
Leo, Jumanne Mei 12, 2026, anga la Kampala limetawaliwa na sura mbili tofauti, wakati upande mmoja ukiwa na shamrashamra za kitaifa za kuapishwa kwa Rais, Yoweri Museveni, upande mwingine umegubikwa na kimya kizito cha kisiasa kinachobeba swali moja, ni ipi hatima ya Uganda baada ya Museveni?
Shamrashamra zimenakshiwa na gwaride la kijeshi, milio ya mizinga ya heshima, viongozi wa Afrika wakipokelewa kwa msafara maalumu na maelfu ya wafuasi wa National Resistance Movement (NRM) wakimshangilia Museveni aliyewaongoza kwa miaka 40.
Lakini nyuma ya nyimbo za uzalendo na bendera zilizokuwa zikipepea katika viwanja vya Kololo, ukimya mzito wa kisiasa unaobeba swali moja kuu, nini hatima ya Uganda baada ya Museveni kukamilisha muhula wake wa saba?
Museveni mwenye umri wa miaka 81, ameapishwa kuanza rasmi muhula wake wa saba baada ya kushinda uchaguzi mkuu wa Januari 17, 2026 kwa asilimia 71.65 ya kura dhidi ya mpinzani wake mkuu, Robert Kyagulanyi, maarufu Bobi Wine aliyepata asilimia 24.72.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa NRM, Richard Todwong, zaidi ya wageni 40,000 wamealikwa kuhudhuria hafla hiyo, wakiwemo wakuu wa nchi zaidi ya 35, mabalozi, viongozi wa vyama vya ukombozi vya Afrika na wageni kutoka mataifa mengine.
Rais Samia Suluhu Hassan ameiwakilisha Tanzania katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na maelfu ya wananchi waliojitokeza kushuhudia uapisho huo.
Mbali na wageni hao, vyama kutoka mataifa mbalimbali pia vimealikwa, vikiwamo ANC cha Afrika Kusini, CCM cha Tanzania, Zanu-PF cha Zimbabwe, Frelimo cha Msumbiji pamoja na Rwandan Patriotic Front (RPF) cha Rwanda.
Lakini kama ilivyo kwa chaguzi nyingi za Uganda katika miaka ya karibuni, ushindi huo wa Museveni haukuja bila mabishano, bali tangu kuanza kwake hadi matokeo kumekuwa na kauli kinzani kutoka pande mbalimbali hadi kufikishana mahakamani.
…uchaguzi ulioacha maswali
Mara baada ya matokeo kutangazwa, Bobi Wine aliyapinga na kuyakataa akidai uchaguzi huo haukuwa wa haki. Alieleza kuwa kulikuwa na kuzimwa kwa mtandao, uwepo mkubwa wa wanajeshi pamoja na madai ya kutekwa kwa baadhi ya mawakala wa upinzani.
Hata hivyo, kwa upande wa Serikali na NRM, uchaguzi huo ulielezwa kuwa huru na wa kidemokrasia huku ushindi wa Museveni ukitajwa kuwa uthibitisho wa imani ambayo wananchi wa Uganda bado wanayo kwa kiongozi huyo mkongwe.
Ndani ya mvutano huo, ndipo simulizi nzima ya siasa za Uganda inapopata maana yake halisi, ambapo wataalamu wanaitaja nchi hiyo kuwa imegawanyika kati ya kizazi cha mapinduzi na kipya kilichoupokea na kulelewa ndani ya utawala wa Museveni.
Kwa nini Mei 12?
Lakini mbali na uchaguzi huo, kuna swali jingine ambalo limeendelea kuwashangaza wachambuzi wa siasa za Uganda kwa muda mrefu; kwa nini Museveni hushikilia Mei 12 kama tarehe yake ya kuapishwa kila muhula anaoshinda?
Kwa nje inaweza kuonekana ni tarehe ya kawaida ya kisiasa, lakini ndani ya historia ya Uganda, Mei 12 ina uzito mkubwa. Kwa mujibu wa Daily Monitor, Mei 12 inatajwa kuwa ni siku ambayo mwaka 1980, aliyekuwa Rais wa Uganda, Godfrey Binaisa aliondolewa madarakani na Tume ya Kijeshi ya Uganda (National Liberation Front) baada ya mgogoro wake na jeshi.
Katika tume hiyo, Museveni alikuwa Makamu Mwenyekiti chini ya Paulo Muwanga. Kuondolewa kwa Binaisa kulifungua ukurasa mpya wa siasa za kijeshi, uchaguzi wenye utata wa mwaka 1980 na hatimaye vita vya msituni vilivyomuingiza Museveni madarakani mwaka 1986.
Hivyo kwa namna fulani, Mei 12 inafafanuliwa kuwa imebeba mizizi ya safari yote ya kisiasa ya Museveni. Wataalamu wa saikolojia ya uongozi wanaamini viongozi wengi hujenga uhusiano wa kihisia na matukio yaliyowapa ushindi mkubwa au yaliyoacha majeraha ya kisiasa.
Hivyo kwa Museveni, Mei 12 inaweza kuwa zaidi ya tarehe ya kuapishwa. Inaweza kuwa ukumbusho wa ushindi, mamlaka, tahadhari dhidi ya usaliti wa kisiasa au hata hofu ya kupoteza dola.
Kwa sababu mwaka 1980, alipokuwa sehemu ya Tume ya Kijeshi iliyomuondoa Binaisa, Museveni alishuhudia kwa karibu namna mamlaka yanavyoweza kubadilishwa kwa nguvu za kijeshi.
Ndiyo maana baadhi ya wachambuzi huamini kuwa ndani ya mfumo wake wa kisiasa kuna hofu ya muda mrefu dhidi ya uwezekano wa kupinduliwa au kusalitiwa.
Anamalizia au bado yupo?
Mbali na hayo kuna swali lingine kuwa; je, huu kweli ni muhula wa mwisho wa Museveni? Hii inakuja huku akinukuliwa kuwa amesema hana nia ya kuendelea na muhula mwingine wa uongozi baada ya sasa.
Mchambuzi wa siasa, Dk Onesmo Kyauke anaamini muhula huu unaweza kutumika kuandaa kizazi kijacho cha uongozi, Museveni akimaliza na kung’atuka madarakani.
“Nadhani safari hii atajikita zaidi katika kuweka mfumo utakaobaki baada yake. Uganda imeendelea kupata maendeleo ya miundombinu na utulivu wa kisiasa kwa muda mrefu chini yake,” anasema.
Lakini si kila mmoja anaamini hivyo. Mwanahabari mkongwe na mchambuzi wa siasa, Absalom Kibanda amesema historia ya Museveni inaonyesha ishara za kutotaka kuachia madaraka.
“Mwaka 2005 nilifanya mahojiano na Jakaya Kikwete akiwa anajiandaa kuwa Rais. Wakati huo Museveni alikuwa tayari na miaka 19 madarakani. Kikwete akaingia, akahudumu miaka 10 akaondoka, lakini Museveni bado yupo hadi leo,” amesema Kibanda.
Kwa mujibu wa Kibanda, viongozi wanaokaa muda mrefu madarakani huanza kushindwa kutenganisha mfumo wa taifa na uwepo wao binafsi.
“Kwa muda aliokaa madarakani, Museveni hana jipya tena, amekaa muda mrefu kiasi kwamba hakuna jipya analotazamiwa kulifanya kwa awamu hii ya saba,” amesema.
Pamoja na lawama zote, wafuasi wa Museveni wanaendelea kumtetea kwa hoja ya utulivu na maendeleo, wakisifu kuwa katika kipindi chake cha uongozi, Uganda imeendelea kupanua miundombinu, kuimarisha usalama wa ndani na kuwa mshirika mkubwa wa operesheni za kijeshi za kikanda hususan Somalia na Afrika ya Kati.
Kwa baadhi ya wananchi waliopitia machafuko ya miaka ya 1970 na 1980, Museveni bado anaonekana kama nguzo ya utulivu wa taifa hilo. Lakini kwa kizazi kipya, hoja hiyo inaanza kugongana na kiu ya mabadiliko inayosukumwa na wanasiasa vijana akiwemo Bobi Wine.
Kingine cha kujiuliza ni je, NRM itaendelea kuwa imara bila Museveni na atamuandaa mrithi mwenye nguvu ya kuhimili mfumo alioujenga au taifa hilo litaingia katika mvutano mpya wa kisiasa siku atakapoondoka na upinzani uliojijenga kuingia ikulu?
Nyuma ya tabasamu na gwaride la kijeshi, Museveni mwenyewe anafahamu jambo moja kubwa kuliko yote; kwamba changamoto ngumu kwa watawala wa muda mrefu si namna wanavyoingia madarakani, bali namna historia itakavyowakumbuka watakapokuwa wameondoka.
Hapa ndipo wachambuzi wanaonesha hofu kuwa, huenda akaamua kuwaina tena muhula wa nane madarakani ikiwa atafika uchaguzi ujao.
“Historia inaonyesha Museveni amejiandaa kuwa Rais wa maisha Uganda, hii ya kusema hatagombea tena inawezekana haamini kama atakuwepo wakati huo, lakini muda ukiisha anaweza kugombea tena,” amesema Kibanda.