Unguja. Kamati ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa imeitaka Serikali kuwashirikisha wananchi katika hatua zote za kuanzishwa, kutekeleza na kuendeleza miradi ya maendeleo husika katika maeneo yao.

Akisoma maoni ya kamati hiyo katika Baraza la Wawakilishi wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara maalumu za SMZ, mjumbe wa kamati hiyo, Mahofudh Abdalla Mohamed amesema ushirikishwaji huo utaongeza uwajibikaji katika matumizi ya rasilimali za umma.

“Hatua hii itasaida pia miradi inayotekelezwa iendane na mahitaji halisi ya wananchi na kuleta tija kwa jamii na Serikali kwa jumla. Hatua hii itajenga hali ya wananchi kuiona miradi hiyo kama ni mali yao,” amesema.

Pia, kamati imeeleza namna ambavyo baadhi ya mabaraza yanashindwa kukusanya mapato yake ikiwamo kwa kutotumika kwa rasilimali zilizopo ipasavyo na kushindwa kuanzisha vyanzo vipya vya mapato.

Ametolewa mfano wa Baraza la Mji Wete ambalo limeshindwa kutumia soko la wajasirimali la Kifumbakai.

“Kutokana na hali hiyo kamati inazitaka taasisi za Serikali kuhakikisha zinalipa kwa wakati mgao unaostahiki kwa halmashauri ili kuongeza mapato.

Amesema kamati imebaini kuwepo kwa baadhi ya mabaraza kukusanya kiwango kisichoridhisha hivyo kuzitaka zibaini vyanzo vipya na kuongeza mapato.

Awali, akiwasilisha makadirio ya bajeti hiyo, Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ, Idrissa Kitwana Mustafa ameliomba baraza lihidhinishe Sh695.735 bilioni.

Kati ya fedha hizo, Sh217.830 bilioni kwa ajili ya mishahara, Sh50.190 bilioni kwa matumizi mengineyo, Sh20.518 bilioni ruzuku kwa Tume ya Utumishi ya Idara Maalumu za SMZ.

Wakala wa Ulinzi wa JKU na Mamlaka za Serikali za Mitaa Sh405.196 bilioni kwa matumizi ya kazi za maendeleo.

Katika bajeti hiyo, Serikali za mitaa zimejielekeza katika ujenzi wa masoko na vituo vya daladala katika maeeno mbalimbali.

Mamlaka za Serikali za mitaa zitaendelea kutekeleza majukumu yake ya kimsingi kwa kuweka mifumo imara ya ukusanyaji wa mapato na kuweka mifumo bora ya ukusanyaji wa taka kutoka majumbani na maeneo ya biashara.

Pia, itaanzisha mashindano ya usafi kwa kila shehia kufanya usafi wa mitaro ya maji ya mvua na maeneo ya wazi, kufanya matengenezo ya miundombinu ikiwamo taa za barabarani, taa za kuongozea magari na alama za barabarani.

“Kufanikisha utekelezaji na shughuli mtambuka kama vile uhifadhi wa mazingira, kampeni za kujikinga na maambukizi ya VVU na hifadhi ya mtoto na kutoa misaada kwa wananchi wanaopatwa na maafa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *