
Harakati ya Mpambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas imelaani ongezeko la uhalifu na ukiukwaji wa haki za wafungwa wanawake wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika magereza ya Israel, ikisema kwamba mateso ya kimwili na kisaikolojia ni uhalifu wa kivita.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi, Hamas ilisema kuendelea kuzuiliwa wafungwa 87 wa kike wa Kipalestina—wakiwemo wanawake wajawazito, wafungwa wagonjwa, na watoto—katika hali ngumu bila huduma bora za afya na chakula cha kutosha kunaonyesha “sura ya ufashisti” ya utawala wa Israel na utumiaji wa magereza kama chombo cha ukandamizaji, kulipiza kisasi, na kuvunja azma ya mapambano ya watu wa Palestina.
Harakati hiyo imesema kwamba kuwafungulia mashtaka na utekaji nyara wa wanawake wa Palestina kutokana na maoni au machapisho yao katika mitandao ya kijamii ni kielelezo cha kuongezeka ugaidi unaofadhiliwa na serikali unaofanywa na baraza la mawaziri la mhalifu wa kivita, Benjamin Netanyahu, dhidi ya watu wa Palestina.
Hamas imetoa wito kwa Umoja wa Mataifa, mashirika ya kimataifa ya kutetea haki za binadamu, na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu kuchukua hatua za haraka za kushinikiza kuachiliwa mara moja wafungwa wote wa kike wanaoshikiliwa katika magereza ya Israel.
Harakati hiyo pia imeuhimiza Umoja wa Mataifa kuwawajibisha viongozi wa Israel kwa uhalifu wao dhidi ya watu wa Palestina na wafungwa wanawake.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Wafungwa wa Kipalestina kuripoti hapo awali kwamba wafungwa wanawake wa Kipalestina katika Gereza la Damon walikuwa wamefanyiwa ukandamizaji na mashinikizo makubwa na askari wa Israel.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, zaidi ya operesheni 10 za ukandamizaji zimefanywa katika Gereza la Damon katika mwezi uliopita, ikiwa ni pamoja na uvamizi wa kikatili, vipigo, kufungwa kwenye seli ya mtu mmoja, na kadhalika.
Ofisi ya Vyombo vya Habari ya Wafungwa wa Kipalestina imeitaja hali ya ndani ya magereza hiizo kuwa “mbaya,” ikitaja msongamano mkubwa wa watu, wafungwa kulala sakafuni, uhaba wa vifaa vya usafi na nguo, pamoja na chakula kisichofaa wanachopewa wafungwa hao.