Dar es Salaam. Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Tukay Thomas, ameibuka mshindi wa shindano la andiko la ubunifu la kutafuta suluhu ya msongamano wa magari mijini, na kuzawadiwa Sh10 milioni.

Shindano hilo lilitangazwa Februari mwaka huu na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, alipowataka wanafunzi kuandika bunifu zao ili kupata suluhu ya changamoto hiyo.

Hadi Ulega anakuja na shindano hilo, msongamano wa magari nchini ulitajwa kuigharimu nchi takribani Sh4 bilioni kwa siku, sawa na Sh1.44 trilioni kwa mwaka, kama ilivyowahi kuelezwa na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka 2021.

Matokeo ya shindano hilo yametangazwa leo, Jumapili, Mei 10, 2026, na Waziri Ulega wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi.

Ukiacha Thomas, nafasi ya pili ilichukuliwa na kikundi cha wanafunzi watano kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), waliopata zawadi ya Sh5 milioni, huku Godson Jackson kutoka Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) akishika nafasi ya tatu na kupata Sh3 milioni.

Aidha, mshindi wa nne alizawadiwa Sh2 milioni, huku washindi wa tano hadi saba wakipata Sh1 milioni kila mmoja. Washindi wa nafasi ya nane hadi 10 walizawadiwa Sh500,000 kila mmoja.

Zawadi nyingine zilizotolewa ni pamoja na kompyuta mpakato, vyeti na ngao. Aidha, washindi wa nafasi ya 11 hadi 21 nao walipatiwa kompyuta mpakato na vyeti vya ushiriki.

Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo, Ulega amesema Serikali imeamua kuwashirikisha vijana katika kutafuta suluhu za changamoto za usafiri mijini ili kuhamasisha matumizi ya maarifa ya darasani katika vitendo na kuongeza ushiriki wao katika maendeleo ya Taifa.

Amesema Tanzania ina wataalamu wa kutosha katika sekta ya miundombinu, jambo linalodhihirishwa na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, ikiwemo reli ya kisasa ya SGR, Bwawa la Umeme la Mwalimu Julius Nyerere na ujenzi wa barabara mbalimbali nchini.

“Tumewashirikisha vijana si kwa sababu hatuna wataalamu, bali tunaamini vijana wana nafasi kubwa katika ujenzi wa taifa lao. Tunahitaji mawazo yao, ubunifu wao na nguvu zao kuwa sehemu ya maendeleo ya Tanzania,” amesema.

Waziri huyo amewataka vijana kuendelea kuipenda, kuiamini na kuilinda Tanzania, huku akiwahimiza kupuuza wanaobeza mafanikio ya Serikali.

Amesisitiza kuwa Taifa linahitaji kizazi chenye uzalendo, maono na uthubutu wa kushiriki kikamilifu katika kuleta maendeleo endelevu.

Pia amewahamasisha vijana walioshiriki mashindano hayo kufungua kampuni zao na kuahidi kuwa wizara itawasaidia katika mchakato wa usajili kupitia taasisi zake ili waweze kutumia taaluma zao kujijengea uchumi na kuchangia maendeleo ya Taifa.

Awali, Mwenyekiti wa Jopo la Majaji, Dk Daniel Matondo, amesema jumla ya maandiko bunifu 561 yalipokelewa, ambapo 328 yalikuwa ya wanafunzi na 233 hayakuwa na utambulisho.

Maandishi hayo yalitoka katika vyuo 38 vya ndani na vyuo vinne vya nje ya nchi.

Amesema kati ya maandiko hayo, 176 yalitimiza vigezo na kuingia katika hatua ya uchambuzi wa kina.

Kwa mujibu wa Dk Matondo, suluhisho zilizowasilishwa zilioyesha kuwa changamoto ya msongamano wa magari inaweza kutatuliwa kwa mbinu mbalimbali badala ya kutegemea njia moja pekee.

Amesema mapendekezo 19 yaliyoibuka yaligusa maeneo muhimu ya usafiri na mipango miji, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya barabara, usafiri wa umma na matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa trafiki.

Mapendekezo hayo pia yalijumuisha ukamilishaji wa mtandao wa mabasi yaendayo haraka (BRT), ujenzi wa flyover, utenganishaji wa barabara katika maeneo yenye msongamano mkubwa pamoja na upanuzi wa miundombinu ya usafiri usiotumia magari.

Mapendekezo mengine ni pamoja na kuhamisha baadhi ya huduma nje ya maeneo ya biashara kuu, ujenzi wa barabara za haraka, kuongeza njia katika maeneo yenye msongamano mkubwa, kudhibiti magari makubwa mijini na kuboresha usafirishaji wa mizigo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *