
Dar es Salaam. Hospitali ya Aga Khan imezindua rasmi kliniki ya kisasa ya uzito uliopitiliza (Comprehensive Obesity Clinic), hatua inayolenga kusaidia wananchi kudhibiti uzito na kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza yanayochangiwa na unene.
Uzinduzi huo uliofanyika Mei 12, 2026 jijini Dar es Salaam, umeelezwa kuwa sehemu ya jitihada za hospitali hiyo kuimarisha huduma maalumu za kinga na matibabu ya muda mrefu kwa wagonjwa wenye changamoto za uzito uliopitiliza.
Kliniki hiyo itatoa huduma jumuishi kupitia timu ya wataalamu wa taaluma mbalimbali wakiwemo madaktari bingwa wa mfumo wa chakula na ini, magonjwa ya moyo, mfumo wa homoni pamoja na wataalamu wa lishe.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Daktari Bingwa wa Mfumo wa Chakula na Ini Hospitali ya Aga Khan, Dk Masolwa Ngwanasayi amesema unene umeendelea kuhusishwa na ongezeko la ugonjwa wa mafuta kwenye ini (fatty liver disease), hali inayotokana na matatizo ya kimetaboli na mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.
Amesema wagonjwa wengi huhitaji tathmini ya kina ya kitabibu ili kubaini chanzo cha tatizo na kupata tiba inayolingana na hali zao.
“Unene si suala la muonekano pekee, bali ni hali ya kiafya inayohusiana na magonjwa mengi ya muda mrefu. Ndiyo maana tathmini ya kitaalamu ni muhimu kabla ya kuanza matibabu,” amesema Dk Ngwanasayi.
Ameongeza kuwa watu wamekuwa wakihangaika kudhibiti uzito bila mafanikio kutokana na kukosa mwongozo sahihi wa kitabibu, akibainisha kuwa kliniki hiyo itatoa matibabu yanayolenga mahitaji ya kila mgonjwa kulingana na hali yake ya afya.
Amesema huduma zitakazotolewa kwenye kliniki hiyo ni pamoja na tiba za kisasa, uwekaji wa puto tumboni (intragastric balloon), upasuaji wa kupunguza uzito pamoja na ushauri wa lishe na mtindo bora wa maisha.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo Hospitali ya Aga khan, Dk Nadeem Kassam amesema uzito uliopitiliza huongeza hatari ya kupata shinikizo la damu, magonjwa ya mishipa ya moyo, moyo kushindwa kufanya kazi pamoja na kiharusi.
Amesema wagonjwa wengi huanza kupata matatizo ya moyo katika umri mdogo kutokana na unene, huku akisisitiza umuhimu wa uchunguzi wa mara kwa mara na mabadiliko ya mtindo wa maisha.
Dk Kassam amesisitiza umuhimu wa uchunguzi wa afya mapema, vipimo vya mara kwa mara na kubadili mtindo wa maisha ili kuzuia madhara ya muda mrefu ya magonjwa ya moyo, hasa kwa watu walio kwenye makundi hatarishi.
Daktari Bingwa wa Mfumo wa Homoni, Dk Hanifa Mbithe amesema changamoto ya unene pia ina uhusiano mkubwa na hitilafu za homoni na michakato ya kimetaboli mwilini.
Amesema hali hiyo huathiri namna mwili unavyohifadhi mafuta, kudhibiti hamu ya kula na mwitikio wa mwili katika mabadiliko ya lishe na maisha.
“Suluhisho la kudhibiti uzito linahitaji zaidi ya kupunguza chakula. Ni lazima kufahamu chanzo cha kitabibu kinachosababisha tatizo hilo,” amesema.
Naye Mtaalamu wa Lishe, Louiza Shem amesema mafanikio ya muda mrefu katika kudhibiti uzito hutegemea mpango wa lishe unaozingatia mtindo wa maisha, utamaduni na mazingira ya mgonjwa.
Amesema wagonjwa wanapaswa kujenga tabia endelevu za kula lishe bora badala ya kutafuta njia za haraka za kupunguza uzito.
Kliniki hiyo itatoa huduma mbalimbali zikiwemo dawa, matibabu ya mfumo wa chakula na homoni, uwekaji wa puto maalum tumboni (intragastric balloon) pamoja na upasuaji wa kupunguza tumbo la chakula (bariatric surgery).
Hospitali hiyo imesema kila mgonjwa atafanyiwa tathmini ya kina ili kupata mpango wa matibabu unaoendana na historia yake ya afya, mtindo wa maisha na malengo ya kiafya.
Ripoti zinavyosema kuhusu unene
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), unene na uzito kupita kiasi hutokana na mkusanyiko mkubwa wa mafuta mwilini unaoweza kuhatarisha afya ya binadamu.
Takwimu zinaonyesha, mwaka 2019, vifo takribani milioni tano vilivyotokana na magonjwa yasiyoambukiza vilihusishwa na kiwango kikubwa cha uzito mwilini (BMI).
Kitaalamu, mtu mwenye BMI zaidi ya 25 huhesabika kuwa na uzito kupita kiasi, huku BMI ya zaidi ya 30 ikielezwa kuwa ni unene wa kupindukia.
Ripoti mbalimbali pia zinaonyesha kuwa kiwango cha watu wenye uzito kupita kiasi na unene kinaongezeka nchini Tanzania, hasa kwa wanawake, ambapo takribani asilimia 36 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 20 hadi 49 wameainishwa kuwa na uzito kupita kiasi au unene uliokithiri.
Kutokana na mabadiliko ya mfumo wa ulaji na maisha ya mijini, kiwango cha unene katika maeneo ya mijini kilifikia kati ya asilimia 30 hadi 37 mwaka 2021, huku wakazi wa mijini, watu wenye kipato kikubwa na wenye umri wa kati ya miaka 35 hadi 49 wakitajwa kuwa kwenye hatari zaidi.