
Umoja wa Mataifa leo umezindua rasmi Ripoti ya Malengo ya Misitu Duniani 2026 , ikionya kuwa licha ya maendeleo yaliyopatikana katika uhifadhi na usimamizi wa misitu, juhudi za sasa bado hazitoshi kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ifikapo mwaka 2030.
Ripoti hiyo ya kurasa 86, imechapishwa wakati ambapo dunia imebakiza chini ya miaka mitano kufikia mwaka 2030, huku misitu ikiendelea kukabiliwa na vitisho vikubwa vinavyotokana na mabadiliko ya matumizi ya ardhi, athari mbayá za tabianchi, mioto ya misitu, wadudu waharibifu pamoja na shughuli haramu za kibinadamu.
Misitu yatajwa kuwa muhimu kwa mustakabali wa dunia
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, misitu ina mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuhifadhi bioanuwai, kuimarisha uhakika wa kupata chakula na kusaidia maisha ya mamilioni ya watu duniani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, Bjørg Sandkjær, ambaye ni Naibu Mkuu wa Idara ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa (UN DESA), amesema kuwa uwekezaji katika misitu ni uwekezaji katika uthabiti wa hali ya hewa na uchumi endelevu.
“Misitu ni muhimu katika kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu, kuanzia hatua za kukabiliana na tabianchi hadi usalama wa chakula na maisha endelevu ya wananchi,” amesema Sandkjær.
Zaidi ya hekta milioni 40 zapotea katika muongo mmoja
Ripoti hiyo inaonesha kuwa kati ya mwaka 2015 na 2025, dunia imepoteza zaidi ya hekta milioni 40 za misitu. Aidha, fedha zinazotengwa kwa ajili ya usimamizi endelevu wa misitu bado ni ndogo sana ukilinganisha na mahitaji halisi yaliyopo.
Hata hivyo, baadhi ya nchi zimeendelea kuchukua hatua chanya kupitia mageuzi ya sera, kuongeza juhudi za kurejesha maeneo yaliyoharibika, kuboresha mifumo ya usimamizi wa misitu na kuimarisha ushirikiano wa kimataifa.
Mafanikio yapo, lakini hayatoshi
Ripoti hiyo imebaini kuwa maendeleo yaliyofikiwa yanatofautiana kati ya nchi na maeneo mbalimbali duniani. Miongoni mwa mafanikio yaliyoonekana ni kuongezeka kwa maeneo yaliyohifadhiwa, mipango ya muda mrefu ya usimamizi wa misitu pamoja na mifumo ya ufuatiliaji wa rasilimali za misitu.
Kati ya malengo 26 yaliyowekwa:
- Malengo saba yamefikiwa kwa kiwango kikubwa;
- Malengo 17 yamefikiwa kwa sehemu;
- Na malengo mawili yako nyuma kabisa ya matarajio, hususan yale yanayohusu kusitisha upotevu wa misitu na kutokomeza umaskini uliokithiri kwa jamii zinazotegemea misitu.
Kasi ya utekelezaji na mapendekezo
Mkurugenzi wa Sekretarieti ya Jukwaa la Umoja wa Mataifa kuhusu Misitu, Juliette Biao, amesema changamoto kubwa sasa si kutambua umuhimu wa misitu, bali ni kuongeza kasi ya utekelezaji wa mikakati iliyopo.
“Kadri mwaka 2030 unavyokaribia, mafanikio yatategemea dhamira ya kisiasa, upatikanaji wa fedha na ushirikiano kati ya sekta mbalimbali,” amesema Biao.
Ripoti hiyo inapendekeza hatua kadhaa za haraka, zikiwemo:
- Kusitisha ukataji holela wa misitu;
- Kurejesha maeneo yaliyoharibiwa;
- Kuongeza maeneo ya misitu inayohifadhiwa na kusimamiwa kwa njia endelevu;
- Kuimarisha usimamizi wa sekta ya misitu;
- Kuziba pengo la ufadhili wa shughuli za misitu;
- Na kuanzisha mifumo bunifu ya kifedha kusaidia uhifadhi wa misitu.
Mataifa yakutana kujadili hatua zaidi
Uzinduzi wa ripoti hiyo umefungua rasmi mkutano wa 21 wa Jukwaa la Umoja wa Mataifa kuhusu Misitu (UNFF21) ulioanza Jumatatu katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, ambapo nchi wanachama pamoja na wadau mbalimbali wanakutana kujadili namna ya kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Misitu Duniani kabla ya mwaka 2030.