ISINGEKUWA majeraha yaliyomuweka nje mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize, alikuwa anapigiwa hesabu za kuwa mbadala sahihi wa John Bocco katika ufungaji wa mabao Ligi Kuu Bara sambamba na kuisaidia timu ya Taifa Stars, inayonolewa na kocha Miguel Ángel Gamondi.
Mzize aliyepandishwa kutoka kikosi B alikocheza mwaka 2020 hadi 2022, nyota huyo msimu uliopita 2024-2025 ndani ya Ligi Kuu Bara alihusika na mabao 19 akifunga 14 na asisti tano. Kabla ya hapo, msimu wa 2023-2024 alihusika na mabao 13, akifunga sita na asisti saba.
Mshambuliaji huyo Septemba 19, 2025 alipata majeraha ya goti wakati Yanga ikiichapa Wiliete SC ya Angola mabao 3-0, mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Tangu hapo, Mzize hakuwa katika ufiti hadi alipofanyiwa upasuaji na sasa yupo nje akiuguza majeraha yaliyomrudisha nyuma katika ushindani wa kufunga mabao.
Kiwango alichokuwa ameanza kukionyesha Mzize kimemuibua aliyekuwa mshambuliaji wa Taifa stars, Yanga na Pan Africans, Peter Tino aliyekiri alikuwa anamuona kama mbadala wa Bocco hasa timu ya Taifa.
Aliifafanua kauli yake akisema: “Miaka ya hivi karibuni aliyekuwa na muendelezo wa kufunga kila msimu Ligi Kuu alikuwa Bocco katika nafasi ya ushambuliaji, hivyo alikuwa muhimu kwa timu aliyokuwa anaichezea na Stars, ndicho nilichokuwa nakiona kwa Mzize kabla ya kuumia na ndiyo maana alikuwa anahusishwa kutakiwa na timu za ndani ya Tanzania na nje.
Ameongeza: “Mzize ni straika ninayemkubali kwa Tanzania, alipopandishwa kutoka kikosi B alikuwa na muendelezo wa kiwango chake, naamini asingekuwa anasumbuliwa angekuwa katika tatu bora ya washambuliaji wenye mabao mengi.”
Akizungumzia rekodi ya mabao ambayo Bocco ameyafunga Ligi Kuu tangu aanze kucheza akiwa Azam FC msimu wa 2008/09, anaamini endapo kama Mzize akarejea akawa fiti anaweza akawa tishio lingine.
“Ingawa mtu akitoka katika majeraha inamchukua muda kuwa fiti, lakini naamini akipata watu ambao watamjenga na yeye mwenyewe akazingatia ipasavyo matibabu na kile anachoambiwa na madaktari, atapona kwa uharaka na kurejea kuendelea na kazi yake,” amesema.
Bocco aliweka rekodi ya mabao 156 katika misimu 17 aliyocheza Ligi Kuu Bara na hakuna msimu ambao aliyowahi kutoka kapa.
Jambo ambalo Tino amesisitiza: “Ukiona mshambuliaji anafunga kila msimu hilo siyo jambo la kubeza, anajua anachokifanya, naamini Mzize atafuata nyayo hizo.”