Rombo. Mzee mwenye umri wa miaka 75, Mkazi wa Mbomai juu, kata ya Tarakea Motamburu, Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro, Thomas Silayo ameuawa kwa kutenganishwa mguu na mkono  wakati wa kusuluhisha mgogoro wa ardhi baina yake na ndugu zake nyumbani kwao alikozaliwa  Kijiji cha Wama,  wilayani humo.

Tukio hilo ambalo limeibua hisia za watu  wengi ndani na nje ya kijiji hicho, limetokea Mei 8, mwaka huu nyumbani alikozaliwa Mzee huyo katika Kijiji cha Wama, kata ya Ubetu Kahe ambapo alikwenda kusuluhisha mgogoro huo wa ardhi wenye ukubwa wa ekari zaidi ya 10.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema jeshi hilo linamtafuta John Philip kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo, ambaye alitoroka.

“Mtuhumiwa huyu alimshambulia kwa kumkata na kitu chenye ncha kali baba yake mkubwa aitwaye Thomas  Silayo wakati akisuluhisha mgogoro wa mipaka ya shamba la familia na kupelekea majeraha makubwa kisha mhalifu huyo kukimbia kusikojulikana,”amesema Kamanda Maigwa.

Aidha, Kamanda Maigwa amesema Mzee huyo baada ya kujeruhiwa  alipatiwa huduma ya kwanza Hospitali ya  Huruma na baadaye alikimbizwa Hospitali ya Rufaa KCMC  ambako alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu Mei 9, mwaka huu.

Dada wa marehemu asimulia

Akisimulia tukio hilo, dada wa marehemu, Sesilia Silayo, amesema siku ya tukio kaka yake alimueleza kuwa ameitwa na ndugu zake kwenda nyumbani alikozaliwa kwa ajili ya kusuluhisha mgogoro wa shamba lao.

Amesema alipofika aliwakuta baadhi ya ndugu zake wakiwa nyumbani hapo na alikaribishwa kama ilivyokuwa kawaida licha ya kwamba hakupewa kiti.

“Siku ya tukio kaka yangu alinipigia simu asubuhi akaniambia kuwa ameitwa na ndugu zake  nikamwambia sitaki uende huko, akaniambia hapana nachukua wazee wawili niende nao nyumbani kwetu tulipozaliwa.”

“Alipofika  huko alikaribishwa vizuri lakini  hakupewa kiti, kijana  mmoja ambaye ni mtoto wa mdogo wake marehemu  aliyemkuta pale akasema ngoja niende huko nyuma ya nyumba narudi.

“Baada ya muda mfupi akawa amerudi na panga na alimzungukia kaka yangu kwa nyuma akaanza kumshambulia kwa panga,  wale wazee wengine aliyokuwa nao  wakaogopa wakakimbia, ndugu waliobaki pale wakaanza kupambana naye kwa kumlaza chini wakakata mguu na kuuweka kwenye gogo, mkono nao ukakatwa mpaka ukadondoka chini,” amedai.

Amedai baada ya kutekeleza tukio hilo walikimbilia kusikojulikana na kumwacha marehemu akihangaika kuomba msaada ndipo  baadaye walipokuja watu na kumpa msaada wa kumpeleka Hospitali ya Karume na baadaye hospitali ya KCMC ambako alifariki dunia akipatiwa matibabu.

Akizungumza Mwenyekiti wa Kijiji cha Wama, kulipotokea tukio hilo,  Jafet Tarimo, amesema tukio limewahuzunisha kwa kuwa ni miongoni mwa watu ambao walishiriki kusuluhisha mgogoro wa familia hiyo.

“Wakati tukio hili linatokea sikuwepo nyumbani, lakini hapo awali tulishakutana na kuzungumza ila baadaye tulikubaliana kuwa wanafamilia wakutane na kuzungumza, na siku hiyo ya tukio  ilikuwa ni siku ya familia kukutana. Nashangaa  baadaye napata taarifa kuwa wamekatana mapanga,” amesema Mwenyekiti huyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *