Ripoti hiyo iliyotolewa leo tarehe 11 Mei 2026 jijini New York inasema ongezeko kubwa la mahitaji ya madini yanayotumika katika magari ya umeme, mifumo ya nishati jadidifu na miundombinu ya kidijitali tayari linaongeza shinikizo kwa vyanzo vya maji katika maeneo maskini na yenye ukame duniani.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo yenye jina “Madini muhimu , kutokuwa na uhakika wa maji na haki”, uzalishaji wa lithiamu duniani mwaka 2024 ulitumia takribani lita bilioni 456 za maji kiwango kinacholingana na mahitaji ya maji ya matumizi ya nyumbani kwa watu milioni 62 katika kanda ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa mwaka mmoja.

Watafiti wameonya kuwa gharama za kimazingira za mpito kuelekea nishati safi zinazidi kubebwa na jamii zenye uwezo mdogo wa kupata maji safi na zilizo na ulinzi dhaifu dhidi ya uchafuzi wa viwanda.

Upanuzi wa uchimbaji madini waongeza shinikizo la maji

Ripoti hiyo imebaini kuwa karibu asilimia 16 ya uchimbaji wa madini muhimu unafanyika katika maeneo ambayo tayari yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji. Jamii zinazoishi karibu na migodi zinashuhudia kushuka kwa kina cha maji ardhini, uchafuzi wa vyanzo vya maji ya kunywa na kuongezeka kwa shinikizo kwa shughuli za kilimo na ufugaji zinazotegemea maji.

“Mbio za kufikia hatua ya kutozalisha kabisa hewa ukaa haziwezi kukanyaga maskini,” ameonya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres wakati wa uzinduzi wa mapendekezo ya Jopo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Madini Muhimu ya Mpito wa Nishati mwaka 2024.

Ameongeza kusema, “Dunia inayotumia nishati jadidifu ni dunia yenye njaa ya madini muhimu.”

Matokeo hayo mapya yanaongeza hofu ndani ya Umoja wa Mataifa kuwa bila hatua madhubuti za ulinzi, mpito kutoka mafuta ya kisukuku unaweza kurudia mifumo ileile ya uharibifu wa mazingira na ukosefu wa usawa ulioshuhudiwa katika sekta za zamani za uchimbaji madini.

Mabilioni ya watu bado hawana maji salama

Onyo hilo linakuja wakati ambapo hal ya kutokuwa na uhakika wa maji duniani inaendelea kuongezeka. Ripoti ya hivi karibuni ya Maendeleo ya Maji Duniani ya Umoja wa Mataifa iliyoratibiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni UNESCO kwa niaba ya UN-Water inakadiria kuwa watu bilioni 2.2 bado hawana huduma salama za maji ya kunywa, huku watu bilioni 3.5 wakikosa huduma salama za usafi wa mazingira.

Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema mahitaji mapya ya maji yanayohusishwa na uchimbaji wa madini yanaweza kuongeza migogoro katika maeneo ambayo tayari yanakabiliwa na ushindani wa rasilimali za maji.

Katika maeneo mengi ya migodi, mito iliyochafuliwa na kupungua kwa maji ya chini ya ardhi tayari vinatishia uzalishaji wa chakula, afya ya umma na maisha ya wananchi.

“Kutokuwa na uhakika wa maji kunaweza kudhoofisha amani, ustawi na uwezo wa jamii kuhimili changamoto,” ripoti hiyo imesisitiza, hasa katika maeneo ambayo tayari yanakabiliwa na shinikizo la mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa usawa wa kiuchumi.

Wito wa sheria madhubuti za kimataifa

Chuo Kikuu cha Umoja wa Mataifa Taasisi ya maji, mazingira na afya,  imesisitiza kuwa tatizo si mpito wa nishati safi wenyewe, ambao wataalamu wanasema ni muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, bali ni ukosefu wa uwajibikaji katika usimamizi wa mnyororo wa usambazaji wa madini hayo.

Ripoti hiyo inatoa wito wa kuwepo kwa viwango madhubuti vya kimataifa kuhusu matumizi ya maji, kuzuia uchafuzi, matibabu ya maji taka na uwazi kutoka kwa kampuni za uchimbaji madini.

Pia inazitaka serikali kuhakikisha kuwa jamii zilizoathirika zinapata taarifa kamili, zinashirikishwa katika maamuzi na zinapatiwa suluhisho pale madhara yanapotokea.

Mapendekezo hayo yanaendana na juhudi pana za Umoja wa Mataifa za kuweka haki za binadamu, ulinzi wa mazingira na usawa wa kijamii katikati ya mpito wa kimataifa kuelekea nishati jadidifu.

Jamii zinakabiliwa na madhara ya haraka

Kwa jamii zinazoishi karibu na migodi na viwanda vya kuchakata madini, athari tayari zinaonekana wazi.

Kupungua kwa maji ya chini ya ardhi kunalazimisha familia kusafiri umbali mrefu kutafuta maji, huku uchafuzi wa mazingira ukipunguza mavuno na kutishia maisha ya wavuvi na wafugaji.

Ripoti hiyo inaonya kuwa ukosefu wa ulinzi madhubuti wa mazingira unaweza pia kuongeza kutokuaminiana, machafuko ya kijamii na migogoro kuhusu ardhi na maji, hasa katika nchi zinazotarajia kunufaika kiuchumi kutokana na ongezeko la mahitaji ya madini muhimu duniani.

Utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP, unaonesha ukubwa wa changamoto hiyo, ukionya kuwa uchimbaji wa malighafi duniani unaweza kuongezeka kwa asilimia 60 ifikapo mwaka 2060 ikiwa hakutakuwa na mabadiliko makubwa katika mifumo ya uzalishaji na matumizi.

Hatua za tabianchi na haki ya maji lazima viende sambamba

Kwa kuangalia mbele, ripoti hiyo inasema mafanikio ya mpito wa nishati duniani hayatapimwa tu kwa kasi ya kuongezeka kwa matumizi ya nishati jadidifu na magari ya umeme, bali pia kwa namna dunia itakavyolinda watu na mazingira.

UNU-INWEH imehitimisha ripoti hiyo kwa kusema kuwa hatua za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na haki ya maji lazima viende sambamba ikiwa dunia inataka kuhakikisha kuwa manufaa ya mustakabali wa kijani yanagawiwa kwa usawa.

Bila usimamizi madhubuti na uwajibikaji wa haki katika matumizi ya rasilimali, ripoti hiyo inaonya kuwa mapinduzi ya nishati safi yanaweza kusababisha migogoro mipya ya kijamii na kimazingira hata wakati yanajaribu kutatua mgogoro mwingine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *