Unguja. Zaidi ya viwanja 300 vilivyotolewa na Serikali kwa wananchi wa Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja, vinatarajiwa kurejeshwa serikalini ili kutafutiwa matumizi mengine baada ya wahusika kushindwa kuviendeleza kwa muda mrefu.
Kwa mujibu wa Kanuni za Sheria ya Matumizi ya Ardhi Na. 12 ya mwaka 1992, mwananchi anayepewa eneo anatakiwa kuliendeleza ndani ya kipindi cha miaka miwili; vinginevyo Serikali ina mamlaka ya kulichukua.
Akizungumza leo, Jumapili, Mei 10, 2026, baada ya kutembelea maeneo hayo katika shehia za Tasani, Mzuri na Kiongoni Makunduchi, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Ardhi, Mussa Kombo Bakari, amesema wananchi hao walipewa viwanja hivyo kati ya mwaka 2011 na 2013, lakini hadi sasa wengi wao hawajaviendeleza.
Katibu Mtendaji Kamisheni ya Ardhi Zanzibar, Mussa Kombo Bakari akionesha mchoro wa viwanja vilivyotolewa na serikali kwa wananchi wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja wakashindwa kuviendeleza. Picha na Jesse Mikofu
“Azimio la Serikali lilikuwa kuhakikisha maeneo hayo yanajengwa makazi bora, lakini tunavyoona kwa sasa karibu maeneo yote yamegeuka vichaka, jambo ambalo halikuwa lengo la Serikali,” amesema Kombo.
Amefafanua kuwa kwa mujibu wa sheria, maendeleo ya kiwanja yanamaanisha ujenzi wa nyumba na si kujenga ukuta au uzio pekee.
“Kujenga fensi au ukuta ni hatua ya ulinzi wa eneo, lakini hiyo haihesabiki kama maendeleo ya kiwanja. Kwa mujibu wa sheria, wananchi hawa wanapaswa kunyang’anywa maeneo hayo ili Serikali iyatafutie matumizi mengine,” amesema.
Katibu huyo ametumia nafasi hiyo kuwataka wananchi wanaopewa viwanja au wanaovinunua binafsi kuhakikisha wanaviendeleza badala ya kuviacha bila matumizi.
“Hatuna nia ya kuwanyang’anya wananchi maeneo yao, lakini wanaposhindwa kuyaendeleza ni lazima kutafutwe utaratibu mwingine ili miji iwe katika mazingira mazuri na changamoto ya makazi ipungue,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali inaweza kulazimika kuchukua hatua hiyo kutokana na ongezeko la mahitaji ya maeneo ya makazi na uwekezaji kutoka kwa wananchi wengine.
Kwa mujibu wake, Serikali inaendelea kuweka mipango ya kuendeleza makazi bora na miji iliyopangwa vizuri, hivyo kuyaacha maeneo hayo katika hali ya sasa hakuakisi taswira nzuri ya maendeleo.
“Wakati Serikali ilipotoa maeneo haya, haikutarajia kwamba baada ya miaka yote hiyo yangekuwa vichaka. Maeneo haya yalipaswa kuwa tayari yameendelezwa na kuwa sehemu ya makazi na mji uliopangika vizuri,” amesema.
Amesema Kamisheni ya Ardhi itaishauri Serikali kuhusu hatua bora za kuchukua ili maeneo hayo yatumike kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.
“Maeneo yenye mandhari nzuri kama haya yangeendelezwa yangeweza kusaidia jamii na hata watu binafsi kiuchumi, lakini kwa sasa hayana manufaa kwa wananchi wala kwa nchi,” amesema.
Aidha, ameonya kuwa kuendelea kuyaacha maeneo hayo bila maendeleo kunaweza kusababisha uvamizi na ujenzi holela unaokwenda kinyume na mipango ya matumizi bora ya ardhi.
Sehemu ya viwanja vilivyotolewa na serikali kwa wananchi katika shehia ya Tasani Wilaya ya Kusini Mkoa wa Kusini Unguja tangu mwaka 2011 lakini wakashindwa kuviendeleza. Picha na Jesse Mikofu
“Wapo wananchi wenye uhitaji wa maeneo ya makazi, huduma za kijamii na miradi ya uwekezaji. Tukiendelea kuyaacha hivi, kuna hatari ya uvamizi na ujenzi usiofuata utaratibu ambao unaweza kuharibu taswira ya nchi,” amesema.
Kwa upande wao, viongozi wa shehia husika wamesema iwapo maeneo hayo yataendelezwa, yanaweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.
Katibu wa Shehia ya Mzuri, Mohamed Issa Change, amesema eneo hilo lilikuwa wazi kwa muda mrefu na hata mwekezaji mmoja aliwahi kuonesha nia ya kulitekeleza, lakini juhudi hizo zilikwama baada ya kubainika kuwa tayari kulikuwa na michoro ya viwanja.
“Kwa kweli haya ni maeneo makubwa yaliyoachwa wazi huku wamiliki wake wakiwa hawana utayari wa kuyaendeleza. Ni vyema Serikali ikaangalia utaratibu mwingine utakaosaidia maendeleo ya maeneo hayo,” amesema.
Naye Katibu wa Shehia ya Tasani, Mbwana Khamis, amesema maeneo hayo yanaweza kusaidia kukuza uchumi wa wilaya na mkoa iwapo yatatafutiwa matumizi bora na kuendelezwa ipasavyo.