
Afrika inaongoza katika fedha, kodi na tabianchi
Guterres amesema uongozi wa Afrika unasukuma mbele mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa “uliobuniwa mwaka 1945 kwa dunia ambayo haipo tena.” Ametaja nafasi kuu ya Afrika katika kufanikisha Mkataba wa Umoja wa Mataifa kwaajili ya Zama Zijazo, kuanzishwa kwa jukwaa la wakopaji ili kuimarisha uwezo wa nchi zenye madeni kujadiliana, na kuunga mkono Azimio la Sevilla linalolenga kuongeza mikopo kutoka benki za maendeleo za kimataifa pamoja na kuvutia mtaji wa sekta binafsi.
Pia ameisifu Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa maono yake ya kuunda upya mfumo wa fedha wa bara hilo, pamoja na juhudi za Afrika za kutaka Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ushirikiano wa Kimataifa wa Kodi ili kukomesha utoroshaji haramu wa fedha na kuhakikisha nchi “hazinyang’anywi tena kile kinachowastahili.”
Kuhusu tabianchi, amesisitiza kuwa nchi za Afrika pamoja na mataifa ya visiwa vidogo na nchi nyingine zilizo hatarini zimeifanya dharura ya tabianchi kuwa ajenda kuu ya dunia.
Dhuluma za kimfumo na mgogoro wa mshikamano
Licha ya uongozi huo, Guterres amekosoa mfumo wa dunia ambao “uliundwa bila Afrika na bado unaendelea kufanya kazi bila Afrika.”
Ameeleza kuwa kutokuwepo kwa kiti cha kudumu cha Afrika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ushawishi mdogo katika taasisi za fedha za kimataifa ni ishara za “dhuluma za karne nzima.”
Ameonya kuwa kupungua kwa Misaada Rasmi ya Maendeleo (ODA), bajeti za misaada na ahadi zilizovunjwa si tatizo la fedha pekee bali pia ni “mgogoro wa mshikamano.”
Aidha amesema Afrika imechangia kwa kiwango kidogo zaidi katika mabadiliko ya tabianchi lakini ndiyo inayopata ongezeko kubwa zaidi la joto kuliko wastani wa dunia, jambo linalosababisha watu kuhama makazi, kupungua kwa mazao na misukosuko ya kiuchumi. Gharama kubwa za mikopo kwa wastani mara mbili ya zile za nchi za OECD zinaondoa rasilimali ambazo zingetumika kuendeleza maendeleo, hasa wakati bara hilo lina asilimia 60 ya uwezo bora wa nishati ya jua duniani lakini linapata asilimia 2 tu ya uwekezaji wa kimataifa katika nishati safi.
Kutoka uporaji wa rasilimali hadi thamani ya haki
Guterres ametaka kukomeshwa kwa mfumo wa kihistoria ambapo madini muhimu ya Afrika yanachimbwa, thamani yake kufaidisha maeneo mengine huku uharibifu wa mazingira ukibaki Afrika.
Akirejelea mapendekezo ya Jopo la Umoja wa Mataifa kuhusu Madini Muhimu kwa Mpito wa Nishati Safi, ametaka kuwepo kwa minyororo ya thamani yenye haki, usindikaji na utengenezaji ndani ya nchi za Afrika, viwango madhubuti vya mazingira na haki za binadamu, pamoja na manufaa ya moja kwa moja kwa jamii zinazoguswa.
“Hakuna tena unyonyaji. Hakuna tena uporaji. Watu wa Afrika lazima wanufaike kwanza na zaidi kutokana na rasilimali za Afrika,” amesema.
Amesisitiza pia kuwa hatua za kukabiliana na athari za tabianchi hazipaswi tena kupewa nafasi ya mwisho, akitaka pengo la ufadhili wa mabadiliko ya tabianchi lifungwe na “ufadhili wa tabianchi wenye haki” utolewe ili nchi za Afrika ziweze kulinda watu na miundombinu dhidi ya athari zinazoongezeka za tabianchi.
Kizazi kipya, ushirikiano mpya
Akizungumza kwa Kifaransa, Guterres amesema mkutano huo ni mwanzo wa “ushirikiano mpya uliobuniwa upya na kizazi kipya” ushirikiano wa usawa, unaojengwa juu ya maslahi ya pamoja na kukamilishana.
Amesema hilo linamaanisha kuwekeza pamoja katika viwanda vinavyomilikiwa na Waafrika, kuimarisha vyuo vikuu na taasisi za utafiti za Afrika, pamoja na kujenga uwezo wa bara hilo katika akili unde (AI) ili teknolojia hiyo ijengwe kwa kutumia data, lugha, watafiti na uongozi wa Kiafrika.
Guterres amesisitiza umuhimu wa ushirikiano unaozingatia mipango ya Afrika yenyewe, ikiwemo Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), Agenda 2063 ya Muungano wa Afrika na vipaumbele vya maendeleo vya kitaifa, kwa ufadhili wenye masharti ya haki na endelevu.
Akiashiria kuwa mtu mmoja kati ya wanne duniani anatarajiwa kuwa Mwafrika ifikapo mwaka 2050, amesema mabadiliko makubwa zaidi ya karne hii ni ya kidemografia kuliko hata ya kiuchumi.
Guterres amewapongeza viongozi vijana waliohudhuria mkutano huo pamoja na mamilioni ya vijana wengine barani Afrika wanaobuni teknolojia, kulima, kujenga na kuandaa mustakabali wao huku wakidai utawala jumuishi wa kidemokrasia na taasisi zinazowajibika.
Amemalizia tarifa yake kwa kusema “mafanikio ya Afrika ni mafanikio ya dunia nzima, Afrika inapopiga hatua mbele, dunia yote inanufaika.”
Ameutaka ulimwengu kusonga mbele pamoja na Afrika “kwa kujiamini, mshikamano na matumaini ya mustakabali wa pamoja.”