
Mchezaji chipukizi wa tenisi kutoka Iran, Hana Shabanpour, amejiondoa katika fainali ya mashindano ya J60 Turkey World Tour siku ya Jumapili baada ya kukataa kucheza dhidi ya mpinzani aliyekuwa akiwakilisha utawala wa Israel, kama ishara ya kupinga mauaji na mateso dhidi ya Wapalestina.
Shabanpour, ambaye ni mwakilishi wa timu ya taifa ya Iran, aliondoka kwenye fainali ya mchezo wa wawili wawili mara tu ilipothibitishwa kuwa timu pinzani ilikuwa na wachezaji kutoka Russia na Israel.
Akiwa pamoja na mwenza wake kutoka Uturuki, alikuwa amefuzu kwa kishindo hadi hatua ya fainali baada ya kuonyesha kiwango cha juu katika michuano hiyo.
Mbali na mafanikio hayo, nyota huyo wa Iran pia alifika robo fainali ya mchezo wa mmoja mmoja, ambapo alipoteza kwa ushindani mkubwa dhidi ya mchezaji aliyekuwa amepewa nafasi ya kwanza kwenye mashindano hayo.
Akieleza sababu za uamuzi wake, Shabanpour amesema hatua hiyo imechochewa na mauaji ya watoto na wanawake wa Kipalestina yanayofanywa askari wa jeshi katili la Israel.
Kujiondoa kwake ni katika mlolongo hatua ya wanamichezo kutoka nchi za Kiislamu kususia kushindana dhidi ya wawakilishi wa utawala haramu wa Israel katika mashindano ya kimataifa.