Dar es Salaam. Kupanda kwa nauli za mabasi ya abiria mijini na bodaboda, kumefungua milango ya neema kwa wadau wa usafirishaji kupitia baiskeli hasa katika mikoa ambayo usafiri huo unatumika kubeba abiria, ikiwamo Mwanza na Shinyanga.

Kwa mujibu wa wadau hao, abiria sasa wanazikimbia bodaboda na mabasi kutokana na nauli kubwa zinazotozwa, badala yake wamegeukia baiskeli kwa kuwa nauli zake zimebaki kuwa kati ya Sh200 hadi Sh500.

Hatua ya kuongezeka kwa nauli za mabasi na bodaboda ilianza Mei 1, mwaka huu baada ya tangazo la Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra), siku 14 kabla ya tarehe hiyo.

Uamuzi huo wa Latra, ulisababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta kulitokana na kuadimika kwa nishati hiyo, baada ya vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati, ikihusisha Marekani, Israel na Iran.

Akizungumza na Mwananchi Mwenyekiti wa waendesha baiskeli wilayani Misungwi mkoani Mwanza, Robert Joseph, amesema kwa sasa kumekuwa na ongezeko la wateja baada ya kuzikimbia bodaboda.

Baiskeli zinazotumika kubeba abiria maarufu kwa jina la daladala katika mkoa wa Simiyu. Picha na Samwel Mwanga

“Wateja wameongezeka sana siku hizi…zamani tulikuwa tunatoza Sh300 hadi Sh500 kwa mzunguko ambayo tunatoza hadi sasa, lakini sasa kipato kimeongezeka  kutokana na wateja wengi,” amesema.

John Masanja, anayefanya shughuli ya kupakia abiria kwa baiskeli wilayani humo, amesema ongezeko la bei ya mafuta limekuwa neema kwao, kwani limewafanya wananchi wengi kushindwa kumudu gharama za bodaboda.

“Tunamshukuru Mungu, kwa sasa tunapata wateja wengi zaidi. Bei ya bodaboda imepanda kutoka Sh1,000 hadi Sh2,000, hivyo watu wengi wanakuja kwetu,” amesema.

Kwa upande wake, mmiliki wa baiskeli za kukodisha mjini Misungwi, Jonson John amesema mahitaji ya baiskeli yameongezeka tofauti na ilivyokuwa awali.

“Nina baiskeli 56 na kwa sasa 47 tayari zimekodiwa, zimebaki chache sana… zamani mchana kama huu baiskeli nyingi zilikuwa hazijakodiwa, lakini sasa wateja ni wengi,” amesema.

Ameongeza kuwa wateja wengi ni wakulima wanaokwenda mashambani, hasa kufuatilia shughuli za kilimo cha nyanya, huku wengine wachache wakizitumia kusafirisha mahitaji kutoka sokoni kwenda majumbani.

Abiria wa baiskeli, Kwandu Noel, amesema amelazimika kupanda usafiri huo kwenda mnadani kwa kuwa nauli ya bodaboda imeongezeka kutoka Sh1,500 hadi Sh3,000 fedha ambayo hawezi kumudu.

“Mimi nilikuwa na bajeti ya nauli ya Sh3,000 kwenda na kurudi…nimefika hapa naambiwa kwenda tu Sh3,000 nimeshindwa ikabidi nipande daladala (baiskeli) ambayo ni Sh500, kwa hiyo kwenda na kurudi natumia ,

Hata hivyo, kupanda huko kwa nauli za baiskeli hakujafikia zile zinazotozwa katika bodaboda. Waendesha baiskeli wanasema walikokuwa wanatoza Sh500 kwa sasa ni Sh1,000 hadi Sh1,500.

“Nauli tumepandisha Nyahanga senta kwa Mathayo ni 1,500 japo ilikuwa ni 500 na saivi hawaji sana sokoni tunaagizwa tunapeleka nyumbani kwa mteja,” amesema.

Ameeleza wateja wanawaagiza mizigo wawapelekee nyumbani kuepusha gharama.

Geita nako, mambo ni yaleyale. Nauli hazikuishia kupanda kwa bodaboda na Bajaji pekee, bali hata usafiri wa baiskeli. Hata hivyo, bado nauli ya baiskeli imebaki kuwa chini na kufanya usafiri huo uwe kimbilio la abiria.

Elias Kanani ni mwendesha baskeli Manispaa ya Geita, amesema kupanda kwa gharama za maisha kumesababisha nao wapandishe nauli, ingawa usafiri wao hautumii mafuta.

“Baada ya kuwa mafuta yamepanda wenzetu wamepandisha bei ila sisi sehemu ya Sh300 kwa sasa tunatoza Sh500, sehemu ya Sh700 tunawambia Sh1,000, sehemu ya Sh1,000 ni Sh1,500,” amesema.

Amekiri unafuu wa maisha akilinganisha na awali baada ya abiria kuongezeka.

Aidha, gharama ya kukopesha baiskeli kwa mikataba imeendelea kuwa kama ilivyokuwa awali, waendeshaji hupewa baiskeli mpya kwa mkataba wa miezi minne huku wakitoa rejesho la Sh3,500 kwa siku.

Baiskeli zinazotumika kubeba abiria maarufu kwa jina la daladala katika mkoa wa Simiyu. Picha na Samwel Mwanga

Furaha Mayombo ni mwendesha baiskeli katika Kituo cha Mabasi cha Manispaa ya Geita, amesema kupanda kwa gharama za maisha kumewasukuma nao kuongeza nauli kuendana na hali ya kiuchumi.

“Maisha yamepanda kama ulikuwa unanunua mkaa kwa Sh500 unanunua Sh1,000, kama mboga ulikuwa unanunua Sh300 sasa hivi ni Sh500,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *