanga vyema” amesema Chonya.
Awali, Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa wacha wa Chama hicho Mbeya Vijijini, (Bawacha), Getruda Legesela amesema kwa sasa usalama wa wananchi na Taifa kwa ujumla ni mdogo, hakuna mwenye uwezo wa kuzuia hilo.