Kigoma. Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema hajaridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Megawati 49.5 katika maporomoko ya Mto Malagarasi mkoani Kigoma.

Mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Dongfang Electric, unadaiwa kucheleweshwa sambamba na kutotekeleza masharti ya mkataba waliouingia na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Waziri Ndejembi ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Mei 10, 2026 alipokagua maendeleo ya mradi huo akibainisha kuwa, mkandarasi huyo amekuwa akitoa visingizio badala ya kutekeleza majukumu yake kwa wakati kama mkataba unavyoelekeza.

Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri huyo amesema Serikali tayari imemlipa mkandarasi zaidi ya Dola 20 milioni (Sh54 bilioni), kama malipo ya awali, lakini kiwango cha kazi zilizotekelezwa hakiendani na fedha fedha iliyotolewa.

Baadhi ya kazi zilizochelewa ni pamoja na ujenzi wa makazi ya wafanyakazi na barabara za mradi, hali ambayo imeonesha kusuasua kwa utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi wakati akizungumza na vyombo vya habari juu ya utekelezaji wa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Megawati 49.5 katika maporomoko ya Mto Malagarasi mkoani Kigoma.

Aidha, ameielekeza Tanesco pamoja na mshauri mwelekezi kuendelea kumsimamia kwa karibu mkandarasi huyo, huku akisisitiza kuwa Serikali haitatoa nyongeza ya fedha wala kuruhusu mabadiliko ya gharama za mradi huo kwa sababu aliwasilisha gharama zake mwenyewe wakati wa zabuni.

Waziri Ndejembi amesema baadhi ya makandarasi wana tabia ya kuomba kazi kwa gharama ndogo ili kupata zabuni na baadaye kuanza kuomba nyongeza ya fedha, jambo ambalo Serikali haitalivumilia.

Katika hatua nyingine, waziri huyo amemuagiza meneja wa mradi upande wa mkandarasi kuondolewa mara moja kutokana na kile alichokieleza kuwa ni visingizio vinavyochangia kuchelewesha utekelezaji wa kazi.

Pia, ameagiza kufanyika kwa ukaguzi maalumu wa matumizi ya fedha za malipo ya awali ili kubaini namna zilivyotumika ukilinganisha na kazi zilizofanyika.

“Mradi huu una umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Kigoma, Katavi, Kagera na maeneo ya jirani kwani utaongeza nguvu katika Gridi ya Taifa na kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini. Serikali haitakuwa tayari kuvumilia ucheleweshaji unaosababishwa na uzembe wa wakandarasi,” amesema Ndejembi.

Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi wakati akizungumza na vyombo vya habari juu ya utekelezaji wa Mradi wa Kuzalisha Umeme wa Megawati 49.5 katika maporomoko ya Mto Malagarasi mkoani Kigoma.

Ameielekeza ikamilishe ukaguzi ndani ya wiki mbili na iwasilishe taarifa ofisini kwake.

Aidha, amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, Lazaro Twange kwa kufanya vikao vya mara kwa mara na mkandarasi huyo pamoja na kuchukua hatua mbalimbali za kutatua changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa mradi.

Mkurugenzi Twange amesema Tanesco imepokea maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri na itahakikisha yanatekelezwa kwa wakati ili mradi huo ukamilike kama ilivyopangwa.

Mradi wa Malagarasi MW 49.5 unatekelezwa na Kampuni ya Dangfang Electric International Corporation (DEC) kutoka China, ulianza kutekelezwa Aprili 30, 2024 na unatarajiwa kukamilika Oktoba 30, 2027 kwa gharama ya zaidi ya Sh300 bilioni.

Kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Kigoma, Katavi, Kagera na maeneo ya jirani kwa sababu utaongeza nguvu katika Gridi ya Taifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *