Umoja wa Mataifa unasema uwekezaji huo utaifanya Nairobi kuwa moja ya vituo vikuu vya shughuli za kimataifa vya shirika hilo duniani, sambamba na New York, Geneva na Vienna.

UNIS Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amewasili Kenya kwa ajili ya Mkutano wa Africa Forward Summit 2026.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres pamoja na Rais wa Kenya William Samoei Ruto leo wameongoza hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi kwa kituo kipya cha mikutano pamoja na uzinduzi wa majengo mapya ya kisasa katika eneo la Gigiri jijini Nairobi. Akizungumza katika hafla hiyo Guterres amesema

“Uwekezaji huu unaakisi dhamira yetu ya kuusogeza Umoja wa Mataifa karibu zaidi na maeneo yanayoathiriwa zaidi na changamoto za kimataifa.”

Mradi huo unajumuisha majengo mapya yanayohimili mabadiliko ya tabianchi, ofisi za kisasa pamoja na ukumbi mkubwa wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua wajumbe 1,600 kwa wakati mmoja. Idadi ya vyumba vya mikutano itaongezeka kutoka 14 hadi 30 huku uwezo wa jumla wa wajumbe ukiongezeka kutoka watu 2,000 hadi 9,000.

Makao ya Umoja wa Mataifa Nairobi yalianzishwa mwaka 1972 baada ya serikali ya Kenya kutoa ekari 100 kwa ajili ya kuanzisha kuanzisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira UNEP na baadaye ekari nyingine 40 kutolewa mwaka 1975 kwa ajili ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi UN-Habitat.

Hivi sasa Nairobi ndiyo makao pekee ya sekretarieti ya Umoja wa Mataifa katika ukanda wa Kusini mwa Dunia, yakihudumia shughuli za mashirika ya Umoja wa Mataifa katika zaidi ya nchi 160 duniani.

Kwa sasa zaidi ya wafanyakazi 4,000 wa Umoja wa Mataifa wanafanya kazi katika eneo la Gigiri, huku mashirika 88 ya Umoja wa Mataifa yakifanya shughuli zake kutoka Nairobi.

UN Nairobi/Julius Mwelu Rais William Ruto wa Kenya anahutubia Mkutano waAfrica Forward Summit 2026 mjini Nairobi, Kenya.

Kwa upande wake Rais wa Kenya William Samoei Ruto amesema hatua hiyo ni ishara ya kuongezeka kwa nafasi ya Afrika katika maamuzi ya kimataifa.

“Kenya inajivunia kuwa mwenyeji wa moja ya vituo muhimu zaidi vya Umoja wa Mataifa duniani, kinachohudumia Afrika na dunia kwa ujumla.”

Makao ya Umoja wa Mataifa Nairobi yanajengwa katika eneo la ekari 140 lililotolewa na serikali ya Kenya, hatua inayotajwa kuwa mchango mkubwa zaidi wa ardhi kuwahi kutolewa kwa Umoja wa Mataifa na nchi mwenyeji.

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa Nairobi, Zainab Hawa Bangura, amesema uwekezaji huo unaonesha namna changamoto na suluhu za dunia zinavyozidi kuelekezwa Afrika.

“Nairobi si tu mji mwenyeji; ni kituo cha kimkakati cha kutekeleza kazi za Umoja wa Mataifa katika karne ya 21.”

Mbali na shughuli za maendeleo na kibinadamu, Nairobi pia ni kitovu muhimu cha hatua za kimataifa kuhusu tabianchi na maendeleo endelevu. Wakati wa ziara yake, hii Katibu Mkuu Guterres atashiriki pia mijadala ya viongozi wa Afrika kuhusu amani, maendeleo na hatua dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *