MWANZA: MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amepongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza Kwa kuimarisha ulinzi na usalama.
Mtanda alisema hayo Mei 9 katika maadhimisho ya Siku ya Familia ya Jeshi la Polisi yaliyofanyika katika uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.
Mtanda amesema Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea kuhakikisha amani, utulivu na usalama unaimarika.

Amesema kuwa kazi inayofanywa na askari wa jeshi hilo imekuwa chachu ya maendeleo kutokana na wananchi kuendelea kufanya shughuli zao za kiuchumi katika mazingira salama na yenye utulivu.
Amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa Jeshi la Polisi katika kulinda raia na mali zao, huku akiwasisitiza askari kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo mkubwa kwa taifa.
“Jeshi la Polisi limeendelea kufanya kazi nzuri ya kuimarisha ulinzi na usalama. Serikali inatambua na kuthamini juhudi zinazofanywa na askari wetu katika kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na usalama wakati wote,” amesema Mtanda.
Amesema serikali ya awamu ya sita imeendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa askari polisi nchini kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo vya polisi, nyumba za askari pamoja na kuongeza vitendea kazi vya kisasa.